23.6 C
Dar es Salaam
Wednesday, September 27, 2023

Contact us: [email protected]

ASALI INA FAIDA KUBWA KWA AFYA NA KIPATO

Na George Mshana


Wajasiriamali wanaouza asali pamoja na wadau wote wa asali, wametakiwa kuwaelimisha Watanzania manufaa yatokanayo na matumizi ya asali na mchango wake mkubwa katika kukuza uchumi na kupata wateja wengi.

 Hayo yamesemwa na mdau wa asali, Sosthenes Sambua, katika mahojiano maalumu jijini Dar es Salaam hivi karibuni.

“Matumizi ya asali hapa nchini ni madogo. Watu hawana taarifa ama uelewa sahihi kuhusiana na manufaa ya asali.

“Tunahitaji kufanya kampeni maalumu ya kuelezea manufaa ya asali kiafya ili watu wayafahamu na kununua asali na hii itasaidia kuwa na soko kubwa la ndani la asali na mahitaji ya asali yataongezeka. Kutoa elimu kwa umma kuhusiana na umuhimu wa asali ni muhimu sana,” anasema.

Ameviomba vyama vya wafugaji nyuki viangalie uwezekano wa kupunguza bei ili kuwawezesha watu wengi zaidi kumudu kuinunua.

Tusiiachie Serikali jukumu la kutangaza asali, wafanyabiashara wenyewe waitangaze na kuelimisha jamii kuhusiana na umuhimu wa kutumia asali,” anasema Sambua.

Bei ya asali ni tofauti kulingana na ubora na mahali ilipotoka.Yule mtumiaji ndiye anaamua anunue asali ipi kulingana na ubora na vionjo tofauti. Namna ambavyo utamuelezea mteja manufaa atakayoyapata baada ya kutumia, ndivyo utamshawishi anunue hiyo asali.

Mfumo wa ufuatiliaji wa bidhaa ni muhimu kwa mjasiriamali kujua mahali asali inapotoka au ilipopatikana ili kujua mazingira ya utunzaji.

“Njia mojawapo ya kufuatilia ubora wa asali ni kwenda na ndoo zako kwa mfugaji ili uweze kukusanya kwenye vyombo safi na vya uhakika. Changamoto kubwa inayowakabili wajasiriamali wa asali ni kupata masoko mengi ya asali, kupata pia machujio bora na imara ya kuchuja asali. Asali iliyochujika vizuri na safi ndiyo yenye kuvutia walaji wengi. Maduka makuu na makubwa ya vyakula na vifaa [supermarkets], hutoa masharti magumu ambayo wajasiriamali hushindwa kuyamudu, hivyo kutoweza kuwauzia bidhaa zao,” anasema Sambua.

Naye mdau wa asali, Deo Kahwa, anasema kuna mafunzo ya kutoa elimu ya ujasiriamali kwa vijana ili waweze kuanzisha biashara zao na kujikwamua kiuchumi.

Hata hivyo, anawahadharisha wafugaji wa nyuki kujitenga mbali na yalipo mashamba ya  tumbaku.

“Nyuki huweza kula asali itokanayo na maua ya tumbaku ambayo huweza kuwa na sumu ya Nicotin. Baraza la Asali liliwataka wajasiriamali wasichukue asali ambayo ipo karibu na tumbaku, kwa sababu tumbaku ina Nicotin ambayo si nzuri kwa afya ya mlaji,” anasema Kahwa.

Ubora wa asali hujulikana kwa kuwa na kiasi kidogo cha maji ndani yake. Ni vyema asali ikavunwa wakati wa jioni kwani unyevu angani hupungua. Inashauriwa pia kuwa unapovuna asali uiweke juu ya kitu cha mbao.

Wadau wa asali wanatakiwa kuzingatia zana za kisasa na ufungashaji wa kisasa wa asali. Ni muhimu kuhifadhi mahali pasipo na joto kali kwani joto kali huibadili rangi asili ya asali pamoja na ladha. Huharibu pia vimeng’enyo vilivyomo ndani ya asali.

“Kabla hujauza nje asali yako lazima uzingatie viwango vya ubora vya nchi unayotaka kuipeleka ile asali yako. Marekani wana viwango vyao, Umoja wa Ulaya wana viwango vyao na Canada wana viwango vyao. Serikali iendelee kutengeneza mazingira, tuingie kwenye soko, tujielimishe, kiwango kipitiwe.

“TFS wametuambia wanaongeza kasi ya kutoa elimu kwa umma kuhusiana na asali. Tutaendelea kuzungumza na wanaouza nje asali, wameanza mchakato wa kutoa vyeti kwa bidhaa ambazo zina uhalisia [organic]. Kuna fursa kubwa kwenye soko la nje kwa asali ya Tanzania, hivyo Watanzania waitumie vizuri fursa hiyo,” Kahwa anasema.

Mjumbe kutoka TANTRADE, anasema wataendelea kutangaza mazao ya asali. “Imeonekana elimu inahitajika kwa watumiaji wa asali. Wadau wengi wamesema kuna changamoto kwenye mnyororo wa thamani wa uzalishaji kuanzia kule zinapozalishwa hadi kumfikia mlaji. Kuna haja ya kuongeza juhudi ya kutoa elimu kuhusiana na umuhimu wa kutumia asali. Asali inaweza ikawainua kiuchumi wafanyabiashara na kupunguza umasikini na kutengeneza nafasi za ajira,” anasema.

Japhet Sanga, Mtaalamu wa mfumo wa ufuatiliaji wa chanzo cha asali au mahali asali ilipotoka, anasema lengo kuu la mfumo huo ni kufuatilia kuanzia asali ilipotoka hadi inapomfikia mtumiaji.

“Ataenda duka kuu la kujihudumia la vyakula na vifaa, ataingiza batch number na ataweza kupata taarifa ambazo zimezalisha ile asali, hii itamwambia jina la wilaya na kijiji ambapo asali ilivunwa. Ukiingiza namba, utapata maelekezo ambayo watayapata kwenye kompyuta na wataona mfugaji ambaye amesajili kwenye mfumo na maelezo yote yanayomhusu,” anasema.

Anasema mfumo huu unatoa cheti kwa wale waliosajiliwa na itaonesha fomu ya maombi, inafanyika kwa vikundi vya masuala ya nyuki.

Anasema mtu anayetaka kufanya biashara lazima awe amesajiliwa ndipo watu watamwamini na kufanya biashara na yeye.

Utachagua aina ya usafiri unaotaka kuutumia kusafirisha bidhaa yako na taarifa za dereva mwenye leseni na taarifa za ule mzigo ambao unataka kuusafirisha. Chombo cha kubebea asali kama ndoo, unakipa namba ambayo inaitwa batch number. Batch number itatoa taarifa, asali imetoka wapi, imechakatwa vipi na imesafirisha vipi.

Mfumo utahusika na wafugaji wote na wafanyabiashara wote ambao wanafahamika. Wakati anapewa kibali, afisa ataziingiza zile taarifa zote kwani atajaza fomu.

Wajasiriamali wa Tanzania wanatakiwa wawe na asali bora na nzuri ili waweze kupata soko na vifungashio bora ili kumvutia mlaji kuinunua.

“Mfumo wa ufuatiliaji unatusaidia sisi tunaofanya biashara ya asali. Tukiweka mfumo ambao utadhibitiwa, wafanyabiashara toka nje hawatakuwa  tishio. Sisi wa ndani tujitahidi kufanya biashara, tuwe na bidhaa nzuri na soko liwe zuri, tutaweza kushindana na wafanyabiashara kutoka nchi nyingine hasa jirani zetu.

“Kama tukiweza kufanya kama mfumo unavyotaka, tutafanya biashara kwa furaha. Tukishakuwa na takwimu ya wafugaji, mfanyabiashara wa nje akija atasajiliwa kwenye mfumo na kufuata taratibu zote za kibiashara. Ni vizuri kwa wafanyabiashara toka nje wakija Tanzania kwani inaongeza ushindani wa kibiashara na kuwafanya wafanyabiashara wa Tanzania kuongeza ubora ili kuvutia wateja. Na hii itaongeza ufanisi,” anasema.

Ni muhimu wajasiriamali watafute masoko ya asali kwa bidii wakiwa na lengo la kufikia viwango vya kimataifa ili kuweza kuuza asali katika soko la kimataifa. Kuboresha mazingira ya ufugaji ni muhimu sana pia ili kuhakikisha kuwa kuna mazingira ya usafi wa hali ya juu. Ni muhimu  wakapewa  mwongozo wa kusafirisha asali kutoka sehemu moja kwenda nyingine kwa kuzingatia vigezo vya kimataifa ili kuweza kumudu soko.

Asali ina manufaa mengi ikiwamo virutubisho vingi vinavyoifanya iwe ni chakula bora na dawa madhubuti ya kutibu magonjwa mengi. Kutokana na kuwa na kiasi kikubwa sana cha sukari, huifanya asali iwe na tabia ya kuua na kuzuia vimelea kuzaliana na kukua. Asali pia ina vimeng’enyo (enzymes) ambavyo hutengeneza kemikali iitwayo Hydrogen peroxide (H202), kemikali hii ina uwezo wa kuua bacteria wengi kwa wigo mkubwa na pia asali ina tindikali nyingi kuiwezesha pia kuua vimelea. Asali ina vitamini na madini mbalimbali yanayoifanya iwe ni moja ya vyakula bora duniani.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,729FollowersFollow
574,000SubscribersSubscribe

Latest Articles