22.5 C
Dar es Salaam
Saturday, June 22, 2024

Contact us: [email protected]

Papa Francis kutua Kenya leo

PopeFrancis-8NAIROBI, Kenya

KIONGOZI wa Kanisa Katoliki Duniani, Papa Francis, anatarajiwa kuwasili Kenya leo jioni kwa ziara ya siku tatu.

Wakati huohuo,  Serikali ya Kenya imetangaza kesho kuwa mapumziko maalumu kwa ibada itakayoongozwa na kiongozi huyo.

Papa anatarajiwa kugusa ardhi ya Kenya saa 11 jioni  ndege yake itakapotua kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta, Nairoibi.

Atakuwa Kenya kwa ziara ya siku tatu kabla ya kwenda Uganda keshokutwa  na baadaye  Jamhuri ya Afrika ya Kati (CAR) atakakohitimisha ziara yake   ya siku sita barani Afrika.

Ingawa hiyo ni ziara ya kwanza kwa Papa Francis barani Afrika tangu achaguliwe kuliongoza Kanisa la Katoliki mwaka 2013, ni ziara ya nne kufanywa na kiongozi mkuu wa kanisa hilo nchini Kenya.

Papa Yohane Paulo aliitembelea Kenya mwaka 1980, 1985 na 1995.

Katika ziara yake,  Papa Francis ataongoza ibada kwa Wakenya na kuwa mazungumzo na viongozi  mbalimbali akiwamo Rais Uhuru Kenyatta, viongozi wa dini, vijana na wanadiplomasia na   kukutana na makundi ya watu wasiojiweza na masikini.

Ibada ya kesho itakayoanza saa 4.00 asubuhi inatarajia kuhudhuriwa na watu milioni 1.4 kwenye viwanja vya Chuo Kikuu cha Nairobi.

Wakati msemaji wa Ikulu, Manoah Esipisu akitangaza kesho kuwa mapumziko, Jeshi la Polisi limetangaza kuwa barabara muhimu za Nairobi zitafungwa kuhakikisha usalama wakati wa ziara ya Papa.

Wakati Yohane Paulo alipoitembelea Kenya miaka 35 iliyopita, shauku ya Wakenya wengi ilikuwa aubane utawala wa Rais Daniel arap Moi kutekeleza sera zitakazosaidia wenye mahitaji.

Miongoni mwa  matarajio ya Wakenya kwa sasa ni Papa Francis kutoa changamoto na kuwataka Wakenya kukabiliana na kutatua suala la ukabila linaloitafuna nchi hiyo.

Kilichowafurahisha Wakenya ni kwamba siku mbili kabla, Papa Francis aliwatumia ujumbe kwa njia ya video   akieleza kuwa maridhiano ya taifa ni miongoni mwa masuala atakayoyazungumzia akiwa Kenya.

Kwa mujibu wa kura za maoni zilizochapishwa Jumapili na asasi za Infotrak Research and ConsuKlting, Wakenya wanataka Papa ajadili suala la umuhimu wa kuishi pamoja kwa amani, utawala bora, haki za binadamu na ubaya wa ukabila.

Pia wanamtaka azungumzie suala la ufisadi wakati atakapokutana na viongozi wa  siasa akiwamo Rais Kenyatta.

Pia walisema wakati atakapoonana na viongozi wa dini kesho asubuhi, anapaswa kuzungumzia kuishi pamoja kwa amani, uongozi bora, maadili na haki za  jamii.

Kwa mujibu wa kamati inayosimamia ziara ya Papa, mapadri na viongozi wote wa roho watakaohudhuria ibada ya kesho, wanatakiwa kuvaa mavazi maalumu kwa tukio hilo.

Wananchi  pia wametakiwa   kutunza mazingira, kabla, wakati, na baada ya ibada.

Viongozi wa  roho wametakiwa kuegesha magari yao katika eneo la makaburi ya Consolata na kwenda katika eneo la ibada.

Watu wenye matatizo ya kutembea watachukuliwa hadi eneo la tukio kwa magari maalumu lakini watapaswa kupata vibali vya kuwaruhusu.

Kutokana na idadi kubwa ya watu wanaotarajiwa kuhudhuria ibada hiyo, hakuna magari yatakayoruhusiwa katikati ya mji au popote karibu na eneo la ibada.

Magari yatakayoruhusiwa ni yale maalumu na dharura tu huku watakaoingia katika eneo la ibada watatakiwa kuwa na kadi maalumu na beji kutoka kamati inayohusika.

Kwa mujibu wa ratiba, Papa atafanya ibada ya pili katika Parokia ya Kangemi keshokutwa kabla ya kwenda Uganda.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
588,000SubscribersSubscribe

Latest Articles