28.9 C
Dar es Salaam
Friday, July 19, 2024

Contact us: [email protected]

Corona yabadili vikao vya Bunge

Waandishi Wetu – Dodoma/Mikoani

KASI ya kuenea kwa maambukizi ya virusi vya ugonjwa wa corona duniani pamoja na hapa nchini, imelilazimu Bunge kubadili mfumo wa vikao vyake kuanzia leo.

Kutokana na hali hiyo, mkutano huo wa Bunge la 19 la Bajeti ambalo ni la mwisho kabla ya kuelekea Uchaguzi Mkuu  unaotarajiwa kufanyika Oktoba, kuanzia leo uendeshaji wa vikao utakuwa tofauti na ilivyozoeleka.

Kwa sasa Bunge litaendeshwa kwa saa nne kuanzia saa nane mchana hadi saa 12 jioni huku wabunge 150 kati ya 393 ndio pekee watakaoingia ndani ya ukumbi wa Bunge huku wengine wakifuatilia mijadala kwa njia ya Video Confrence katika kumbi ambazo zitakuwa zimeandaliwa.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini hapa jana, Spika wa Bunge, Job Ndugai alisema kutokana na ugonjwa wa corona kuwa ni rahisi kuambukizana, kuanzia leo Bunge litaendeshwa tofauti na mabunge ya nyuma.

Alisema kuwa Bunge litaendeshwa kwa saa nne kuanzia saa nane mchana hadi saa 12 jioni lengo likiwa ni kupunguza msongamano wa wabunge, watumishi wa Bunge na wageni ambao huenda kuangalia shughuli za Bunge.

“Ndani tuna wabunge 393, jumlisha watumishi wa Bunge na wageni, ukitazama kuna watu kama 700 kwa wakati mmoja, huu ni mkusanyiko mkubwa, itabidi tuupunguze, mkutano huu wa 19 tutakuwa na utaratibu tofauti kabisa.

“Ndani ya ukumbi wa Bunge kutakuwa na wabunge 150 kwa wakati mmoja, kutoka kwenye ile namba ya 700 sasa itashuka hadi 150 na watakaa kwa nafasi ili kupunguza uwezekano wa kugusana.

“Kwa mamlaka niliyonayo, nitakuwa ninatoa waraka kwa  wakati, kubwa ni kupunguza idadi ya wabunge na kupunguza muda wa wabunge kuwepo katika kikao kwa wakati mmoja.

“Wakati wa nyuma tulikuwa tunafanya kwa masaa tisa au zaidi, lakini kwa sasa tutafanya kwa saa zisizozidi nne,” alisema Spika Ndugai.

MWISHO WA BUNGE

Alisema mkutano huo utaanza leo na unatarajiwa kukamilika Juni 30, hivyo utaendeshwa kwa siku 64 kama siku za kazi, ukiondoa tarehe za sikukuu na mapumziko ya mwishoni mwa juma.

Spika Ndugai alisema wameandaa kumbi kadhaa ambazo wabunge watakaokosa kuingia bungeni watafuatilia kwa njia ya Video Conference.

“Tumeandaa kumbi kadhaa hapa bungeni ambazo wabunge watakuwa wakifuatilia kwa utaratibu wa Video Conference katika kumbi za Msekwa na sehemu zingine hapa hapa bungeni na kipindi ambacho wabunge hawataingia bungeni watatawanyika na kwenda katika kumbi hizo kufuatilia mkutano huo ili wafuatile kila kinachoendelea.

“Na wataweza kuchangia, kuuliza maswali kwa kutumia tablet (kishkwambi) zao na watapata majibu kupitia tablet hizo hizo na maofisa wa wizara watajibu,” alisema Spika Ndugai.

Alisema hakutakuwa na karatasi yoyote ndani ya Bunge na itatumika njia ya mtandao pekee kwani kila mbunge ana tablet yake.

“Nyaraka zote ambazo zitatumika zitawafikia wabunge na nyinyi waandishi kwa njia ya mtandao, lakini mawasiliano yote yatakuwa kwa njia ya mtandao na kila mbunge ana tablet yake.

“Nyaraka  zote zitatumwa asubuhi ya siku ambayo bajeti ya wizara hiyo inashughulikiwa.

 “Kwa hiyo asubuhi watapata randama zile na mambo mengine yote yanayotakiwa kwenye tablet zao watapitia, watatengeneza maoni yao na mchana Bunge linapoanza kama ni mchangiaji unaenda kusikiliza hotuba ya waziri halafu anaanza kuchangia.

“Hii inampa nafasi zaidi mbunge kuweza kujiandaa na kuchangia na kwenye mabunge mengi huo ndio utaratibu,” alisema Spika Ndugai.

MAWAZIRI NA VIPAZA SAUTI MEZANI

Aidha, Spika Ndugai alisema utaratibu mwingine tofauti ni kwamba mawaziri na wabunge wa upinzani watazungumza kupitia vipaza sauti ambavyo vipo katika viti vyao tofauti na zamani ambapo walikuwa wakienda mbele.

“Mawaziri wote watazungumza kutokea kwenye nafasi zao kwa kutumia ‘microphone’ yake ile ile, hakuna waziri ambaye ataenda mbele, wapinzani wataeleza mambo yao kutoka kwenye meza zao,” alisema Spika Ndugai.

Alisema pindi mbunge anapoingia ndani ya ukumbi wa Bunge akiwasha kishkwambi chake itaonyesha kwamba amehudhuria kikao cha siku husika.

MASWALI MTANDAONI

Vilevile, Spika Ndugai alisema hakutakuwa na utaratibu wa kuuliza na kujibiwa katika kipindi cha maswali na majibu kama ilivyokuwa zamani na badala yake utatumika utaratibu wa maswali na majibu kuingizwa kwenye mtandao.

“Hakutakuwa na maswali kama kawaida, maswali yote kwa siku hiyo na majibu yake yataingizwa katika mtandao wa wabunge asubuhi na majibu yake na kama mbunge aliyeuliza atakuwa na swali la nyongeza, ataandika kwenye tablet yake na kabla ya saa saba mchana majibu yatakuwa yamepatikana,” alisema Spika Ndugai.

Alisema jumla ya maswali 525 ya kawaida yanatarajiwa kuulizwa huku kila mbunge akipewa nafasi ya maswali mawili ya nyongeza kuuliza kupitia tablet yake ambapo hakutakuwa na maswali kwa Waziri Mkuu.

“Hakutakuwa na maswali kwa Waziri Mkuu kwa Bunge lote 525 maswali ya kawaida ya nyongeza, kila mbunge atauliza maswali ya nyongeza yasiyozidi mawili kupitia tablet,” alisema.

Kuhusu utaratibu wa kupiga kura wakati wa kupitisha bajeti, Spika Ndugai alisema wataweka utaratibu wa kupiga kura za ndiyo ama hapana kwa kutumia tablet za wabunge ambazo wamepewa na Bunge.

 “Kwa mbunge kubonyeza ndio au hapana katika tablet yake tutapata orodha ya wabunge waliopitisha bajeti husika. Itakuwa ni rahisi kwetu pale jioni ninapoahirisha Bunge nitakuwa naziona kura kupitia ‘screen’,” alisema Spika Ndugai.

Alisema kwenye upitishaji wa bajeti kuu wabunge watakuwa wakiingia kwa uchache kisha kupiga kura kwa sauti na baadae kutoka nje kuwapisha wengine.

“Isipokuwa siku ya bajeti yenyewe ambapo Katiba inamtaka mbunge kutamka kwa njia ya wazi ndio au hapana, tutaweka utaratibu kwenye ile siku ya bajeti wataingia wabunge wachache watakuwa wakisema ndio au hapana kulingana na utaratibu ambao utakuwa umewekwa,” alisema Spika Ndugai.

WAGONJWA WAONGEZEKA

Jana Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, alisema kuwa idadi ya wagonjwa wanaougua homa kali ya mapafu inayosababishwa na virusi vya corona (Covid-19), imeendelea kuongezeka kutoka 13 na kufikia 19.

Ummy alisema kuwa wagonjwa hao waligundulika baada ya kufanyiwa vipimo katika maabara ya taifa.

“Ninapenda kutoa taarifa kuwa leo (jana) tunathibitisha kuwepo kwa wagonjwa wapya watano wa Covid-19 baada ya kufanyiwa vipimo katika maabara ya taifa, kati ya wagonjwa hawa watatu ni kutoka Dar es Salaam na wawili kutoka Zanzibar.

“Hivyo sasa jumla ya wagonjwa wa Covid-19 nchini ni 19 akiwemo mgonjwa mmoja aliyetolewa taarifa na Waziri wa Afya wa Zanzibar, Machi 28 mwaka huu,” alisema Ummy.

Aliainisha wagonjwa walioko Dar es Salaam ambao wanaume ni wawili na mwanamke mmoja.

“Mwanaume mwenye umri wa miaka 49 Mtanzania alikutana na raia wa kigeni kutoka miongoni mwa nchi zilizoathirika zaidi, mwingine ni mwanamke mwenye umri wa miaka 21 Mtanzania ambaye ni miongoni mwa watu waliokuwa wakifuatiliwa na mwanaume mwenye umri wa miaka 49 ambaye pia ni miongoni mwa watu wanaofuatiliwa,” alisema Ummy.

Hata hivyo alisema kuwa kazi ya kuwafuatilia watu wa karibu wote waliokutana na wagonjwa hao bado inaendelea na kuwataka wananchi waendelee kuchukua tahadhari ili kujikinga na virusi hivyo.

WAGONJWA ZANZIBAR

Katika taarifa yake ya jana, Kituo cha Huduma za Dharura za Afya ya Jamii cha Zanzibar kilieleza kuwa wamebaini maambukizi kwa mtu mwingine mmoja zaidi.

Taarifa hiyo ilieleza kuwa kwa ongezeko hilo hadi jana tayari inathibitisha idadi ya watu watatu waliobainika kuambukiwa virusi hivyo vya Covid-19 katika visiwa hivyo.

Ilieleza pia kuwa tayari kuna watu 81 ambao bado wanafuatiliwa katika maeneo mbalimbali kwenye visiwa hivyo.

Taarifa hiyo ilieleza pia kuwa watu 165 wanaendelea kuwekwa kwenye karantini kuthibitishwa afya zao ili kubaini kama wamepata maambukizi hayo au la na kwamba hadi jana hakukuwa na kifo chochote kilichotokea kutokana na ugonjwa huo.

JAJI KIONGOZI NA MAHAKIMU

Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Dk. Eliezer Feleshi, amewataka mahakimu kusikiliza kesi za jinai kwa mfululizo ili kuweza kupunguza msongamano wa mahabusu na kuepuka maambukizi ya virusi vya corona.

Kauli hiyo aliitoa jana baada ya kutembelea mahakama mbalimbali za Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam kwa ukaguzi maalumu.

“Anzeni kusikiliza kesi za jinai mfululizo, itasaidia tusiwe na msongamano wa mahabusu na wale wanaostahili dhamana wapewe, hatua hii itatuwezesha kujikinga na maambukizi ya  virusi vya corona,” alisema Dk. Feleshi.

Aidha aliwataka watumishi wa mahakama kuendelea kuepukana na vitendo vya rushwa na kuzingatia maadili ya kazi zao.

Dk. Feleshi alizipongeza mahakama za mwanzo kutokuwa na mlundikano wa mashauri.

WANAWAKE ACT NA ULINZI WA WATOTO

Ngome ya Wanawake ya Chana cha ACT Wazalendo, imewakumbusha wanawake kutengeneza mazingira salama ya watoto wao ili kuwaepusha na magonjwa mbalimbali, ikiwamo ugonjwa wa corona pamoja na vitendo vya ukatili wa kijinsia.

Pia imeiomba Serikali kuongeza vifaa tiba vya kutosha kwa lengo la kupima maambukizi ya ugonjwa wa corona.

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa ngome hiyo, Mkiwa Kimwanga alisema wanatambua familia ndiyo chanzo cha ulinzi wa mtoto, hivyo ni vema kila mzazi akabeba jukumu hilo.

Mkiwa alisema watoto wana haki ya kulindwa, kuishi, kuwa na wazazi, kusikilizwa na kuwa katika mazingira salama, hivyo kuwaacha wazagae mitaani ovyo ni ukiukwaji wa malezi.

“Kwa bahati mbaya mamilioni ya watoto hawana ulinzi, kila siku watoto wengi wanakabiliwa na ukatili, unyanyasaji, utelekezwaji, unyonyaji, utengwaji na ubaguzi jambo ambalo linaleta uwezekano wa kupunguza kuishi, kukua vizuri na kufikia ndoto zao,” alisema Mkiwa.

Alisema katika kipindi hiki ambacho Serikali imesitisha masomo kwa kufunga vyuo na shule ili kuwakinga watoto na maambukizi ya virusi vya corona, ni vema wazazi nao wakawalinda.

Mkiwa alisema inashangaza kuona bado kuna baadhi ya watoto wazurura mitaani jambo ambalo linahatarisha afya zao na wazazi wanatakiwa kuchukua hatua ili kuwalinda kupata maambukizi ya ugonjwa huo.

“Katika hili tunaomba wazazi wanawake na wanaume kushirikiana kwa karibu katika malezi ya familia, ikiwamo kusimamia matumizi ya vitakasa mikono (Sanitezer) na kunawa mikono mara kwa mara,” alisema Mkiwa.

Alisema jamii inapaswa kubadilika kwa sasa na kuhakikisha suala la ulinzi na ustawi wa jamii, hasa kwa watoto  linazingatiwa kwakuwa ni haki ya binadamu ya kimataifa na kila nchi inapaswa kulifuata.

“Ripoti ya Shirika la Umoja wa Mataifa  la Mpango wa Chakula Duniani (WFP), inaeleza takribani watoto milioni 300 sasa wanakosa huduma ya mlo shuleni kwa sababu ya virusi vya corona  yaani Covid-19 na kusababisha maelfu ya shule kufungwa duniani jambo ambalo linahitaji wazazi kuimarisha ulinzi kwa watoto wao kwakuwa wao ndio walinzi wakuu.

“Ugonjwa huu unahitaji ulinzi na umakini kwa mfano familia ya Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe ipo makini lakini mtoto wao amepata maambukizi, hivyo ni jukumu la wazazi kuhakikisha wanaimarisha zaidi ulinzi,” alisema Mkiwa.

Alisisitiza kuwa ni miezi kadhaa sasa dunia imekuwa ikishuhudia kuenea kwa kasi kwa maambukizi hayo ambapo nchi 150 ikiwamo Tanzania zimeathirika na ugonjwa huo.

Hata hivyo alisema ngome hiyo inaunga mkono tamko la chama hicho linalotaka kufanyika kwa kina tathimini na udhibiti wa maambukizi ya ugonjwa huo ambayo yameathiri pia watoto na wanawake ambao ndio nguzo ya familia.

Pia wameitaka jamii kufuata ushauri na maelekezo ya wataalamu wa afya kuhusu kujikinga na maambukizi ya virusi vya corona hasa kwenye ngazi ya familia.

MSIKITI DAR WAFUNGWA

Uongozi wa Msikiti Ngazija uliopo maeneo ya Posta jijini Dar es Salaam umetoa uamuzi mgumu wa kuufunga kwa muda wa siku 21 kuanzia jana hadi Aprili 19.

Taarifa iliyotolewa na uongozi wa msikiti huo na kusambazwa kwenye mitandao ya kijamii, ilieleza kwamba uamuzi huu umechukuliwa baada ya kufanya tathmini ya hatua zilizochukuliwa mwanzoni na kutafakari hatari za mlipuko wa ugonjwa wa corona na mkusanyiko mkubwa unaofanyika wakati wa sala.

“Katika kipindi hicho cha siku ishirini na moja (21), uongozi utachukua hatua za kuweka mazingira ya kuridhisha ya kupunguza uwezekano wa maambukizo.

“Hii ni pamoja na kupulizia dawa, kuweka vitakasa mikono na vifaa zaidi vya usafi, kupunguza msongamano msikitini na sehemu ya kuchukua udhu.

“Shughuli zote za ibada zitasimama hadi tarehe hiyo na baada ya kufanya tathmini ya hali halisi wakati huo,” ilieleza taarifa hiyo.

ASKOFU ATOA WITO

Askofu Mkuu wa Kanisa la Highway of Holliness Cathedral  (HHC) la jijini Mwanza, Eugine Murisa, amesema pamoja na kuchukua tahadhari zinazotolewa na wataalamu wa afya, Watanzania ni lazima wazingatie kusimama katika imani na maombi, kuacha hofu na vitisho pamoja na kushikamana na kupendana ili kushinda vita dhidi ya ugonjwa wa corona.

Wito huo aliutoa jana kanisani kwake jijini Mwanza wakati wa ibada maalumu ya kuliombea taifa dhidi ya ugonjwa wa corona, iliyowakutanisha viongozi mbalimbali wa dini, viongozi wa Serikali wakiongozwa na Mkuu wa Wilaya ya Ilemela, Dk. Severine Ralika sambamba na waumini wengine.

Alisema kutokana na kuibuka kwa janga hilo, wapo wanaopotosha kuwa huenda huu ukawa ndio mwisho wa dunia, lakini ukweli ni kwamba huu ni ugonjwa kama magonjwa mengine yaliyowahi kuibuka na baadaye yakakosa nguvu yakiwemo ebola, Ukimwi na dengue ambayo yote Mungu alisaidia yakapita hivyo hata huu nao utapita kwa nguvu ya Mungu.

WAGONJWA ZAIDI KENYA

Waziri wa Afya wa Serikali ya Kenya, Mutahi Kagwe ametangaza wagonjwa wapya nane wa corona, na kufanya idadi ya wagonjwa nchini humo kufikia 50.

Kwa mujibu wa gazeti la Daily Nation, Waziri Kagwe alisema jana kuwa wagonjwa hao nane waliambukizwa virusi vya corona ndani ya nchi na kutoa tahadhari ya ugonjwa huo kuenea ndani kwa kuwa hakuna maambukizi mapya kutoka nje.

Hadi Jumamosi, Kenya ilikuwa na wagonjwa 38. Juzi Jumapili Kagwe alitangaza wagonjwa wapya wanne na kufanya idadi kufikia 42, hivyo idadi ya wagonjwa wapya 12 nchini humo imetangazwa ndani ya siku mbili. Mgonjwa wa kwanza aliripotiwa nchini Kenya Machi 13. Mtu mmoja tayari amepoteza maisha nchini humo kutokana na virusi hivyo.

HABARI HII IMEANDALIWA NA RAMADHAN HASSAN (DODOMA), YOHANA PAUL (MWANZA), ANDREW MSECHU, AVELINE KITOMARY NA CHRISTINA GAULUHANGA (DAR ES SALAAM)

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles