30.2 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

Wanajeshi SADC wapiga kambi mapango ya Amboni

Na AMINA OMARI-TANGA

VIKOSI maalumu vya majeshi ya nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) vimepiga kambi kwenye eneo la mapango ya Amboni, Tanga.

Katika mapango hayo, mwaka jana yalitokea mauaji yaliyofanywa na watu wasiojulikana na kuzua hofu kwa wakazi wa eneo hilo ambao mwishowe walihamishwa na Serikali.

Akizungumza na waandishi wa habari   jana, Mkuu wa mpango huo, Meja Jenerali Harrison Msebo, alisema vikosi hivyo vitakuwa vikifanya mazoezi katika eneo hilo kama sehemu ya kupambana na ugaidi na uharamia baharini.

Kwa mujibu wa Meja Jenerali Msebo, mazoezi hayo yajulikanayo kwa jina la EX Matumbawe, yanatarajia kuanza Agosti 2 hadi Septemba mosi mwaka huu.

“Mazoezi hayo yanafanyika kwa mara ya kwanza  Tanzania baada ya vikosi vya majeshi ya nchi washirika kuanza kufanya mazoezi

ya pamoja kwa ajili ya kujihami dhidi ya matukio mbalimbali ya uhalifu tangu mwaka 2015.

“Pamoja na mambo mengine, lengo letu ni kuhakikisha vikosi vya majeshi katika nchi

washirika vinajengewa uwezo wa kupanga na kutekeleza operesheni za vikosi maalumu  na kujifunza mbinu na weledi katika kupambana na matukio ya uvamizi yanayoweza kufanywa na maharamia na magaidi.

“Mazoezi hayo yanatokana na mbinu za kupigana vita pamoja na matishio ya ugaidi kubadilika mara kwa mara.

“Hivyo kupitia mazoezi hayo, tutaweza kuvitayarisha vikosi vyetu dhidi ya mapambano ya aina yoyote yanayoweza kutokea,” alisema Meja Jenerali Msebo.

Alizitaja nchi zenye majeshi yatakayoshiriki mazoezi hayo  kuwa ni Afrika Kusini, Botswana, Lesotho, Malawi, Zambia, Zimbabwe   na wenyeji Tanzania.

Naye  Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Martine Shigela, alisema mazoezi hayo yataimarisha uhusiano wa kijeshi baina ya nchi wanachama wa SADC na yatawasaidia wanajeshi hao kubadilishana uzoefu katika utendaji kazi wao.

“Kwa hiyo napenda kuwaomba wananchi, kwamba watoe ushirikiano wakati wote wa mazoezi hayo ingawa pia nawaomba wananchi wasipende kuokota vitu ambavyo wana hofu navyo.

“Kama wananchi wakiona kitu wasichokielewa, basi watoe taarifa wahusika waje

kuvitambua badala ya kuviokota kwa ajili ya matumizi yao,” alisema Shigela.

Wakati mazoezi hayo yakitarajia kuanza mwaka jana hali ilikuwa tete na ilizua taharuki jijini Tanga baada ya watu wasiojulikana, kuua idadi kadhaa ya watu katika eneo la mapango hayo.

Serikali ililazimika kupeleka vikosi vya Jeshi la Polisi na askari wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) kwa ajili ya kukabiliana na wahalifu hao.

Wakati vikosi hivyo vya ulinzi na usalama vikifanya kazi, vilikuwa vikiendesha operesheni maalumu ya upekuzi ndani ya mapango hayo kwa lengo la kukabiliana na wahalifu hao.

Kutokana na hali ya usalama kuwa tete katika eneo hilo, baadhi ya watu walilazimika kuhama makazi yao kuokoa maisha yao.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles