Na Mwandishi Wetu
MWENYEKITI wa Chama Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe, leo anatarajiwa kutoa maazimio mazito ya Kamati Kuu ya chama hicho iliyokutana kwa siku mbili, Dar es Salaam.
Taarifa iliyotolewa Dar es Salaam jana na Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano na Mambo ya Nje, John Mrema, ilisema pamoja na mambo mengine, kamati hiyo ilijadili kwa kina hoja tatu za msingi.
Alitaja hoja hizo kuwa ni hali ya mwenendo wa siasa na ukandamizaji wa demokrasia, kuporomoka kwa uchumi na hali ngumu ya maisha inayowakabili Watanzania.
Alisema hoja ya tatu ni kamatakamata inayoendelea kufanywa na vyombo vya dola dhidi ya viongozi, wanachama na wafuasi wa chama hicho katika maeneo mbalimbali.
“Pamoja na mambo niliyotaja hapo juu, tunategemea mwenyekiti wetu atatoa maelezo mengi kesho (leo), atakapokutana na waandishi wa habari makao makuu.
“Tuna mambo mengi mno, kumekuwapo na tatizo la viongozi wetu wengi kukamatwa kila kukicha maeneo mbalimbali, sisi kama chama cha upinzani hatuwezi kunyamazia jambo hili,” alisema Mrema.
Moja ya matukio ambayo yalitikisha nchi hivi karibuni ni kukamatwa kwa Mwanasheria Mkuu wa chama hicho, Tundu Lissu, kwa tuhuma za kutoa maneno ya uchochezi kuwa “Serikali ya awamu ya tano chini ya Rais Dk. John Magufuli ni ya ubaguzi wa ufamilia,ukabila, ukanda na udini.”
Kutokana na tuhuma hizo, alifikishwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu na kusomewa mashtaka ya uchochezi.
Baada ya kupewa dhamana Lissu alisema hakuna gereza likalowanyamazishwa mahabusu na kwamba wataendelea kuzungumza siku hadi siku hadi kifo kitakapowachukua.