Na RAMADHAN HASSAN-DODOMA
CHANZO cha moshi uliotokea juzi usiku ndani ya ukumbi wa Bunge kimetajwa kuwa ni kifaa cha ielektroniki cha kuchajia simu ya mkononi (Power Bank) ambacho kilikuwa kikichaji simu mbili kwa wakati mmoja.
Akitoa taarifa bungeni jana, Naibu Spika wa Bunge, Dk. Tulia Ackson alisema tukio hilo lilitokea juzi saa 1:20 usiku wakati kikao cha Bunge kikiendelea.
Alisema ulitokea mlipuko wa kifaa cha elektroniki cha kuchajia simu ya mkononi uliosababisha harufu kali na kutanda moshi katika ukumbi wa Bunge hasa upande wa kulia wa kiti cha Spika.
“Kwa mujibu wa maelezo ya askari wa Bunge, mlipuko ulitokea kwenye power bank ambayo ilikuwa ikichaji simu mbili kwa wakati mmoja kwenye droo ya meza ya mbunge Richard Mbogo,”alisema.
Alisema kifaa hicho kiliteketea kwa moto na kilianguka chini na kuunguza zulia na pembeni mwa kiti cha mbunge huyo.
“Katika tukio hilo hakukuwa na majeruhi isipokuwa baadhi ya wabunge walipata mshtuko na baadhi yao walikimbia nje ya ukumbi wa Bunge na waliobaki ndani ya ukumbi walipaliwa na moshi na kukohoa,” alisema Dk. Tulia
Naibu Spika alisema kutokana na hali hiyo ilimlazimu Mwenyekiti wa Bunge, Mussa Zungu kuahirisha kikao cha Bunge.
Akiomba mwongozo kwa Spika, Mbunge wa Viti Maalumu, Ruth Mollel (Chadema), alisema haelewi ni kwnini moshi ulitokea ndani na hakuna kifaa cha kiashiria moshi huo.
“Nilitegemea kungekuwa na alarm za kutushtua sisi huku ndani niliona ni jambo very serious lakini sijaona kifaa cha kuashiria na tangu tumekuja humu ndani hatujapewa eneo ambalo tutaweza kukutana kama moto ukitokea na tutokeje,” alisema Mollel.