30.2 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

CHID BENZ NI ZAIDI YA SIKIO LA KUFA!

Na CHRISTOPHER MSEKENA

KATIKATI ya wiki, Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoa wa Dodoma, Gilles Muroto alikutana na waandishi wa habari na kutoa taarifa ya kukamatwa kwa rapa, Rashid Makwilo ‘Chid Benz’ na wenzake watatu wakiwa na dawa za kulevya zinazodhaniwa ni Heroine, Desemba 30, mwaka jana mkoani humo.

Chid Benz na wenzake watatu akiwamo meneja wa msanii Pam D, Gilla The Boss walikamatwa katika kituo cha mabasi, Dodoma walipokuwa kwenye maandalizi ya kwenda kufanya shoo ya funga mwaka mkoani Mwanza.

Katika taarifa hiyo Kamanda Muroto aliwaasa wasanii na jamii kwa ujumla kuwa sanaa ni uwanja wa burudani na elimu na siyo ulingo wa kufanya uhalifu hivyo waache tabia ya kujihusisha na dawa za kulevya.

UNAKUMBUKA HII?

Baada ya kufahamika kuwa Chid Benz hayupo kwenye muziki kwa sababu ya kuanza kutumia dawa za kulevya, mwezi Machi mwaka juzi, meneja Babu Tale na Kalapina walifanikiwa kumshawishi na kumpeleka kwenye kituo cha Life and Hope Rehabilitation kilichopo Bagamoyo ili kumsaidia kuacha matumizi ya dawa hizo.

Baada ya matibabu, rapa huyo alirudi tena kwenye ubora wake huku akiwa na kiu ya kufanya kazi za muziki na kufanikiwa kuachia nyimbo kadhaa ukiwemo ule wa Chuma aliomshirikisha Rayvanny.

Tetesi za kurudia dawa za kulevya zilisambaa mtaani, mwezi Desemba mwaka juzi zikiambatana na picha mbaya zinazomwonyesha akiwa amedhoofu, lakini mwenyewe aliibuka na kudai hafanyi tena michongo hiyo.

Akadhibitisha hilo mwezi Agosti mwaka jana katika tamasha la Usalama Barabarani lililofanyika kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam ambapo yeye na Q Chief waligonga bonge la shoo kwa kutumbuiza kibao chao kiitwacho ‘Muda’  na wimbo wake maarufu Dar es Salaam Stand Up.

ALIWAHI KUKAMATWA ILALA, AIR PORT

Lakini baada ya tamasha hilo, Kamanda wa Polisi mkoani wa kipolisi Ilala, Salum Hamdun alitangaza kuwa katika msako walioufanya Agosti 12, mwaka huo, Chid Benz na wenzake sita walikamatwa na dawa za kulevya aina ya Heroine.

Itakumbukwa kuwa Oktoba 24, mwaka 2014, Chid Benz alikamatakwa na dawa za kulevya katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es salaam akijaribu kuvuka nazo kwenda jijini Mbeya kwenye tamasha la Instagram Party.

AKWEPA KIFUNGO

Baada ya uchunguzi, Chid alifikishwa mahakamani ambapo alikiri shitaka hilo na Februari 26, 2015, Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu ilimhukumu kifungo cha miaka miwili jela au faini ya shilingi laki 9 baada ya kupatikana na hatia ya makosa matatu likiwamo la kukutwa na dawa za kulevya aina ya bangi na heroine zenye thamani ya Tsh. 40,358, alifanikiwa kukwepa kifungo baada ya kulipa faini.

CHID BENZ TENA DODOMA

Ndiyo maana taarifa za kukamatwa kwake mkoani Dodoma ziliposambaa zimezua gumzo kubwa wiki hii kwani ni mara yake ya tatu kutiwa nguvuni na vyombo vya dola kwa tuhuma hizo.

Kamanda Muroto amesema jalada lake lipo kwa mwanasheria wa Serikali linachunguzwa na uchunguzi ukikamilika atafikishwa mahakamani.

KISHERIA INAKAAJE?

Swaggaz limemnasa mwanasheria maarufu nchini, Jebra Kambole kutoka kampuni ya Law Guards Advocates ambaye anaelezea ishu hii ya Chid Benzi ilivyokaa kisheria.

“Kimsingi sheria ya kuzuia dawa za kulevya ambayo ni sheria namba 5 ya mwaka 2015 ambayo imeanza kutumika mwezi Mei 2015 inakataza matumizi ya dawa za kulevya kwa kile kiwango kidogo, kama hizo kete mbili ni miongoni mwa viwango vidogo.

“Ambapo kifungu cha 17 (A ) kinakataza mtu yeyote kutumia, kuhifadhi au kufanya matumizi yake binafsi kwa mtindo huo na adhabu yake ni faini ambayo haipungui shilingi milioni 1 au kifungo kisichozidi miaka mitano au vyote kwa pamoja,” alisema Kambole.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles