23.3 C
Dar es Salaam
Wednesday, April 24, 2024

Contact us: [email protected]

TRUMP ACHOTA ‘HEKIMA’ ZA MAGUFULI

Na Mwandishi Wetu,

SITAWAANGUSHA. Ndilo neno ambalo lilitawala katika hotuba ya Rais mpya wa Marekani, Donald Trump, wakati akiapishwa Januari 20, mwaka huu katika viwanja vya Capitol Hill mjini Washington DC.

Zilikuwa dakika 15 ambazo zilionyesha dira ya uongozi wake, akiwa na matamshi mazito kuanzia uongozi uliopita na matumaini mapya kwa wananchi wa taifa hilo kubwa kiuchumi duniani.

Hotuba ya Rais Trump haina tofauti sana na kauli za Rais Dk. John Magufuli, ambazo amekuwa akizitoa mara kwa mara katika ziara zake tangu alipokabidhiwa kuongoza Serikali ya Awamu ya Tano. Makala haya yanaangalia maudhui ya hotuba za Trump zinavyofanana na Magufuli.  

HAPA KAZI TU

Mchanganyiko wa hotuba ya Trump umetengeneza mseto wa kile ambacho kilisemwa na kusisitizwa na Rais wa Tanzania, John Magufuli kwamba ‘Hatawaangusha’ na kwamba huu si muda wa maneno wala utani bali ni wakati wa ‘Hapa Kazi Tu’.

Kudhihirisha jambo hilo, Trump anasema: “Kuanzia sasa chochote tukachofanya ni kwa masilahi ya Marekani. Uamuzi wowote juu ya biashara, kodi, uhamiaji na sera za nje, utakuwa kwa manufaa ya wafanyakazi, wananchi wa Marekani na familia zao.

“Tutalinda mipaka yetu kuhakikisha nchi nyingine hazitengenezi bidhaa zetu, wala kuiba katika kampuni zetu na kuchukua ajira zetu. Kulinda rasilimali zetu utakuwa mpango bora. Nitatumia kila pumzi yangu mwilini kupigania masilahi yenu. Nawahakikishia sitawaangusha.

“Marekani itaanza kupaa tena, kushinda kuliko awali. Tutarejesha ajira zetu. Tutalinda mipaka yetu. Tutarudisha utajiri wetu. Na tutafanikisha ndoto zetu. Tutajenga barabara mpya chini na juu, madaraja, viwanja vya ndege, reli katika taifa hili lenye mengi ya ajabu.”

WAPIGA DILI

Sehemu nyingi ambayo kuna mfanano mkubwa kati ya marais hawa wawili ni pale wanapowazungumzia wapiga dili walivyodhoofisha maisha ya wananchi.

Magufuli amekuwa akipaza sauti akidai sasa ni wakati wa kuhakikisha wananchi wanapatiwa huduma muhimu na maendeleo. Aidha, anasema ni wakati wa kuwatumikia wananchi hivyo wapigadili na wanasiasa wasioitakia mema nchi hii hawana nafasi tena.

Trump katika hotuba yake kwa tafsiri ya Kiswahili isiyo rasmi, anasema: “Kwa muda mrefu kulikuwa na kundi dogo likinufaika na mtaji wa nchi hii na kuinyima fedha halali Serikali wakati mamia ya watu wakiishi kwa shida. Kundi hili lipo Washington, watu hawakunufaika na keki ya taifa.

“Wanasiasa walisababisha ajira ziondoke nchini (Marekani) na viwanda vikafungwa. Wana mtandao wanajilinda wenyewe, lakini hawajali mustakabali wa wananchi. Ushindi wao haukuwa ushindi wenu; mafanikio yao hayakuwa mafanikio yenu na wakati wakinufaishwa na fedha za nchi hii, kulikuwa na mambo madogo ya kushangilia kwa familia ambazo zilikabiliwa na matatizo chungu mzima.”

UMASIKINI

Rais Magufuli amesikika mara kadhaa akitumia maneno haya; ‘wananchi wa hali ya chini’, ‘wananchi wa kawaida’ na ‘watoto wa masikini’. Maneno hayo yameibua hisia kwamba kiongozi huyo amekuja kuwatumikia Watanzania. Na mara kadhaa amesema hayupo tayari kuona mtu, kiongozi au mwanasiasa yeyote anamkwamisha. Magufuli alisisitiza kuwa yeye hajaribiwi.

Maneno kama hayo yametamkwa na Trump kwenye hotuba yake. Akizungumzia suala la umasikini nchini Marekani, Trump alisema: “Hii ni kuwathibitishia kuwa kila mwananchi ana haki. Lakini wananchi wengi wanaishi katika mazingira tofauti ya uhalisi. Akina mama na watoto wamezingirwa na umasikini ndani ya miji yao.

“Hapa ninapokula kiapo, ninafahamu kuwa miongo kadhaa iliyopita tumekuwa nyenzo ya mafanikio ya viwanda vya nje kwa gharama ya maisha ya Wamarekani. Tumekuwa tukipeleka majeshi yetu kulinda mipaka ya nchi nyingine na kutumia trilioni za dola, halafu tukashindwa kulinda mipaka yetu.”

VIWANDA

Katika hotuba yake, Trump alisisitiza suala la kurejesha nguvu katika viwanda nchini humo, ambapo alizituhumu Serikali zilizopita na wanasiasa kushindwa kusimamia ajira viwandani ili zisaidie wananchi.

Trump anasema: “Moja kwa moja, viwanda vyetu vilifungwa na kuacha pengo la ajira pamoja na mamilioni ya wafanyakazi wa Marekani wakiachwa gizani. Tabaka la kati limekuwa kwenye wakati mgumu maeneo mbalimbali. Hayo yamepita. Sasa tunatazama maisha ya baadaye.”

Kauli za viongozi hao zinaonyesha dhahiri misimamo yao katika nchi wanazoziongoza.

Rais Donald Trump ameshika nafasi hiyo wiki iliyopita kutoka kwa Rais Mstaafu Barack Obama, huku Rais Dk. John Magufuli akiwa madarakani kwa zaidi ya mwaka mmoja nafasi iliyokuwa inashikiliwa na Rais Mstaafu Jakaya Kikwete.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles