NA WINFRIDA MTOI, Mtanzania Digital
Mashindano ya wazi ya gofu,CDF Trophy yameanza rasmi leo Septemba 17,2021 kwenye viwanja vya Klabu ya Lugalo jijini Dar es Salaam, huku mchezaji Frank Mwinuka wa Lugalo akiongoza siku ya kwanza kwa mikwaju 67.
Michuano hiyo ambayo imeanza na wachezaji wa kulipwa, (proffesionals), Mwinuka ameshika namba moja akifuatiwa na Hassan Kadio wa Dar es Salaam Gymkhana aliyefungana na Abdallah Yusuph kwa mikwaju 73 huku wa tatu akiwa ni Rajabu Pembe aliyechapa mikwaju 75.
Akizungumzia mashindano hayo, Mwinuka amesema anafurahi kuongoza kwa siku ya leo na wanatarajia kuendelea Jumapili katika hatua ya fainali.
Naye Kadio amesema kuwa: “Mchezo sio mbaya nimecheza kiasi fulani vizuri inangawa tumefungana wawili na Abdallah Yusufu wa Lugalo na yupo anayeongoza wa hapa hapa Lugalo amecheza vizuri,”
Kwa upande wake Abdallah Yusuf ambaye pia ni mwalimu wa mchezo huo, amesema hawezi kuahidi ushindi bali anasubiri siku ya mwisho ya kufunga mashindano.
Mashindano hayo ambayo yanashirikisha wachezaji wa ridhaa zaidi ya 100 wanaotarajia kucheza kesho, yatafikia tamati Jumapili Septemba 19 mwaka huu.