23.6 C
Dar es Salaam
Saturday, May 18, 2024

Contact us: [email protected]

Chadema: Tumechoka

mbowe*Wajipanga kutoa tamko zito kwa wanachama

Na Waandishi Wetu, Dar/Kilombero

KAMATI Kuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), imerusha kombora kwa Rais Dk. John Magufuli na kusema kuwa sasa wamechoka na uonevu.

Chama hicho kimesema kuwa wanashangazwa na hatua ya kukamatwa kwa wabunge wao huku viongozi wa juu wa Serikali wakibaki kimya, hasa Rais Magufuli, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa na Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue.

Kimesema tangu ulipovurugika Uchaguzi wa Meya wa Jiji la Dar es Salaam, wabunge na madiwani wao wamekuwa wakikamatwa na kudhalilishwa kwa madai ya kufanya fujo jambo ambalo si sahihi.

Akitoa tamko la Kamati Kuu kwa waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, alisema katika kipindi cha siku mbili watatoa tamko kwa wanachama wao ikiwamo kuchukua uamuzi mzito kutokana na vitendo hivyo vya udhalilishaji.

Alisema kuwa vitendo hivyo vya uonevu ambavyo vinafanywa na Jeshi la Polisi, vinatokana na shinikizo la viongozi hao wa Ikulu na Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Mbowe alisema wakati vitendo hivyo vinaendelea, Rais Magufuli, Waziri Mkuu Majaliwa pamoja na Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Sefue wamekaa kimya, jambo ambalo linaonyesha wazi kuwa wanahusika kutoa amri ya kufanyika kwa vitendo hivyo.

Alisema hadi sasa Mbunge wa Ukonga, Mwita Waitara na Mbunge wa Kawe, Halima Mdee wamezuiliwa na polisi kwa ajili ya kuhojiwa huku baadhi ya askari wakienda nyumbani kwao kwa ajili ya upekuzi.

Mbowe alisema wakati hali hiyo ikiendelea, hivi sasa Mbunge wa Ubungo, Saed Kubenea amekuwa akitafutwa na polisi kwa madai kama ya wenzake ya kuvuruga uchaguzi.

Alisema chama hicho hakitavumilia kuona vitendo vya wazi vya kuua demokrasia nchini vinafanyika, na kwamba kikao hicho kitakuja na uamuzi mzito wa kitaifa ambao utawasilishwa kwa wanachama ili kuchukua uamuzi.

Mbowe alisema hawawezi kuvumilia vitendo vya unyanyasaji, uonevu na dhuluma inayofanywa na Serikali ya CCM, hivyo basi watatangaza uamuzi mzito ambao utafanywa na wanachama wao nchi nzima.

“Tumechoka kunyanyasika, tutatoa tamko kali la kitaifa ambalo litawasha moto kwa wanachama wetu, kwa sababu wao wameandaa mkakati wa kuua demokrasia nchini, hatutakubali.

“Kama polisi wamepanga kuwabambikia kesi ya dawa za kulevya ili waweze kuwatia hatiani, mpango huo umefeli, tutapambana mwanzo mwisho,” alisema Mbowe.

Alisema hawatavumilia kuona Serikali ya awamu ya tano ikiwakandamiza viongozi wao na kwamba wapo tayari kupambana ili kuhakikisha demokrasia inalindwa.

“Kazi ya upinzani si kuisifia Serikali, bali ni kutetea demokrasia pamoja na kuikosoa Serikali, kazi ya kuisifia Serikali inapaswa kufanywa na CCM na Katibu Mwenezi wake Nape,” alisema Mbowe.

Akizungumzia kuhusu Uchaguzi wa Umeya wa Jiji la Dar es Salaam, Mbowe alisema kuwa umevurugwa na CCM kwa sababu wanaamini hawawezi kushinda.

Alisema vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), vina idadi kubwa ya madiwani katika Halmashauri ya Ilala na Kinondoni, kuliko Temeke, lakini CCM inafanya hujuma ili wasiweze kupata meya, hali iliyochangia Uchaguzi wa Meya wa Jiji kuvurugika.

“Mbona Uchaguzi wa Meya wa Temeke haujavurugika? Kwa sababu tunajua CCM ina madiwani wengi, lakini Ilala na Kinondoni idadi kubwa ya madiwani wanatoka Ukawa ndiyo maana wanatafuta kila sababu ya kuvuruga uchaguzi ili waweze kushinda,” alisema.

Aliongeza kuwa kitendo cha kumtuma Katibu Tawala (RAS) kutangaza zuio la kughushi ambalo halijatolewa na mahakama yoyote, ni sawa na kuvitaka vyama vya upinzani kushindwa kufanya uchaguzi hivyo hawatakubali.

Alisema kuwa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam ina kashfa nyingi, ikiwamo ya Shirika la Usafiri Dar es Salaam (UDA), nyumba za jiji, viwanja vya wazi, wizi kwenye miradi mbalimbali ikiwamo ya maji, barabara na mengineyo, ambapo Serikali ya CCM inataka kuficha uozo huo, jambo ambalo limewafanya kupanga kila aina ya mikakati ili kuvuruga uchaguzi.

Mbowe alisema hadi sasa vurugu nyingine zimetokea Halmashauri ya Wilaya ya Kilombero, Morogoro na Kyerwa mkoani Kagera.

Alisema kwa upande wa Kilombero, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), George Simbachawene, aliwaambia polisi wamwondoe Mbunge wa jimbo hilo, Peter Jualikali kwa madai si mpigakura halali.

Mbowe alisema kwa upande wa Kyerwa, madiwani wa halmashauri hiyo wamefikishwa mahakamani ili wasiweze kushiriki kwenye Uchaguzi wa Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo.

KATIBU WA BUNGE

Hata hivyo, Mbowe alisema Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema, Pauline Gekuru na Esther Bulaya wameandikiwa barua ya wito na Katibu wa Bunge ya kuwataka Machi 9, mwaka huu kwenda kuhojiwa na kuapa kwenye Kamati ya Bunge ya Kinga, Madaraka na Haki za Bunge kutokana na kushindwa kutii amri ya Mwenyekiti wa Bunge, Andrew Chenge.

Alisema wabunge hao waliambiwa kukaa chini na wao kugoma wakati wa kujadili suala la kurushwa kwa matangazo ya moja kwa moja na Shirika la Utangazaji la Taifa (TBC).

UPEKUZI KWA MDEE

Mbunge wa Kawe, Halima Mdee aliondoka polisi jana akiwa chini ya ulinzi wa polisi na kwenda nyumbani kwake Makongo Juu kwa ajili ya ukaguzi.

Hatua hiyo inatokana na uwepo wa taarifa za ndani kueleza kuwa Msimamizi wa Uchaguzi wa Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Theresia Mmbando, alinyang’anywa nyaraka za uchaguzi na mbunge huyo wa Kawe.

Kutokana na hali hiyo, tangu juzi Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam limekuwa likiendesha msako na hata kuwatia mbaroni makada na viongozi wa Chadema.

Ilipotimu saa 9 alasiri askari polisi wakiwa wameambana na Mdee, walifika nyumbani kwake maeneo ya Makongo Juu na kufanya upekuzi kwa muda wa saa moja.

Askari hao pamoja na Mdee walikuwa katika gari namba T 322 FN aina ya Noah.

Hata hivyo, askari hao walijikuta wakikwama kwa muda baada ya mwanasheria wa Mdee, John Malya, kuwataka waonyeshe vielelezo vinavyowataka kufanya ukaguzi ambapo walionyesha na kutaka aitwe Ofisa Mtendaji wa Mtaa.

Baada ya dakika chache alikuja mtendaji huyo ambaye jina lake halikufahamika mara moja na kuingia na askari hao ndani.

Baada ya kumaliza kazi hiyo, walieleka katika ofisi binafsi za mbunge huyo zilizopo Kinondoni ambako pia walifanya upekuzi.

Lakini askari hao walishindwa kupata nyaraka zozote hadi tunakwenda mitamboni.

Wakati hayo yakiendelea, jana saa 7 mchana Mbunge wa Ukonga, Mwita Waitara (Chadema), alijisalimisha polisi ambako alihojiwa na askari kwa muda wa zaidi ya saa sita.

Ilipofika saa 12:30 jioni, Jeshi la Polisi liligoma kutoa dhamana kwa mbunge huyo ambaye naye alilala rumande.

KAULI YA KIBATALA

Akizungumzia matukio hayo, Mwanasheria wa Chadema, Peter Kibatala, alisema kwamba wanasubiri maagizo ya polisi ili kuweza kujua kama wangemwachia kwa dhamana Mdee au watampeleka mahakamani leo.

UKAWA WAMSUSA RC

Katika hatua nyingine, wabunge na mameya wa vyama vinavyounda Ukawa, wamesusia mkutano wa ukaguzi wa miradi ya barabara zilizoko chini ya Wakala wa Barabara (Tanroads).

Pia wamesema hawatashiriki kikao cha Kamati ya Ushauri ya Mkoa (RCC) kinachotarajiwa kufanyika leo kwenye Ukumbi wa Karimjee, Dar es Salaam.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Meya wa Manispaa ya Kinondoni, Boniface Jacob, alisema uamuzi wao wa kujitoa kushiriki ziara za kukagua miradi na mkutano wa RCC, unalenga kushinikiza viongozi wa Serikali kulizuia Jeshi la Polisi kuwakamata viongozi wao.

“Leo (jana) tumewasilisha ujumbe wetu kwa mkuu wa mkoa  kumweleza uamuzi wetu wa kutoshiriki shughuli za maendeleo za mkoa hadi pale atakapowazuia polisi kuendelea kuwakamata viongozi wetu, ambao wengi wao wanashiriki kikao ca RCC kama wajumbe,” alisema Jacob.

Aliwataja viongozi wengine waliokamatwa juzi na kutupwa rumande, ni pamoja na Diwani wa Saranga, Ephraim Kinyafu (Chadema) na kada wa chama hicho, Rafii Juma.

“Baadhi ya wabunge na madiwani wanashikiliwa na polisi, huku wengine kama vile Mbunge wa Ukonga, Mwita Waitara (Chadema), Mbunge wa Ubungo, Saed Kubenea (Chadema) nao wanameitwa polisi,” alisema.

Naye Mbunge wa Temeke, Abdallah Mtolea (CUF), alisema CCM na Jeshi la Polisi kwa pamoja hawana nia njema kwa sababu mtu waliyedai kuwa amejeruhiwa wamemuona ofisini akiwa na afya njema.

KAULI YA RC

Akijibu hoja za wabunge na mameya hao wa Ukawa, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Meck Sadiki, alikiri kufuatwa na wabunge hao ofisini kwake na kuwasihi wahudhurie kikao hicho.

“Niliwaambia nitafurahi kama watahudhuria kikao chetu, michango yao inatakiwa kwa sababu inasaidia wananchi. Nawaomba suala hili wasilichanganye na maendeleo ya wananchi, waje tu,” alisema Sadiki.

MBUNGE MWINGINE AKAMATWA

Wakati huohuo, Jeshi la Polisi Wilaya ya Kilombero, Mkoa wa Morogoro, linamshikilia Mbunge wa Kilombero, Peter Lijualikali (Chadema) kwa tuhuma za kukaidi agizo lao.

Mbunge huyo alizuiwa kuingia katika mkutano wa Uchaguzi wa Mwenyekiti wa Halmshauri ya Kilombero ambao unajumuisha Jimbo la Kilombero na Mlimba.

Kabla ya kuzuiwa na kukamatwa kwa mbunge huyo, waandishi wa habari na viongozi wa wilaya wa Chadema  walizuiwa kuingia katika mkutano huo wa uchaguzi, huku Jeshi la Polisi likidai kuwa wamepewa agizo na Msimamizi wa Uchaguzi, Azimina Mbilinyi kutowaruhusu.

Mbunge Lijualikali alifika eneo la tukio saa 3:30 asubuhi na kuzuiwa na askari waliokuwa wakilinda na kumsihi kwamba haruhusiwi kuingia ukumbini kwa sababu hawana taarifa zake, huku mbunge huyo akidai yeye ni mbunge na ana kibali cha kuhudhuria mkutano huo kwa mujibu wa sheria.

UCHAGUZI WAFANYIKA

Katika uchaguzi huo, Mwenyekiti wa muda Yahya Naniya alimtangaza David Ligazo ambaye ni Diwani wa Kata ya Sanje kupitia CCM kuwa mshindi kwa kupata kura 19 dhidi ya Diwani wa Kata ya Namwawala, Goferd Lwena kupitia Ukawa aliyepata kura 18.

Nafasi ya makamu mwenyekiti imekwenda kwa Diwani wa Kata ya Mwaya kupitia CUF, Adamu Sungura aliyepata kura 19 dhidi ya 18 za mgombea wa CCM ambaye ni Diwani wa Kata ya Uchindile, Emael Ndagalasi.

Habari hii imeandaliwa na Patricia Kimelemeta, Asifiwe Goerge, Silvan Kiwale, Martha Lukumay, Shaban Matutu (Dar es Salaam) na Ramadhan Libenanga (Kilombero)

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
587,000SubscribersSubscribe

Latest Articles