LIBREVILLE, GABON
BAADA ya Senegal kutolewa kwenye michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika nchini Gabon katika hatua ya robo fainali dhidi ya Cameroon, kocha wa timu hiyo, Aliou Cisse, amewaomba radhi wachezaji wa timu hiyo na mashabiki kwa kushindwa kusonga mbele.
Senegal imetolewa kwa kichapo cha mabao 5-4 ya mikwaju ya penalti, baada ya dakika 90 kumalizika kwa suluhu, hivyo kocha huyo amesema hawakuwa na bahati ya kusonga mbele hatua inayofuata.
“Haikuwa jambo rahisi kutolewa, ni jambo la kusikitisha sana kwa taifa ambalo lilikuwa linatarajia kuona makubwa kutoka kwetu, naomba radhi kwa wachezaji ambao walikuwa na lengo la kutaka kuweka historia mpya katika maisha yao ya soka.
“Najua taifa nalo lilikuwa na matumaini makubwa ya kuiona timu yao ikifika mbali na hata kuchukua ubingwa lakini mambo yamekuwa tofauti, hivyo naomba radhi kutokana na matokeo hayo tuliyoyapata.
“Nitakuwa mtu wa kwanza kuhisi maumivu ya watu wa Senegal baada ya kutolewa, wachezaji wangu walipambana kwa kiasi kikubwa kuanzia mwanzo hadi mwisho wa dakika 90, lakini kwenye matuta hatukuwa na bahati hiyo,” alisema Cisse.
Kocha huyo amedai kuwa, kuna wachezaji walishindwa kuonesha uwezo wao binafsi mara baada ya timu kushindwa kucheza pamoja.