28.2 C
Dar es Salaam
Friday, November 15, 2024

Contact us: [email protected]

CCM YALIA NA NIDHAMU, MAADILI KWA VIONGOZI

Na NORA DAMIAN-DAR ES SALAAM


CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Ilala, kimesema nidhamu na maadili ya viongozi bado ni tatizo kubwa kwani kumekuwa na kutoheshimiana kati ya wanachama na viongozi, jambo ambalo ni hatari kwa chama.

Mwaka huu CCM kinaadhimisha miaka 40 tangu kuanzishwa kwake na kimejielekeza kufanya makongamano mbalimbali kuelekea kilele cha maadhimisho hayo yanayofanyika Februari 5 kila mwaka.

Wilaya ya Ilala walifanya kongamano hilo jana ambapo mada mbalimbali zilijadiliwa zikiwamo ‘Miaka 40 ya CCM changamoto na mafanikio yake, Uchaguzi wa CCM na jumuiya zake na Mikakati ya ushindi dhidi ya upinzani’.

Akifungua kongamano hilo, Mwenyekiti wa CCM Ilala, Assah Simba, alisema chama kinaongozwa kwa kufuata taratibu, kanuni na miongozo hivyo ni vizuri wanachama na viongozi wakazingatia ili kuepuka kukipeleka chama kusikotarajiwa.

“Acheni udalali wa kisiasa unaoweza kuwaletea madhara kwa sababu CCM hakina madalali, tusome Katiba ya chama chetu ituongoze kwenda kule tunakotarajia. Hatutaki migawanyiko isiyokuwa na tija, tuwe na dhamira moja ya kukitumikia chama na si kuwa na dhamira mbadala,” alisema Simba.

Naye Kada wa chama hicho, Dk. Lucas Kisasa, ambaye aliwasilisha mada kuhusu ‘Miaka 40 ya CCM changamoto na mafanikio yake’ alisema licha ya kufanikiwa kushika dola lakini bado kinakabiliwa na changamoto ambazo zimesababisha kuwapo kwa mitafaruku na mipasuko.

Dk. Kisasa aliainisha baadhi ya changamoto hizo kuwa ni upungufu wa mapato ya chama katika ngazi zote, udhibiti hafifu wa miradi na kushindwa kutunza na kukarabati rasilimali zilizopo. 

“Nidhamu ya maadili imekiathiri chama, mtu hawezi kuchaguliwa hadi atote fedha mambo yote haya yanapunguza mvuto wa chama kwa wananchi, CCM kijiimarishe kihakikishe kinapata viongozi sahihi bila rushwa au ujanjaujanja,” alisema Dk. Kisasa.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Dar es Salaam, Ramadhani Madabida, alisema wakati wanaadhimisha miaka 40 ya chama hicho wanajivunia kuwapo kwa mafanikio makubwa katika kukuza demokrasia.

“Licha ya kushika dola marais wamekuwa wakiachiana madaraka, kwa hiyo haya ni mafanikio makubwa hasa katika kukuza demokrasia, wako wenzetu wanapigana vita kwa sababu tu ya kukataa kuachia madaraka,” alisema Madabida.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles