28.7 C
Dar es Salaam
Thursday, February 22, 2024

Contact us: [email protected]

CHONDECHONDE WABUNGE MSIRUDIE MAKOSA

Na Dennis Luambano, Dar es Salaam

VIKAO vya Mkutano wa Sita wa Bunge vinatarajiwa kuanza Januri 31, mwaka huu.

Pamoja na mambo mengine, mjadala mkubwa katika vikao hivyo utajikita katika hoja za namna Serikali ilivyotekeleza bajeti yake ya mwaka wa fedha wa 2016/2017.

Licha ya mjadala huo mkubwa, inadaiwa kuwa baadhi ya wabunge hasa wa vyama vya upinzani wanaounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) wamevipania vikao hivyo na pengine wanaweza kuvitumia kujadili mwenendo wa siasa za nchi hasa ikizingatiwa kuwa bado hawaruhusiwi kufanya mikutano ya hadhara, huku kukiwa na zuio la matangazo ya vikao hivyo kutorushwa moja kwa moja (live) na vituo vya runinga.

Kukazia hoja hiyo ni kwamba Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe, alinukuliwa Ijumaa ya wiki iliyopita akilalamika kuwa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) ambacho ni chama kikuu cha upinzani nchini, kina hofu kubwa kuhusu viongozi wao kuanzia wale wa kitaifa, wabunge, madiwani, wenyeviti wa vijiji, wenyeviti wa mitaa, vitongoji na wanachama wao kutotendewa haki.

“Kuna watu wana hofu ya uhaba wa chakula, kuna wenye hofu ya kuporomoka kwa uchumi, kuna watu wana hofu za kiusalama, sisi kama chama kikuu cha upinzani tuna hofu kubwa kuhusu usalama wa viongozi wetu, tuna hofu kubwa kuhusu kutokutendewa haki viongozi wetu kuanzia viongozi wa kitaifa, kwenda kwa wabunge, madiwani, wenyeviti wa vijiji, mitaa na vitongoji na wanachama wetu.

“Tumeona namna viongozi wanavyohukumiwa vifungo katika mazingira yasiyo ya kawaida katika historia ya vyama vingi katika nchi yetu, tunaona namna mahakama nayo tuliyoiamini kwa muda mrefu ni kimbilio la Watanzania wanyonge kutafuta haki lakini sasa tunaona inaamua kufunga viongozi waliochaguliwa na wananchi na wengine wananyimwa dhamana katika makosa yanayostahili dhamana,” alinukuliwa Mbowe.

Kutokana na kauli hiyo ya Mbowe, ni dhahiri sasa Ukawa watavitumia vikao hivyo kufanya siasa kwa kujenga hoja mbadala za kuikosoa Serikali na kwa kuwa havitaonyeshwa ‘live’ wakati majadiliano yakiendelea bila shaka tutarajie baadhi ya video zikisambaa katika mitandao ya kijamii hasa WhatsApp zikiwaonyesha wabunge wakitoa hoja zao bungeni.

Huku miongoni mwa wabunge hao wakiwamo wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) au wale wa Ukawa wakitoa hoja zenye tija na wengine hazina tija.

Kama hivyo ndivyo na kwa kutumia uzoefu wa kuchambua mwenendo wa hoja za baadhi ya wabunge, naweza kubashiri kwamba baadhi yao watapwaya na watafanya makosa yale yale waliyoyafanya katika vikao vya Bunge la mwaka jana.

Kwamba matusi, kebehi, chuki, ubaguzi, vitisho, fitina, uongo na ubabe vilivyotawala katika Bunge la mwaka jana pengine ndiyo hayo hayo yatakayojirudia.

Chonde, chonde msirudie kufanya hivyo, yaani chupa iwe ile ile na mvinyo uwe ule ule kwamba hakuna kitakachobadilika kwa sababu ni wabunge wachache watakaojadili hoja za kitaifa, huku wengine wakijadili mambo ya watu binafsi.

Kwamba wabunge wa CCM na wale wa Ukawa watakita miguu chini kuhakikisha itikadi za vyama vyao kwanza na mengine yatafuata baadaye.

Hakuna atakayekubali kuwa chini ya mwenzake na hilo litaonekana hata katika hoja zilizo wazi kabisa. Vikao hivyo vikianza watavutana na kusigana na wataligeuza Bunge kuwa jukwaa la kufanya siasa badala ya kuwa chombo cha uwakilishi na kutunga sheria. 

Kwamba kwa kuwa mbunge fulani ni kutoka Ukawa au kwa kuwa mwingine anatoka CCM, basi lazima apingwe hata kama hoja anazozitoa zina mantiki kitaifa.

Kutokana na ubinafsi huo, ndiyo maana baadhi ya wabunge watatumia zaidi migogoro ya ardhi, kero za maji, uhaba wa dawa hospitalini, vituo vya afya na ubovu wa miundombinu ili kujijenga kisiasa kwa kutoa hoja kinzani hata pale wasipostahili.

Si hivyo tu, pia nina wasiwasi kwamba pengine vikaibuka vituko katikati ya vikao hivyo wakati mijadala ikiendelea kwa sauti na video za baadhi ya wabunge kusambaa mitandaoni ikionyesha namna wanavyotoa maneno ya kebehi na dharau wakati wenzao wakitoa michango yao.

Kutokana na maneno yao, nina shaka kwamba kuna baadhi ya Watanzania wataacha kabisa kufuatilia mijadala ya Bunge hilo kupitia magazeti.

Kuna sababu kadha wa kadha zitakazowafanya kutolifuatilia, huku iliyo kubwa ni kuona baadhi ya wabunge wakilinajisi Bunge hilo kwa kuangalia masilahi ya vyama vyao.

Sababu ya kwanza ni kwamba baadhi yao wataangalia zaidi masilahi yao na ya vyama vyao kuliko masilahi ya wapiga kura wao.

Kwa hiyo watashindwa kufanya kile walichotumwa kwa sababu walichaguliwa kwenda bungeni kuwawakilisha wapiga kura wao lakini kazi hiyo itawashinda.

Binafsi natarajia kushindwa kwao kwa kuwa siku zote huwa siwaamini wanasiasa kama kweli wana nia njema na Watanzania katika baadhi ya mambo.

Ndiyo, hawana nia njema na sisi na katika mambo ya msingi wameendelea kuhubiri utofauti wa itikadi za vyama vyao badala ya kuhubiri masilahi mapana ya Tanzania yetu.

Kuthibitisha ninachokisema ni kurudia ubashiri wangu kwamba yatakayofanywa katika vikao hivyo na baadhi ya wabunge ndiyo hayo hayo watakayoyafanya kwa muda wa miaka mingine mitatu ijayo, kwa maana hadi tutakapokaribia Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020. Kwa sababu kazi zao za kibunge watazifanya kwa mazoea.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
583,000SubscribersSubscribe

Latest Articles