25.5 C
Dar es Salaam
Saturday, May 18, 2024

Contact us: [email protected]

Magufuli kuwasainisha mikataba mawaziri wake

g2-3NA BAKARI KIMWANGA, DAR ES SALAAM

MGOMBEA urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. John Magufuli, amesema kama atafanikiwa kuingia madarakani, atawasainisha mikataba maalumu ya kazi mawaziri wake kabla ya uteuzi.

Amesema lengo la kufanya hivyo ni kuhakikisha anakuwa na mawaziri wanaokwenda kwa wananchi badala ya kukaa ofisini wakiandika madokezo.

Dk. Magufuli alitoa kauli hiyo jana kwa nyakati tofauti katika mikutano yake ya kampeni wilayani Kisarawe, Mkoa wa Pwani na Ukonga, Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa Dk. Magufuli, atalazimika kufanya hivyo kwa kuwa anahitaji kuunda Serikali itakayokuwa na mawaziri walio tayari kulitumikia taifa kwa uadilifu.

“Kauli za watu kuniita mkali zinatokana na msimamo wangu katika kusimamia rasilimali za nchi, kwani nahitaji kuwa na wasaidizi waadilifu na wenye hofu ya Mungu.

“Jamani Magufuli ndiye rais wa awamu ya tano, kwa sababu Watanzania wameamua. Ndiyo maana nasema hapa mchana huu, kwamba nitateua mawaziri wachache nitakaowasainisha mikataba maalumu ya kazi.

“Kabla ya uteuzi, nitakuuliza, unaweza kazi? Sitaki waziri wa kukaa ofisini kazi yake kuandika madokezo tu.

“Kama ni mradi wa barabara uende ukaziangalie na kama ni miradi ya maji, pia uende ukaiangalie siyo kukaa ofisini,” alisema Dk. Magufuli.

Kutokana na kujipambanua kwamba anapinga ufisadi, alisema kuna baadhi ya watu wamekuwa wakimchukia kwa msimamo huo, lakini hataacha kuwaambia ukweli Watanzania.

“Mimi napinga ufisadi na nimekuwa mwana CCM mzuri tu na mwaminifu kwa chama change, ndiyo maana hamjasikia hata siku moja nimefukuzwa au kukaripiwa, mimi kwangu ni kazi tu,” alisema.

Pia, alisema anawashangaa baadhi ya wanasiasa wanaosema Serikali ya CCM haijafanya chochote katika miaka 54 ya uhuru.

“Hawa watu ni wa ajabu, leo wanasema hakuna kilichofanyika wakati wao walikuwa viongozi wakuu kwa miaka 10 na mwingine miaka miwili.

“Kama wangejua, wale marais wa awamu ya tatu na nne wangenichagua mimi kwenye uwaziri mkuu, badala ya wao,” alisema.

Kuhusu milipuko ya mabomu katika kambi ya Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ), Gongo la Mboto jijini Dar es Salaam mwaka 2011, alisema anajua kuna baadhi ya wakazi wa Ukonga ambao nyumba zao ziliathiriwa na milipuko hiyo, hawajalipwa haki zao.

Kutokana na hali hiyo, alisema atahakikisha anasimamia haki zao na hakuna atakayekosa haki zake kwa mujibu wa sheria.

 

FOLENI DAR

Dk. Magufuli ambaye pia ni Waziri wa Ujenzi, alisema moja ya mkakati wa Serikali yake ni kujenga barabara za juu (fly over) saba zitakazopunguza foleni jijini Dar es Salaam.

Alisema hivi sasa Serikali ipo kwenye mchakato wa kuhakikisha miradi hiyo inatekelezwa kwa wakati ili wananchi waweze kuondokana na kero hiyo.

Katika hilo, jana mchana alisimamia utiwaji saini wa ujenzi wa fly over katika eneo la Tazara itakayojengwa na kampuni ya Japan.

Kuhusu eneo la Ubungo, alisema itajengwa barabara ya njia tatu ambayo Benki ya Dunia imeshatoa Sh bilioni 80 kwa ajili hiyo.

Pamoja na hayo, alisema Serikali yake itapanua barabara ya kutoka Dar es Salaam kwenda Chalinze na kuwa ya njia sita ili kukabiliana na ongezeko na magari.

“Kwahiyo, ninaomba urais kwa sababu nafahamu Tanzania ilipotoka, ilipo na inapoelekea,” alisema Dk. Magufuli.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
587,000SubscribersSubscribe

Latest Articles