27.1 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

CHADEMA YAVUKA KIKWAZO KIMOJA

WananchiNA BENJAMIN MASESE, MWANZA

 MAHAKAMA Kuu, Kanda ya Mwanza, jana ilitupilia mbali pingamizi lililowekwa na Jeshi la Polisi mkoani hapa, lililokuwa likitaka kesi iliyofunguliwa na Charles Lugiko ambaye ni baba mdogo wa aliyekuwa Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Mkoa wa Geita, marehemu Alfonce Mawazo, isisikilizwe kwa kuwa mlalamikaji hana haki kisheria.

Jaji anayesikiliza shauri hilo, Lameck Mlacha, alitupilia mbali maombi hayo ya polisi, baada ya kusikiliza hoja walizowasilisha kwake.

Katika shauri hilo, mvutano uliibuka mwishoni mwa wiki iliyopita baada ya Jeshi la Polisi kuzuia mwili wa marehemu Mawazo usiagwe jijini Mwanza kwa kile walichodai kuna mlipuko wa ugonjwa wa kipindupindu.

Hata hivyo, hoja hizo za Jeshi la Polisi zilipingwa na wanasheria wa Chadema wanaomtetea Lugiko na familia yake.

Jumatatu wiki hii, ndugu wa marehemu Mawazo pamoja na wanasheria wa Chadema, waliamua kufungua kesi namba 10/2015, katika Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Mwanza, iwasaidie kutoa tafsiri ya zuio la jeshi hilo la polisi.

Kutokana na hali hiyo, Jeshi la Polisi jana liliwasilisha rasmi pingamizi lao mahakamani hapo, likimuomba jaji anayesikiliza shauri hilo, kutolisikiliza kwa kile kilichoelezwa kuwa Lugiko si baba mzazi wa marehemu Mawazo.

Katika kesi hiyo, Jeshi la Polisi liliwakilishwa na mawakili wawili wa Serikali ambao ni Seth Mkemwa na Emilly Kilia na upande wa Lugiko uliwakilishwa na mawakili wa Chadema, John Mallya, James Milya na Paul Kipeja.

Katika maelezo yake mahakamani hapo, Wakili Mkemwa, alimuomba Jaji Mlacha kutoisikiliza kesi hiyo kwa kuwa mlalamikaji si baba mzazi wa marehemu Mawazo.

“Mheshimiwa jaji, kesi hii ya dharura ya Lugiko, tunaomba isipewe nafasi ya kusikilizwa kwa kuwa mlalamikaji hana hoja za kimasilahi anazotetea, kwani hajazingatia pia taratibu na sheria katika maombi yake.

“Tunafahamu kwa mujibu wa sheria zetu, mtu yeyote anayeleta ombi la kesi ya namna hii, lazima awe na masilahi ya kutosha. Sisi kama upande wa jamhuri, hatuoni mlalamikaji ana masilahi yoyote kwa marehemu Mawazo, kwa sababu wazazi wa marehemu hatujaambiwa kama wapo au walishafariki.

“Katika shauri hili, mlalamikaji anapaswa kuwasilisha vielelezo mahakamni vya kuonyesha kweli wazazi wake marehemu Mawazo walishafariki au barua ya kumkabidhi kumlea,” alisema Wakili Mkemwa.

Mkemwa alipomaliza kutoa maelezo hayo, Wakili Millya anayemtetea Lugiko, alijibu hoja kwa kuiambia mahakama hiyo, kwamba Lugiko ana masilahi na marehemu kwa kuwa ndiye aliyemlea tangu mwaka 1977 alipokuwa akiishi naye eneo la Butundwe, Wilaya ya Sengerema, mkoani Mwanza.

Katika maelezo yake, Millya aliiambia mahakama, kwamba mawakili wa Serikali wanapaswa kutambua kuwa ombi hilo ni la dharura, na pia  Lugiko ni miongoni mwa wazazi wa marehemu na ana masilahi naye.

Baada ya mvutano wa kisheria kushika kasi, Jaji Mlacha aliomba apewe dakika 45 ili apitie maelezo ya pande zote mbili ili kuona kama kuna kesi ya kusikilizwa.

 

HUKUMU YA AWALI

 

Baada ya dakika 40, Jaji Mlacha alirejea tena mahakamani hapo na kuanza kusoma maelezo ya kila upande, kisha akasema upande wa baba mdogo wa marehemu Mawazo una haki ya ndugu yao kuagwa, na hivyo akasema kuna hoja za msingi za kusikiliza kesi hiyo ingawa polisi walikuwa wanapinga.

“Sheria ziko wazi katika masuala ya misiba, mtu yeyote ndani ya familia anaweza kuwasilisha ombi mahakamani kwa ajili ya taratibu za kifo cha ndugu yao. Katika mila na tamaduni za Kiafrika, baba, mama, baba mdogo na mjomba ni sehemu ya ndugu wa karibu sana.

“Hivyo, Lugiko ambaye ni baba mdogo wa marehemu Mawazo, ana haki ya kuwasilisha ombi mahakamani kama alivyofanya. Kwa maana hiyo, mahakama yangu inatupilia mbali hoja ya Jeshi la Polisi ya kutaka kesi hii isisikilizwe,” alisema Jaji Mlacha.

Pamoja na uamuzi huo wa awali, Jaji Mlacha aliwataka wanasheria wa Chadema waandae na kuwasilisha kwake hati ya kuaga mwili wa marehemu Mawazo ili kuipitia na kuruhusu taratibu nyingine za mazishi.

 

WANANCHI WAZINGIRA MAHAKAMA

 

Kesi hiyo ambayo imeonekana kuvuta hisia za wakazi wa Mwanza, ilisababisha mamia ya wananchi kufurika maeneo yote yanayozunguka viwanja vya Mahakama Kuu, Kanda ya Mwanza iliyopo Barabara ya Posta.

Kwa kuwa watu walikuwa wengi, polisi walilazimika kufanya kazi ya ziada kuwazuia ili wasiingie mahakamani kwa ajili ya kuhofia uvunjifu wa amani.

Pamoja na polisi kuwazuia wananchi hao wasiingie mahakamani hapo, bado wananchi hawakukubali kuondoka kwani waliweka kambi kandokando ya mahakama hadi uamuzi wa awali ulipotolewa.

Baada ya uamuzi huo kutolewa, viongozi wa Chadema, wakiwamo wabunge zaidi ya 20 kutoka majimbo tofauti nchini, walikuwa wakionyesha vidole viwili juu kama ishara ya ushindi.

Ishara hiyo, ilisababisha shangwe na kelele na kuwafanya polisi wawe na kazi ya kuwazuia wananchi wasisogee karibu na mahakama hiyo.

Wakati kelele za shangwe zikiendelea, Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, alilazimika kuzungumza na wananchi hao kwa kutumia kipaza sauti, akiwaeleza kilichotokea mahakamani.

Katika maelezo yake, Mbowe alisema wameshinda hatua ya kwanza, na kwamba walikuwa wakijiandaa kuingia katika hatua ya mwisho ya kuruhusiwa kuaga mwili wa marehemu Mawazo.

“Kwahiyo, nawaomba muondoke katika eneo la mahakama kwa utulivu na mrejee tena baada ya saa mbili kwa kuwa wanasheria wamepewa maelekezo na jaji kuwasilisha hati ya maombi ya kuuaga mwili wa marehemu,” alisema Mbowe.

Kauli hiyo ya Mbowe iliheshimiwa, lakini wananchi waliongozana naye hadi Hoteli ya Gold Crest iliyopo katikati ya Jiji la Mwanza, ambako viongozi wa Chadema na wanasheria wao, wameweka kambi kwa ajili ya kesi hiyo.

 

POLISI WAJAA MWANZA

 

Katika hali isiyokuwa ya kawaida, idadi kubwa ya askari polisi iliongezeka jijini Mwanza huku wengi wao wakiwa ni wageni.

Wakati wa kuimarisha ulinzi, askari hao walijipanga eneo lote linalozunguka Mahakama Kuu na wengine walikuwa kwenye magari kwa ajili ya kuimarisha ulinzi.

Taarifa zilizopatikana mjini hapa, zinasema idadi kubwa ya askari hao waliletwa kutoka katika mikoa ya Shinyanga na Simiyu.

MTANZANIA ilipomuuliza Kamanda wa Polisi, Mkoa wa Mwanza, Charles Mkumbo, juu ya wingi wa askari hao, hakuwa tayari kuzungumzia suala hilo kwa kile alichosema kuwa ni kuingilia uhuru wa mahakama kwa kuwa Jeshi la Polisi ndilo lililoshtakiwa.

Wakati hayo yakiendelea, Wakili Millya aliwaambia waandishi wa habari, kwamba waliwasilisha mahakamani hapo madai matatu ya msingi.

“Dai la kwanza, tumeiomba mahakama itengue zuio la kutouaga mwili wa marehemu Mawazo hapa jijini Mwanza, ambalo lilitolewa na Kamanda Mkumbo, pili tumeiomba mahakama itoe tamko, kwamba zuio la Mkumbo ni batili na mwisho tumeiomba mahakama kumkataza Mkumbo asijihusishe kwa namna yoyote na masuala ya kuuaga mwili au kwenye mazishi ya Mawazo.

“Pamoja na hayo, kesi hii namba 11/2015 itaanza kusikilizwa kesho (leo) saa tatu asubuhi na kutolewa hukumu,” alisema Millya.

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles