22.5 C
Dar es Salaam
Sunday, July 21, 2024

Contact us: [email protected]

Chongolo: Serikali iendelee na mchakato uwekezaji bandari

Na Nora Damian, Mtanzania Digital

Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimeielekeza Serikali kuendelea na mchakato wa uwekezaji wa bandari huku ikisikiliza maoni yenye dhamira njema na kuyachukua ili yaongeze tija.
Kimesema kinachofanywa na Serikali ni utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ambayo inatakiwa ifikapo mwaka 2025 mambo yote yawe yametekelezwa.

Hayo yamesemwa leo Julai 29,2023 na Katibu Mkuu wa CCM, Daniel Chongolo, wakati wa mkutano wa hadhara uliofanyika Uwanja wa Tanganyika Pakers, Dar es Salaam na kuhudhuriwa pia na viongozi wa Mikoa ya Pwani na Morogoro.

“Sisi ndio tuliahidi, dhamira ya Chama Cha Mapinduzi ni kuhakikisha tunapata fedha za kutosha kwenye kila chanzo cha muhimu ili zitusaidie kukimbiza utekelezaji wa ilani lakini kubwa kutatua changamoto za wananchi.

“Tunachozungumzia wengine wanaita mkataba, wengine wanaita makubaliano, lakini kisheria hayana tofauti, makubaliano si msaafu, kurekebishwa neno, sentensi au maana inawezekana.

“Kama kuna mtu ana mstari ambao ukiwekwa utaleta maana nzuri alete tutoke na kitu bora ambacho kikienda kutekelezwa kitatuongezea tija kubwa, masilahi ya nchi yatakuwa yamelindwa zaidi na tutatekeleza ilani kwa kasi zaidi,” amesema Chongolo.

Naye Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Atupele Mwakibete, amesema Tanzania inashindana na nchi jirani ambazo zimeizidi kwa kila kitu hali inayosababisha baadhi ya wafanyabiashara kuacha kuitumia Bandari ya Dar es Salaam na kutumia nyingine.

“Magati tunayo 12, wenzetu wa Mombasa wana gati 28, Afrika Kusini wana magati 58, katika magati 12 tuliyonayo meli zinazoweza kushusha kwa wakati mmoja ni tisa peke yake…mfanyabiashara anaweza asipitishe bidhaa zake kwa sababu magati machache na vifaa hatuna vya kutosha,” amesema Mwakibete.

Mwanasiasa Mkongwe, Stephen Wasira, amesema bandari ni mpaka kati ya Tanzania na nchi nyingine hivyo hakuna anayeweza kuiuza.

“Mwaka 1979 tulipigana vita vya Kagera kwa sababu sehemu ya mpakani ilichukuliwa na adui, sasa kama unaweza kupigana kwa ajili ya kipande cha ardhi ya Kagera utauzaje bandari?” amehoji Wasira.

Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma (PIC), Jerry Silaa, amesema maoni mengi waliyoyapokea yanatengeneza uangalizi kwenye mikataba ambayo bado haijasainiwa.

“Maoni bado yanapokelewa, kila Mtanzania mwenye maoni ambayo anaamini yataboresha anakaribishwa na Serikali ni Sikivu, yote yatafanyika katika kulinda masilahi ya Mtanzania,” amesema Silaa.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Mipango na Uwekezaji), Profesa Kitila Mkumbo, amesema mkataba huo unarekebishika kwani ibara ya 22 inaruhusu kufanya marekebisho hivyo Serikali itazingatia maoni yao na kuyafanyia kazi.

“Mkataba huu si vitabu vitakatifu, Serikali haijasaini biblia wala Quran, imesaini mkataba, mikataba yote duniani huwa inarekebishika na katika mkataba huu ipo ibara ya 22 ambayo inaruhusu marekebisho…kwahiyo Serikali haina tatizo na wataalam na Watanzania wenye nia njema,” amesema Profesa Mkumbo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles