27.2 C
Dar es Salaam
Friday, November 29, 2024

Contact us: [email protected]

CCM yaonya wasaka ubunge, udiwani

Andrew Msechu – Dar es Salaam

WAKATI baadhi ya viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM)  katika wilaya na mikoa mbalimbali, wakipita kuwahamasisha wanachama wenye nafasi za uongozi ndani ya chama kuwania nafasi za ubunge na udiwani hatimaye uongozi wa juu wa chama hicho umetoa tamkoa na kuzuia mpango huo.

Hilo limekuja wakati huku baadhi ya viongozi wa wilaya wakihamasisha wanachama kujitokeza kuwania nafasi za uongozi ikiwamo ubunge na udiwani hasa kwa wenyeviti wa wilaya na kata pamoja na jumuiya zake na pindi wataposhinda wataachia nafasi walizonazo ndani ya chama.

Kutokana na hali hiyo CCM kimeonya wanachama wake wenye nia ya kuwania ubunge na udiwani kwa kuwataka kufuata utaratibu uliowekwa na chama hicho.

Akizungumza jana MTANZANIA, Katibu wa Itikadi an Uenezi wa CCM, Humphrey Polepole, alisema kwa wale viongozi wenye nafasi ndani ya chama ambao wanajipeleka ka wananchi kuwa wanataka kuwania nafasi za ubunge na udiwani kwenye Uchanguzi Mkuu wa mwaka huu, waache mara moja na kwamba agizo la kofia moja bado liko pale pale.

Alisema japo kuwa kila mwanachama ana haki ya kuchagua na kuchaguliwa lakini bado CCM haijaondoa suala la kofia moja mtu mmoja.

“Suala la agizo la kofia moja liko palepale wala halijawahi kuondoka, haijapadilishwa popote na hiyo ndiyo kauli ya chama. Mtu kutaka kugombea ni haki ya kila mwanachama kutaka kugombea tunachosema watu wasubiri muda ukifika.

“Kugombea ni haki ya kila mwanachama, lakini katika mazingira yoyote yale hakuna mwana CCM kiongozi atakuwa na nafasi mbili sipokuwa kama ilivyoelekezwa kwenye Katiba.

“Hadi sasa kama kuna watu wanajipanga, kujipanga na kufanya kampeni kabla ya muda ni makosa na kwamba hatujazuia haki ya watu kugombea lakini tusubiri muda,” alisema.

Alisema kwamba kofia moja iko pale pale, hajazuiliwa kiongozi yeyote kugombea lakini wanachosisitiza ni kwamba kabla ya wakati hatujatangazwa ni marufuku kufanya vitendo vyovyote vinavyoashiria kwamba mtu anataka kugombea.

Alisema muda ukifika ni vyema watu wafuate utaratibu wa kugombea lakini katika mazingira yoyote yale hakuna mtu atakayekuwa na kofia mbili kinyume na maelekezo ya Katiba na Kanuni.

Alisema wapo watu kwenye Katiba ya CCM wanaruhusiwa kuwa na kofia mbili lakini wengine wote ni mtu mmoja kofia moja.

MAANDALIZI YA ILANI

Akzungumzia suala la maandalizi ya ilani ya chama hicho tawala kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu wa 2020, alisema yanakwenda vizuri baada ambapo Januari 25, mwaka huu walipokea maoni mengi kutoka kwa wananchi na wanachama kwa maelfu ambao wametoa michango mahususi.

Alisema kwa sasa kamati ya kuandika ilani inaendelea pamoja na timu ya wataalamu wa kuandika ilani wanaendelea na wako ndani ya ratiba.

“Mungu akipenda ifikapo Machi tutakuwa tayari na rasimu ya ilani ambayo itapitishwa kwenye vikao vya chama na hiyo itakwenda sambamba na mwelekeo wa sera za CCM kwa mwaka 2020 hadi 2030,” alisema Polepole.

MSIMAMO WA CHAMA

Msimamo huo wa CCM unaosisitiza kwamba viongozi wa umma wabaki na kofia moja ya uongozi, huenda ukawaweka kwenye wakati mgumu baadhi ya vigogo wa Serikali, ambao wamejitokeza kuwania nafasi za uongozi ndani ya chama.

Vigogo ambao wanabanwa na msimmao huo unaotokana na mabadiliko ya Katiba ya CCM mwaka 2017 unawabana wakuu wa wilaya, mikoa, wakurugenzi, wenyeviti wa CCM mikoa na wilaya, pamoja na viongozi katika ngazi ya kata, ambapo chama kinawataka kutumia hekima na busara kujitathmini kama bado wanaweza kutumikia nafasi zao ndani ya utumishi wa umma, ilhali wana nafasi nyingine za uongozi ndani ya CCM.

Msimamo huo wa CCM ni sehemu ya mabadiliko ya kimuundo na uongozi, unaolenga kuwafanya watumishi wa umma kuwa karibu zaidi ya wananchi ili waweze kutekeleza majukumu yao ya kiutendaji kama ilivyoainishwa kwa mujibu wa sheria ya utumishi wa umma.

Akizungumza Oktoba 21, 2017 wakati akizungumza na Shirika la Utangazaji la Taifa (TBC), Polepole alisema Katiba ya nchi na ile ya CCM, zimejieleza vizuri kuhusu jambo hilo.

“Katiba na Kanuni za chama zimejifafanua vizuri, lakini tunaongozwa na hekima kwa sababu hakuna kanuni zilizotungwa zikaweza kutuongoza moja kwa moja.

“Msingi ulikuwa CCM ni chama kinachoongoza nchi. Kama sisi ndio serikali na serikali inasema utii wa sheria bila shuruti, CCM tunapaswa kuwa mstari wa mbele kuishi maisha yanayoakisi usemi huo,” alisema Polepole.

Alisema waraka namba moja kwa watumishi wa umma, uliotolewa mwaka 2015, unaelezea kuhusu utaratibu wa watumishi wa umma wanaogombea nyadhifa za kisiasa nchini.

Polepole alibainisha kuwa, waraka huo umeeleza bayana kwenye kifungu cha 3.1.6, kinachoeleza kuwa, endapo mtumishi wa umma kama akiamua kugombea nafasi yeyote ndani ya chama cha siasa, analazimika kuacha kazi au kuomba likizo isiyokuwa na malipo.

Alisema likizo hiyo itaanza siku ya kupokea majina ya wagombea nafasi za uongozi kwa mujibu wa taratibu za chama husika.

“Kifungu kinaendelea kusema, endapo mtumishi atashindwa kwenye uchaguzi na akataka kurejea kwenye utumishi wa umma, hana budi kuomba ajira upya kwa mamlaka husika. Na atakayekwenda kinyume na waraka huu, atachukuliwa hatua kali za kisheria.

“CCM tunawapenda wanachama wetu, ambao wana dhamana mbalimbali kwa mujibu wa sheria ndani ya serikali. Wana-CCM ambao ni watumishi wa umma, milango iko wazi kuendelea kukiunga mkono chama. Wasije wakaingia kwenye uongozi wakapata matatizo ya ajira zao,” alisema.

Kwa upande wa maofisa wa umma, ambao ni wakuu wa mikoa na wilaya, Polepole alisema suala lao linapaswa kuongozwa na hekima.

Alifafanua kuwa, wengi wao waligombea nafasi za Ujumbe wa Mkutano Mkuu Taifa, ambapo kanuni ya uchaguzi ndani ya CCM, imeweka katazo kwa baadhi ya watu wenye nafasi moja kushiriki kugombea nafasi nyingine.

“Kwenye kanuni ya uchaguzi ya CCM, toleo la mwaka huu, inasema nafasi ya uongozi yenye kazi za muda wote, mkutano mkuu wa taifa haujatajwa.

“Lakini mkuu wa wilaya ni kiongozi wa serikali na kiongozi wa Chama na kamisaa wa chama kwenye serikali, ambaye pia ni ofisa wa umma anayefanyakazi zote ndani ya CCM. Hekima ituongoze kama mtu una dhamana zote hizo, kwanini mkutano mkuu usimwachie mwanachama mwingine?” Alihoji.

Katibu huyo wa NEC, alieleza kuwa endapo wakuu wa wilaya wote 166 wakiomba nafasi hizo, wajumbe 1,700 wa mkutano mkuu wa taifa, 166 watakuwa wakuu wa wilaya.

Alibainisha kuwa, kwa upande wa wakurugenzi walioomba nafasi hizo, wao ni watumishi wa umma, hivyo wanabanwa na waraka namba moja wa watumishi wa umma wa mwaka 2015.

Alisema wakurugenzi ni watumishi wa umma na viongozi, hivyo kama wameomba nafasi hizo, itakuwa mtihani.

“Upande mmoja ni katiba, kanuni na maelekezo ya serikali, ambayo CCM inapaswa kuyaheshimu. Upande wa pili ni hekima ya kuwa na kiasi, kwamba kwa nafasi nyingine, tumwachie mwingine asiyekuwa na nafasi.

“Lingine linakwenda na maelekezo ya CCM, yanayosema mtu mmoja, kofia moja. Ukiwa kiongozi, una dhamana, nafasi nyingine waachie wengine nao waweke mawazo yao,”alisisitiza.

Mbali na hayo, alisema mabadiliko ya CCM kwenye awamu ya tano ya serikali yanayohusu mifumo ya uongozi, muundo na utendaji, yataleta ufanisi mkubwa kwa lengo la kurudi kwenye asili ya CCM, ambayo pamoja na mingine ni haki, watu na uongozi wa kiutumishi.

Alisema kila ambalo serikali inalifanya kwa sasa, limetokana na vikao halali vya Chama, vinavyoushauri serikali inayoongozwa na mwenyekiti wake, akisaidiana na wasaidizi wengine.

Polepole alisema kwenye CCM, kuna wakuu wa chama, ambao ni Mwenyekiti, Makamu Wenyeviti Bara na Zanzibar na Katibu Mkuu ambao wanaiongoza CCM.

DK. BASHIRU NA SOKO LA KURA

Septemba 2, mwaka jana Katibu Mkuu wa CCM, Dk. Bashiru Ally, aliwaonya wanachama wa chama hicho waliogeuza uchaguzi ni sawa na soko la kununua au kuza kura huku akisema sasa hawana nafasi.

Pamoja na hilo alisema chama hicho hakitamwacha yeyote atakayehuska katika rushwa, wakati ikielekea kwenye Uchaguzi Mkuu mwaka 2020.

Kauli hiyo aliitoa alipokuwa akizungumza na wanachama wa CCM Jimbo la Kawe, ambapo alisema kuwa rushwa imekuwa ikifanywa kwenye soko la kura imekuwa chanzo cha mvurugano wakati wa kuelekea katika chaguzi, suala ambalo halitavumiliwa.

Alisema matokeo ya rushwa katika kutafuta nafasi za uongozi yamekuwa na maumivu kwa wagombea na kusababisha kupata vipongozi wasiostahili, ambao mwisho wake hawawezi kuwa watumishi wa wananchi.

“Rushwa inayotumika kwenye soko la kununua kura imewaumiza wengi. Imeumiza wote, walioshinda na walioshindwa kwa sababu wote wanajikuta katika madeni.  Walioshindwa hawana raha wanaendelea kuugulia wakiwa hawajui ni kwa namna gani watarejesha kile walichopoteza.

“Kwa upande wa walioshinda, pia wanakuwa hawana raha, muda wote wanawaza kutafuta fedha kwa ajili ya kulipa madeni. Hawawezi kuwa na muda wa kuwasikiliza na kuwatumikia waliowachagua kwa kuwa wanaona kuwa wamenunua nafasi hizo,” alisema Dk. Bashiru

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles