29.7 C
Dar es Salaam
Friday, October 4, 2024

Contact us: [email protected]

JPM AIPAISHA TANZANITE DUNIANI

Na MASYAGA MATINYI


UJENZI wa ukuta kuzunguka machimbo ya Tanzanite katika eneo la Mirerani, Wilaya ya Simanjiro, Mkoa wa Manyara, umeongeza thamani ya madini hayo kwa asilimia 15 katika soko la dunia.

Mbali ya kuongeza thamani ya madini hayo ya kipekee ya vito, pia imani ya watumiaji imeongezeka wakiamini uwepo wa ukuta utaifanya biashara ya Tanzanite kupitia mkondo sahihi na salama kabla ya kufika sokoni.

Uhalisia huo umewekwa bayana na Mwenyekiti wa Chama cha Wanunuzi na Wauzaji Madini Tanzania (TAMIDA), Sammy Mollel, katika mahojiano yake na MTANZANIA kuhusu umuhimu wa ukuta huo.

“Tunampongeza Rais kwa kuonyesha moyo wa uzalendo na nia ya dhati ya kulinda rasilimali zetu ili ziweze kuwanufaisha Watanzania na nchi kwa ujumla.

“Tarehe 20 Septemba, 2017 alipotangaza na kutoa maagizo ya kujenga ukuta kuzunguka machimbo ya Tanzanite pale Mirerani, thamani ya Tanzanite katika masoko ya Marekani na Ulaya mara moja iliongezeka thamani kwa asilimia 15, alisema Mollel.

Alisema wananchi wengi hawakufahamu jambo hilo isipokuwa wafanyabiashara ambao wana wanunuzi katika masoko ya kimataifa ndiyo waliopata ya kupanda kwa thamani ya madini hayo.

“Unajua suala la kujenga ukuta Mirerani lilianza mwa 2002 baada ya fedha zitokanazo na madini hayo kuhusishwa na ugaidi pamoja na kundi la Al-Qaeda, jambo ambalo liliathiri kwa kiasi kikubwa biashara.

“Hivyo Serikali kwa maana ya Wizara ya Nishati na Madini wakati huo, sisi TAMIDA na wadau wengine tukalazimika kwenda Tucson, kule Arizona Marekani kutetea madini yetu.

“Baada ya majadiliano marefu na mikikimikiki mingi, kikazaliwa kitu kinaitwa “Tucson Tanzanite Protocal”, ambapo kimsingi yalikuwa makubaliano yatakayohakikisha madini ya Tanzanite yanapita katika njia na mikono salama hadi kuwafikia watumiaji au walaji,” alisema.

Mollel alisema makubaliano ya Arizona yalikuwa na kipengele muhimu kilichoitaka Serikali kujenga uzio kuzunguka machimbo ya Tanzanite, lakini kilichojengwa ni uzio wa senyenge kuzunguka eneo la Kitalu C, eneo ambalo lilikuwa chini ya mwekezaji AFGEM (Tanzanite One).

Alisema uamuzi wa Rais kujenga ukuta umekamilisha ndoto iliyosubiriwa kwa takribani miaka 17 na wadau wa Tanzanite ndani na nje ya Tanzania, na usalama wa biashara ya madini hayo hauna shaka tena.

“Utoroshaji wa madini utadhibitiwa, kodi ya Serikali itakusanywa na wahalifu sasa hawataweza kuingia katika eneo la machimbo, hivyo hatutarajii madini yetu kuhusishwa na uhalifu wa kimataifa tena,” alisema Mollel.

 

WACHIMBAJI WASWEKWA MAHABUSU

Katika hatua nyingine, viongozi wa Chama cha Wachimbaji Mkoa wa Manyara (MAREMA), hawakuweza kuhudhuria hafla ya uzinduzi wa ukuta wa Mirerani, baada ya kuwekwa mahabusu katika kituo cha polisi Mirerani.

Waliowekwa mahabusu ni Jafari Matambi (Mwenyekiti), Wariamangi Marko (Makamu Mwenyekiti), Aboubakar Madiwa (Katibu) na Zephania Mungaya (Naibu Katibu wa Mkoa).

Viongozi hao waliwekwa mahabusu baada ya kuitikia wito wa Mkuu wa Kituo cha Polisi, Evaris Makala, aliyewaita kwa ujumbe mfupi wa simu (sms).

Ujumbe wake kupitia namba yake ya simu 07676455… kwenda kwa viongozi hao ulisomeka, “Kaka Madiwa shikamoo! Nakuomba wewe, Wariamangi Sumari@ a.k.a Meze, Jafari Matambi, Zephania na Samwel Rugemarila, mje ofisini kwangu saa kumi jioni leo tarehe 05.04.2018. OCS MIRERANI.”

Mmoja wa viongozi hao alisema walipoitwa walidhani wanaenda kuulizwa kuhusu taarifa kuhusu baadhi ya vijana wasiokuwa wafanyakazi migodini kuandaliwa kuleta vurugu wakati wa ziara ya Rais.

“Lakini tulipofika tukageuziwa kibao na kuwekwa ndani huku baadhi yetu tukiulizwa kwanini tumekuwa kwenye uongozi wa MAREMA kwa muda mrefu, kwa kweli tumesikitishwa sana, ni uonevu usiokuwa na sababu.

“Sisi hatuwezi kuratibu vurugu, turatibu vurugu ili iweje? Hata suala la mishahara kwa vijana tunaoshirikiana kwenye uchimbaji tayari tumelifikisha serikalini na tumeshafanya vikao kadhaa na Katibu Mkuu wa Wazara ya Madini, ila kwa bahati nzuri mchezo wote ulivyofanyika hadi tukawekwa ndani tumeufahamu,” alisema mmoja wa viongozi hao.

Walisema wamesikitishwa na kitendo hicho kwa kuwa kimewanyima fursa ya kushiriki ufunguzi wa ukuta wakati ni wadau muhimu.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Manyara, Augustino Senga alithibitisha kushikiliwa kwa viongozi hao kwa kile alichoeleza kuwa waliitwa polisi kwa mahojiano.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Alexander Mnyeti alisema hana taarifa zozote kuhusu tukio hilo na kusema suala la watu kukamatwa linahusu Jeshi la Polsi.

Viongozi hao waliachiwa Ijumaa saa 1 jioni na kutakiwa kuripoti leo Jumatano.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
590,000SubscribersSubscribe

Latest Articles