Na Dennis Luambano, Dar es Salaam
HELIKOPTA iliyobeba makada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) ikitokea Dar es Salaam kwenda Njombe imeanguka ndani ya Pori la Akiba la Selous lililopo eneo la Kilombero mkoani Morogoro.
Akitoa taarifa za ajali hiyo kwa MTANZANIA jana, Meneja wa Selous, Benson Kibonde, alisema helikopta hiyo ilianguka karibu na Mto Ruaha katika Kitalu cha Uwindaji cha R3.
“Ajali hiyo imetokea jana jioni na tulipata taarifa kwa njia ya simu ya satellite kutoka kwa professional hunter (mwindaji) mmoja ambaye alisema akiwa katika hema lake ndani ya Pori la Selous katika Kitalu cha R2 alisikia kishindo cha helikopta ikianguka na kutoa moshi katika upande wa Kitalu cha R3,” alisema Kibonde.
Alisema baada ya ajali hiyo kutokea, mwindaji huyo pia alitoa taarifa kwa Kampuni ya Uwindaji ya Foa Adventure ambayo imempeleka katika pori hilo.
Alisema kutokana na eneo hilo kuwa karibu na Mto Ruaha ilikuwa ni vigumu kwao kwenda kwa kuwa usiku ulishaingia.
“Si rahisi kwenda eneo lile nyakati za usiku kwa sababu usiku ulishaingia na kwa mazingira yalivyo ni vigumu na sisi tumeamua askari wetu wa wanyamapori wataenda asubuhi katika eneo lilipotokea ajali hiyo,” alisema Kibonde.
Hata hivyo, MTANZANIA lilipata taarifa kuwa miongoni mwa makada waliokuwamo katika helikopta hiyo alikuwa ni mgombea ubunge wa Jimbo la Ludewa kwa tiketi ya CCM, Deo Filikunjombe.
MTANZANIA lilimtafuta Mathias Luoga ambaye ni Msaidizi wa Filikunjombe na alisema katika helikopta hiyo kulikuwa na abiria watatu na rubani mmoja.
“Saa 10 jioni ya jana, Filikunjombe alikuwa anatokea Dar es Salaam kwenda Njombe lakini wakiwa angani helikopta yao ikapata hitilafu wakiwa eneo la Kilombero na kuanguka katika Mbuga ya Selous.
“Lakini eneo ilipoanguka helikopta hiyo hakuna mtandao wa simu unaopatikana kwa hiyo mawasiliano yamekuwa magumu ndiyo maana hawajapatikana na askari wanyamapori walisema watawatafuta,” alisema Luoga.
Katika hatua nyingine, MTANZANIA lilimtafuta Filikunjombe kupitia simu yake ya mkononi ambayo iliita kwa muda mrefu bila kupokelewa kisha baadaye haikupatikana.