21.5 C
Dar es Salaam
Saturday, July 27, 2024

Contact us: [email protected]

Chadema wataka NEC iweke wazi ilikochapisha karatasi za kupigia kura

Na MWANDISHI WETU-DAR ES SALAAM

CHAMA Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimeitaka Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), kuweka wazi mambo matatu.

Mambo hayo  kwanza ilikochapisha karatasi za kupigia kura, pili kutoa daftari ya kudumu la wapiga kura lenye maji na picha na tatu kuwaruhusu kukagua mfumo wa kuhesabu kura.

Hayo yalibainishwa jana na Katibu Mkuu wa chama hicho, John Mnyika katika mkutano wake na Waandishi wa Habari uliofanyika Makao Makuu ya chama hicho, Kinondoni, Dar es Salaam.

 Mnyika alianza kwa kusema; “Kuna jambo ambalo Waandishi na umma wa Watanzania hawalifahamu, tarehe 8  Oktoba NEC iliitisha kikao cha kwanza cha Kamati ya Taifa ya manunuzi na logistics.

“Tafsiri yake toka mchakato uanze NEC imekuwa ikifanya taratibu  za manunuzi bila kuhusisha vyama vya siasa hadi tarehe 8 Oktoba ilipotisha kikao ambacho kimsingi ilikuwa kuvieleza vyama kama tume imefanya manunuzi.

Katika hilo Mnyika alihoji mchakato ambao NEC imeutumia pasipo kuvishirikisha tangu mwanzo vyama vya siasa katika manunuzi ya karatasi za kupigia kura.

“Hili ni jambo nyeti sana kumbuka NEC ilitangaza kwenye vyombo vya habari Machi 9, 2020 zabuni ya kuitisha makampuni ya kuchapisha karatasi cha kupigia kura katika taratibu za kawaida NEC ilipaswa baada ya hapo itoe taarifa kwamba kampuni gani zilishindanishwa na ipi imeshinda.

“Lakini toka hapo tume ilikuwa kimya hadi Juni baadhi ya vyombo vya habari kunusanusa na kuandika kuwa kampuni ya Afrika kusini imeteuliwa kuchapisha karatasi za kupiga kura na Juni 30 Mwenyekiti wa NEC, Jaji Semistocles Kaijagekaijage alipoulizwa na waandishi wa habari hakukanusha badala yake akaviambia vyombo vilivyomuhoji kwamba siku chache wangetoa taarifa kwamba kampuni gani imeshinda, toka hapo zaidi ya mienzi miinne imepita  NEC haikuwahi kutoa taarifa.

Mnyika alisema hata kamati ya zabuni inayohusisha vyama vya siasa katika kikao chake cha tarehe 8 Oktoba haikuelezwa chochote lakini kwa vyanzo vyao wamebaini kampuni moja ya jijini Dar es salaam ambao miongoni mwa wamiliki wake wana uhusiano wa karibu na CCM ndiyo iliyopewa zabuni hiyo.

Katika hilo Mnyika alisema wana wasiwasi na usalama wa kura zitakazopigwa Oktoba 28 na hivyo wao wanaitaka NEC ijieleze ni kampuni gani iliyopewa zabuni  ya kuchapisha karatasi hizo ili kuondoa ukakasi uliopo.

“Tume ieleze ni mchakato gani ilitumia kupitisha mchakato wa kuteua kampuni iwaeleze Watanzania… kwa sababu kama hakuna usalama katika kuchapisha karatasi za kura upo uwezekano wa kuchapisha karatasi za ziada,” alisema Myika 

Alitaka jambo hilo lisichukuliwe kwa wepesi kwa sababu lilileta mgogoro mkubwa Kenya hadi kufikia kupelekwa Mahakamani na kubatilisha uchaguzi wa mwaka 2017.

Aidha Mnyika aliitaka NEC kutoa nakala ya daftari la kudumu la wapiga kura la mwisho kwa vyama vya siasa.

“Kupitia kwa Kamshna wake mmoja walisema imetoa orodha lakini orodha sio daftari la kudumu la wapiga kura.

“ Daftari linakuwa na si tu orodha bali na picha hili daftari ndilo ambalo tutalitazama kama halina wapiga kura hewa na hili ndilo mawakala watalitumia kuhakikisha mpiga kura anayekuja kupiga kura namba yake na picha yake inalingana,”. 

“Daftari hili halijatolewa, tunalitaka tume itoe daftari hilo. wametoa orodha hiyo kwenye flash, kama hawatatuletea daftari printed ambalo litasambazwa nchi nzima tunaitaka NEC iharakishe litupatie daftari.

Kuhusu mfumo wa kumjulisha matokeo Mnyika alisema katika kikao cha manunuzi na logistic cha Oktoba 8 NEC haikuweka wazi masuala ya mfumo wa ujumlishaji wa matokeo.

“Kwa ratiba waliyoitangaza NEC inatarajia kuanza mafunzo kwenye huo mfumo tunataka kabla haujaanza kutolewa mafunzo kwa wasimamizi vyama vya siasa tupewe fursa ya kuona mfumo na kuhakiki”.

Mnyika alikumbusha jinsi alivyoonya kuhusu jambo hilo katika Uchaguzi wa mwaka mwaka 2015 akisisitiza kuwa;

“Safari hiii nimeamua kulisema mapema ili kuukagua mfumo kuufanyia ‘system audit’  kabla haujaanza kutumika”.

Gazeti hili lilimtafuta Mkurugenzi wa NEC, Dk. Wilson Mahera ambapo baada ya kusikiliza maswali ya mwandishi kuhusu hoja za Mnyika aliahidi kupiga simu akimaliza jambo analolifanya.

Lakini hadi tunakwenda mitamboni hakufanya hivyo.

KUHUSU POLISI

Wakati huo huo Chadema wamelitaka Jeshi la Polisi kutenda haki na kuwachukulia hatua maofisa wao wanaoingilia siasa na kwenda kinyume na maadili ya jeshi hilo.

“Tumeshangazwa na kauli ya IGP kuhusu tukio la wazi la OCD wa Hai kufanya tukio la wazi kufanya siasa na kukiuka kanuni za jeshi la polisi kumtamkia Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe kwamba wewe hutashinda na IGP kusema eti wameunda kamati ya uchunguzi katika tukio la wazi kama hilo”.

Katika hilo Mnyika alimtaka IGP kumwondoa ofisa huyo kwa sababu ameonyesha wazi kukiuka maadili yake ya kazi. 

Alisema matukio ya Hai yamekuwa mengi mengi ikiwamo watu wenye silaha kuwateka kwa Evarist Espareti na Malya wa kata ya Nalumu na kisha kuwatesa na kuwatupa.

“Baadhi ya watu wakafahamika badala ya polisi kuwachukulia hatua waliohusika polisi wanasema hakuna tukio hilo”. 

Kuhusu tukio la Tarime, Mnyika alisema kuna upotoshwaji huku akiwalaumu polisi kuvamia mkutano wa mbunge wao na kuwakamata baadhi ya wafuasi wao ambao wako kwenye timu ya kampeni.

“IGP amezungumzia vilevile kuhusu Tarime akazungumzia akisema kuna kijana amekamatwa ametoka Zanzibar, IGP aeleze kwanini tangu Oktoba 5 baada ya  polisi kuvamia  ngome ya mgombea wetu sio tu wakakamata watu bali kuvunjavunja spika na kufanya uharibifu wa mali hivi zile spika zilifanya kosa gani kama sio uharibifu wa mali na kukamata timu rasmi ya kampeni 10 na mwananchi  mmoja mgonjwa aliyefika kumwombe mbunge amsaidie pesa ya matibabu”.

“Tangu tarehe 5 hakuna aliyepelekwa mahakamani, ndugu zao wanakataliwa kuwaona, wala kupelekewa chakula, kama wangekuwa wakosaji polisi wangejitokeza kusema wamefanya kosa gani”.

Mnyika alizungumzia vilevile tukio la Shiyanga  Mjini akisema;

“Bahati nzuri  hili nalo limerekodiwa OCD amevamia ngome ya kampeni anakwenda na bango la Magufuli lililochanwa ili awasingizie wafuasi wetu lakini bahati nzuri tukio limerekodiwa”.

Katika hayo yote Mnyika alimtaka IGP kuwachukulia hatua wale wote wanaokwenda kinyume ili kurudisha imani kwa jeshi la polisi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles