27.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 18, 2024

Contact us: [email protected]

MISHAHARA MIPYA Z’BAR YALETA UTATA

Na VERONICA ROMWALD

-DAR ES SALAAM

SAKATA la nyongeza ya mishahara kwa kiwango cha asilimia 104 limezidi kuchukua sura mpya visiwani Zanzibar, baada ya Jumuiya ya Wawekezaji wa Sekta ya Utalii Zanzibar (ZATI) kupinga hatua hiyo.

Uamuzi huo uliofanywa hivi karibuni na Waziri wa Kazi, Uwezeshaji Wazee, Vijana, Wanawake na Watoto, Maudline Castico, umeonekana kupingwa na waajiri hao wakidai kutoshirikishwa katika kufikia uamuzi huo.

MTANZANIA ilimtafuta Waziri Castico ili kupata kauli ya Serikali juu ya hatua hiyo, lakini hakuweza kutoa ushirikiano kwa mwandishi wa habari na badala yake alikata simu baada ya kusikia maelezo.

Waziri Castico ambaye alipigiwa kwa simu yake ya kiganjani namba 0652…348 hakuweza kutoa ufafanuzi baada ya kuulizwa swali kuhusu madai hayo, kwani alikata simu.

Pamoja na hali mwandishi alimtumia ujumbe mfupi kwa njia simu uliosomeka. “Habari mheshimiwa Waziri ….ni mwandishi wa gazeti la MTANZANIA nahitaji kupata kauli ya Serikali juu ya malalamiko yaliyotolewa na Jumuiya ya ZATI,” ulisema ujumbe huo ambao haukujibiwa.

Kutokana na hali hiyo gazeti hili lilimtafuta Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Mohamed Abood, ambapo naye alisema kwa sasa hana mamlaka ya kuzungumzia suala hilo.

“Siwezi kulizungumzia jambo hilo hivi sasa, sisi hatutoi kauli kwenye jambo hilo kwa wakati huu lipo chini ya ofisi ya waziri husika (Castico) bado halijafikishwa kwetu,” alisema.

MTANZANIA lilimfahamisha kwamba kwa mujibu wa ZATI tayari suala hilo limewasilishwa pia katika Ofisi ya Rais.

“Hata wakiwasilisha ni sawa lakini sisi hatuwezi kuzungumza kwa sababu tumepokea kutoka kwao, kwa mujibu wa taratibu za kiserikali tunazungumza pale tunapokuwa tumepokea taarifa kutoka kwa Waziri mwenye dhamana.

“Kwa hiyo, jambo hilo anayepaswa kulizungumzia hivi sasa ni waziri husika, mtafute… umesema hajapokea wala kujibu ujumbe mfupi, naye ni binadamu inawezekana amebanwa hivi sasa (jana)  kwa hiyo ni vema ukaendelea kumtafuta.

“Lakini ikiwa waziri husika atawasilisha taarifa hiyo kwetu kwa mujibu wa utaratibu wa kisetikali hapo tutazungumza,” alisema

Mwishoni mwa wiki Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wawekezaji wa Sekta ya Utalii Zanzibar (ZATI), Seif Masoud Miskry, alisema wanashangaa kulaumiwa kukwamisha kutolipwa kwa mishahara mipya.

Alisema licha ya Waziri Castico kutangaza kima kipya cha mshahara kwa wafanyakazi wa sekta binafsi hakuna sehemu yoyote wao kama wadau waliposhirikishwa zaidi ya uamuzi binafsi wa kiongozi huyo.

“Tuliwasiliana na waziri mwenye dhamana (Castico) na kutuambia tuendelee kulipa mishahara ya zamani wakati malalamiko yetu yakiendelea kushughulikiwa na Serikali,” alisema.

Mwenyekiti huyo alishangazwa na hatua ya waziri kwa sasa kuwatumia maofisa wa ofisi yake kupita kwenye ofisi mbalimbali na kuwataka wamiliki wa makampuni binafsi kuanza kulipa mishahara hiyo, huku malalamiko yao yakiwa hayajafanyiwa kazi.

Naye Mlezi wa ZATI ambaye pia ni Mwakilishi wa Tunguu, Simai Mohamed Said (CCM), alimwomba Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein aingilie kati sakata hilo kuokoa sekta ya utalii nchini.

Alisema wageni hao Zanzibar hushindana na nchi kama Thailand, Tunisia, Morocco, Spain, Visiwa vya Ugiriki kama Crete, Mexico, Cuba, St. Lucia pamoja visiwa vingine.

Alisema wanaouza nafasi za hoteli kwa Zanzibar kwa nchi za Ulaya tayari wanaanza kuona Zanzibar ni bei ghali hasa ikiwa mishahara itapanda kupindukia na wao itawafanya wapandishe bei.

“Ninamwomba Rais wetu Dk. Ali Mohamed Shein aingilie suala hili maana kauli yake inaweza kunusuru ajira za Wazanzibari pamoja na wawekezaji wa utalii ambao sasa huenda wakakumbwa na mzigo mkubwa wa gharama na nchi yetu ikajikuta ikishuka kwenye utalii.

“Kama waziri Castico alikuwa na nia njema kwa nini hadi sasa anawaogopa wawekezaji hao wa hoteli kufanya nao kikao cha pamoja?,” alihoji.

Mabadiliko hayo yamefanyika kwa mujibu wa kifungu cha 97 (1) cha sheria ya Ajira nambari 11 ya mwaka 2005 ambapo kima cha chini kwa wafanyakazi  wenye mikataba ya maandishi kwa taasisi ndogo zitakazoainishwa kwenye kanuni kimeongezeka kutoka Sh 145,000 hadi 180,000 Kwa wafanyakazi wenye mikataba ikiongezwa kutoka kiwango cha sasa cha Sh 145,000 hadi 300,000.

Kwa vibarua wa kutwa wenye ujuzi, kima kimeongezwa kutoka Sh 10,000  hadi 30,000  kwa siku na kwa vibarua wa kutwa wasio na ujuzi, kimeongezwa kutoka Sh 7000  hadi 25,000.

Takwimu mbalimbali ikiwemo za Serikali zinaonyesha kati ya asilimia 100 kuna watalii zaidi ya asilimia 40, ambao huingia Zanzibar moja kwa moja  ambao hununua likizo zao kwenye makampuni yanayouza mapumziko katika visiwa tofauti duniani huko Ulaya.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles