32.1 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 26, 2024

Contact us: [email protected]

CCM YAFUTA UCHAGUZI KATA 42

Na NORA DAMIAN
DAR ES SALAAM

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), kimefuta uchaguzi katika kata 42 na kuamuru urudiwe upya.

Uamuzi huo umefikiwa baada ya Mwenyekiti wa Taifa wa chama hicho, Rais Dk. John Magufuli,  kupokea kero na malalamiko ya uchaguzi ya wanachama na kuagiza ufutwe na kufanyika upya.

Kata zilizoathirika na uamuzi huo ni pamoja na kata zote za Wilaya ya Simanjiro, mkoani Manyara ambazo zimefutiwa uchaguzi huo.

Akizungumza katika ofisi ndogo za chama hicho jijini Dar es Salaam jana, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Humphrey Polepole, alisema wamebaini kuwapo kwa uonevu na kutotenda haki katika mchakato wa uchaguzi, huku baadhi ya viongozi wakibainika kupanga safu za uongozi.

“Upo ushahidi wa wanachama unaonesha kuna viongozi ambao wameshindwa kutoa usimamizi mzuri wa mali za chama, lakini bado wamerejea na wengine wameomba dhamana ya uongozi katika maeneo ambayo wao si wakazi.

“Pia kuna mahali ambapo tumepitisha jina la mgombea mmoja tu wakati kuna wanachama wengi wazuri. Yaani hapo vikao havikupewa taarifa sahihi kuhusu mgombea, hali hii haikubaliki.

“Tusingependa kuona uchaguzi unanajisiwa kwa vitendo na mienendo inayokwenda kinyume na mageuzi makubwa ya chama chetu.

“Chama chetu kinaongozwa kwa mujibu wa Katiba na kama kuna viongozi waliokiuka kanuni na maadili ya chama, watachukuliwa hatua stahiki.

“Kamati za usalama na maadili zitawahoji watu hawa na kupitia vikao tutachukua hatua stahiki.

“Kiongozi ambaye ataweka ubinafsi kwenye uchaguzi, chama kinazo adhabu nyingi na mojawapo ni kumsimamisha ili kupisha uchaguzi na vikao vya chama vitaendelea kuona adhabu stahiki,” alisema.

Mbali ya Simanjiro, Polepole alizitaja kata nyingine zilizofutiwa uchaguzi huo kuwa ni Wilaya ya Ilala ambazo ni Buguruni, Liwiti, Kariakoo, Mchafukoge, Gerezani, Segerea, Pugu, Pugu Stesheni, Kitunda na Ukonga.

Kwa upande wa Wilaya ya Kinondoni, alizitaja kuwa ni Ndugumbi, Makumbusho na Msasani wakati katika Wilaya ya Ubungo ni Manzese, Mabibo na Makuburi.

Nyingine ni Kiburugwa, Kilungule na Mianzini zilizoko Wilaya ya Temeke, Serya iliyoko Kondoa Mjini, Lumemo iliyoko Kilombero, Mapinga ya Bagamoyo na Kata ya Kigamboni.

Alifafanua kuwa, katika baadhi ya kata, uchaguzi kwa nafasi zote umefutwa wakati kata nyingine nafasi zilizofutwa ni mwenyekiti na katibu.

Kuhusu makundi, alisema wanaoendeleza chuki ni wasaliti kwani anapopatikana mgombea mmoja, wana CCM wote wanapaswa kuwa pamoja na kumuunga mkono kuhakikisha anashinda kwa kishindo.

Kutokana na hali hiyo, aliwataka viongozi wa chama hicho kuendelea kusimamia katiba, kanuni za uchaguzi na maadili ya chama chao.

“Tunataka aina ya viongozi ambao wanapiga vita rushwa, ubadhirifu wa mali ya umma na kutoa taswira njema ya kukirejesha chama kwa wanachama.

“Hivyo basi, nawaomba viongozi wa chama  pamoja na wanachama kwa ujumla wao, waendelee kukipenda chama chao kwani kila tutakapobaini hujuma zozote, tutachukua hatua kadiri inavyowezekana,” alisema Polepole.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles