NA SAMWEL
MWANGA
SERIKALI imesema watoto wanaozaliwa na mtindio wa ubongo na kuharibika mimba
kwa kina mama ni miongoni mwa athari zinazotokana na kukosekana
matumizi ya chumvi yenye madini joto.
Kauli hiyo ilitolewa juzi na Mratibu wa Lishe Mkoa wa Simiyu, Dk. Chacha Magige alipotembelea mgodi wa chumvi uliopo katika kijiji cha Nyalanja wilayani humo kufahamu athari zinazotokana na matumizi ya chumvi isiyo na madini joto.
Dk. Magige
alisema ni lazima kwa wachimbaji hao wa chumvi
kuboresha biashara ya chumvi kwa kuongeza madini joto kukuza soko na kuwaepusha watumiaji na
madhara ya kiafya.
Alisema wamekuwa wakifanya ziara ya mara kwa mara katika mgodi huo na
kukutana na wachimbaji hao na kila mara huwakumbusha madhara ya kutumia
chumvi isiyo na madini joto kwa sababu kuna madhara zaidi ya 104 yanayosababishwa
na ukosefu wa madini hayo.
“Athari zinazotokana na kutotumia chumvi yenye madini joto ziko nyingi
mojawapo ndiyo hiyo kwamba tunapata watoto ambao wana mtindio wa ubongo, watoto
hawakui vizuri ule udumavu wa watoto lakini pia kuna kuharibika kwa mimba kwa kinamama
wajawazito,”alisema.
Aliwataka wazalishaji wa chumvi kuhakikisha wanaweka madini joto kuepuka kuwasababishia walaji madhara kwa vile
madini hayo hutolewa bure bila gharama
yoyote pamoja na wananchi kuitumia vizuri elimu ya matumizi ya chumvi hiyo
ambayo hutolewa kupitia njia mbalimbali.
Dk. Magige alisema mikakati ya mkoa huo kuwakomboa wakazi wa wilaya ya
Meatu maeneo mengine ya nchi kutoka katika matumizi ya chumvi isiyo na
madini joto ni pamoja na kutoa mafunzo kwa wanahabari waweze kujua ukubwa wa tatizo na kupanga
mikakati ya kuweza kuisaidia jamii.
“Lakini mkakati mwingine ambao tumejiwekea kama mkoa ni kuipeleka hii elimu pia
kwa watu wa afya ngazi ya jamii tunaita ‘community health workers’.
“Hawa pia
wameandaliwa mafunzo yao ambayo ni tofauti kidogo, wao wataenda
kufundishwa ukubwa wa tatizo lakini pia kuwatengenezea mkakati wa namna gani
watashirikiana na jamii kuhakikisha kwamba chumvi inakuwa na madini joto,”
alisema.
Mkuu wa Wilaya ya Meatu, Dk. Joseph
Chilongani alisema wilaya hiyo imechukua hatua ya kutoa elimu kwa
wananchi juu ya matumizi ya chumvi isiyo na madinijoto na wengi wao kwa sasa
hawaitumii chumvi isiyo na madini joto inayopatikana katika kijiji cha
Nyalanja.