25.6 C
Dar es Salaam
Monday, November 25, 2024

Contact us: [email protected]

CCM shangilieni lakini kumbukeni meli ikizama tutazama wote

5t7a3137

Na BALINAGWE MWAMBUNGU,

KATIKA ulimwengu wa leo, hakuna ‘classified information’ (taarifa za siri). Teknolojia imekwenda mbele sana kiasi kwamba hata kitu kilicho chini ya ardhi; kwa mfano madini, huonekana kwa vipimo maalumu kwa kutumia ndege ya uchunguzi.

Nakumbuka enzi zile, makambi yote ya jeshi letu kulikuwapo na matangazo yaliyoandikwa kwenye vibao: ‘Hairuhusiwi kupiga picha’. Sasa hivi anayetaka kupiga picha si lazima aje Tanzania, anaweza kupiga picha ya makambi ya jeshi la nchi akiwa nje ya Tanzania na anaweza kujua aina ya silaha tulizonazo.

Nakumbuka yule Mmarekani, Edward Snowden, ambaye anaendelea kusota nchini Urusi kama mkimbizi kwa sababu ya kuweka bayana mambo ya wakubwa ambayo wao waliyaweka kuwa siri. Snowden ameifungua macho dunia kiasi kwamba viongozi hawawaamini hata wateule wao.

Inafika mahali kiongozi anamaliza mkutano wa Baraza la Mawaziri halafu anasema nendeni mkawaambie; yaani wakawaambie waandishi wa habari kilichojiri kwenye baraza.

Tulinong’onezwa kipindi fulani kwamba mkuu wa kaya aliwashangaa wateule wake alipokutana nao kwenye Baraza la Mawaziri, kila mjumbe alikuja na ama chupa ya chai au maji ya kunywa. Hawakugusa chai na maji ambayo kwa kawaida huwa wanaandaliwa wajumbe.

Inaelezwa kwamba mkuu akashangaa. ‘Tumefika huko?’ Hii ilitokana na baadhi ya wateule kuugua magonjwa yasiyojulikana kutokana na vyanzo vya kukisiwa sabuni ya kunawa mikono au taulo la kufuta mikono vinavyowekwa maliwatoni au kutiliana sumu inayoua pole pole kwenye chai au chakula ofisini.

Alikuwapo mwandishi wa gazeti la ‘Mfanyakazi’, Stanslaus Katabalo (RIP), aliugua ugonjwa usiojulikana, akafa katika kipindi kifupi sana, wengine wakasema alikuwa na Ukimwi, wengine wakasema aliwekewa sumu ama kwenye kinywaji au chakula.

Alikuwa anapenda ulabu tena pale mtaani karibu na ofisi za ‘Mfanyakazi’ palikuwa na bar na mgahawa. Kila mchana wafanyakazi wa ‘Mfanyakazi’ walikuwa wanakula hapo.

Niliteuliwa kuwa Mhariri wa Mfanyakazi kuchukua nafasi ya Hamidi Nzowa (RIP), siku nyingi kidogo baada ya kifo cha Katabalo. Wasaidizi wangu wakanitambulisha kwa viongozi wa bar na mgahawa na nikapewa ofa ya chakula (nyama choma na bia).

Ilinichukua muda kufahamiana na wahudumu wa mgahawa huo. Lakini kilichonishangaza baadhi ya wateja pamoja na wafanyakazi wa ‘Mfanyakazi’ walikuwa na sehemu zao maalumu za kukaa na baadhi yao walikuwa na glasi zao maalumu za kunywa bia! Hii ni hatari sana kwa waandishi wa habari, hasa wanaofanya habari za uchunguzi.

Gazeti la Mfanyakazi, kupitia kalamu ya Stanslaus Katabalo, ndilo lililoibua ‘kashfa ya Loliondo’ na liliandika makala nzito nzito ambazo ziliwagusa baadhi ya mawaziri na watendaji serikalini.

Hawakujiuzulu. Ilibidi Rais Ali Hassan Mwinyi wakati huo, afanye mabadiliko katika Serikali yake, lakini hakuna aliye ‘tumbuliwa jipu.’

Hii inatokana na sababu kuu mbili; Watanzania hatuna utamaduni wa kujiuzulu, acha ile wanayosema kubeba mzigo kwa ajili ya kosa ambalo limetendwa na watu waliokuwa wanatekeleza hayo waliyoyafanya yalikuwa ni maagizo kutoka mamlaka ya juu zaidi.

Kwa mfano chanzo cha skendo ya Loliondo ilikuwa ni uamuzi wa Serikali kumpa eneo Tengefu la Loliondo Brigedia Mohammed Abdurahim al-Ali wa Falme za Emirates. Safari yake ya kwanza alikuja na familia yake na marafiki kuja kuwinda wanyama, walifanya uharibifu mkubwa sana kwa kuua wanyama ambao hawakutakiwa kuwaua.

Kama watu wamefanya uamuzi wa pamoja, hakuna mtu atakayeambiwa awajibike lakini yako matukio mengine yanafanywa na ofisa wa juu kabisa au mkuu wa idara, nani atamwajibisha?

Mfano mtu bila kufanya utafiti au upelelezi, anatangaza jambo fulani (akijua si la kweli), ili kumfurahisha mkuu wa kaya. Huku ni kujipendekeza ili aonekane kuwa mtendaji mzuri.

Juzi juzi hapa, Rais wa Mali, Ibrahim Boubacar Keita, amemfuta kazi Waziri wa Ulinzi, Tieman Hubert Coulibaly, baada ya kikundi cha kigaidi kuteka kijiji kimojawapo nchini humo.

Jambo hili linafikirisha. Kwani kazi ya waziri ni kulinda nchi? Kwanini asifukuzwe kazi mkuu wa majeshi?

Hapa nyumbani maofisa watano wa polisi wameuawa na watu wasiojulikana, hakuna aliyewajibika kana kwamba matukio hayo yalikuwa jambo la kawaida! Nani alipaswa kuwajibika, Mkuu wa Operesheni au ni Mkuu wa Jeshi la Polisi?

Vivyo hivyo, wakuu wa taasisi za umma, mawaziri na wakurugenzi panapotokea jambo fulani ambalo limeifedhehesha nchi na jamii ya Watanzania, waliokubali kupokea fimbo ya uongozi, wawe tayari pia kuwajibika kwa makosa ya maofisa walio chini yao.

Rais Ali Hassan Mwinyi, alijiuzulu akiwa Waziri wa Mambo ya Ndani baada ya watu kurundikwa rumande kule Butimba, Mwanza na baadhi yao kufa kwa kukosa hewa.

Nilianza na swali la je, kuna siri tena katika ulimwengu huu wa utandawazi? Siri kwenye utandawazi hakuna. Hata kwenye vikao vya vyama vya siasa, iwe ni kwenye Kamati Kuu vikao ambavyo waandishi wa habari wanafukuzwa lakini yaliyojadiliwa huvuja,  yanayozungumzwa ndani ya watumishi wa Serikali na taasisi zake yanavuja.

Mfano ni hili la kupungua kwa mizigo katika Bandari ya Dar es Salaam, wahusika walikanusha kwamba ulikuwa ni uzushi kumbe ni kweli. Jingine linalofuatana na hilo linaihusu Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), ambao nao walikana kwamba pamoja na habari za kupungua mizigo bandarini, mapato yao yalikuwa yanaongezeka jambo ambalo hawakuliweka wazi ili wasionekane kuwachongea Mamlaka ya Bandari (TPA).

Hawakutaka kueleza kwamba hatua ya Hazina kuzinyang’anya halmashauri za miji vyanzo vya mapato kama kodi ya majengo, imeiongezea mapato TRA na kwamba Sheria ya Kodi inayompa madaraka mtoza ushuru kumkadiria mfanyabiashara kodi, imewapa uwezo wa kuingiza fedha nyingi.

Lakini wanaogopa kumweleza Mkuu wa Kaya kwamba ili wafanyabiashara wajisikie kuwajibika kulipa kodi, sheria hiyo ingefaa ibadilishwe haraka. Wafanyabiashara wakubwa kwa wadogo wakipunguza kodi kwa kutoza asilimia ndogo ya mauzo, watalipa kodi kwa wingi na kwa hiari.

Hivi sasa, pamoja na uwepo wa mashine za EFDs, wafanyabiashara makini wanazitumia mashine hizo kwa mauzo au manunuzi makubwa tu. Mtu anakwenda dukani kununua shati moja au mawili kwa mfano, anatajiwa bei mbili kama unataka kutimiza ile azma; ukinunua kitu dukani, dai risiti bei yake iko juu na kama hutadai risiti, bei yake poa!

Mwisho kabisa viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wamekaa kimya hata pale mwenyekiti wao amevunja Katiba ya nchi kwa kupiga marufuku mikutano ya vyama vya siasa. Wao wamejawa na woga na hofu kwa sababu mkuu wa nchi amevaa pia kofia ya Mwenyekiti wa CCM (Taifa).

Rais Magufuli mara baada ya kuchaguliwa hakumung’unya maneno. Aliwaambia kwamba ndani ya chama hicho kuna ‘majipu’ na hivi sasa anasubiri muda mwafaka kufanya safisha safisha baada ya uchaguzi wa ndani mwaka ujao.

Kisirisiri watu waliokuwa mstari wa mbele kumpigia kampeni, wanasema hawakujua atakuwa hivi na wengine wanataka kofia ya Rais na Mwenyekiti wa Chama zitenganishwe. Wako pia ambao wanasema wazi kwamba 2017, hawatachukua fomu na kutetea nafasi zao.

Vijana wengi wa CCM wanashangilia kuwa mwenyekiti wao anavikomoa vyama vya upinzani, lakini wanasahau kwamba ‘Boma’ letu Tanzania, linapita katika mtikisiko mkubwa wa kiuchumi na waathirika wakuu ni watu wa hali ya chini.

Uchumi wa nchi unapita katika mdororo hata Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imeonyesha hivyo katika ripoti yake ya kila robo mwaka. BoT kwa mfano, imeonyesha kupungua kwa shughuli za kiuchumi katika sekta mbalimbali,  usafiri na usafirishaji kutoka asilimia 14.50 (2015) hadi asilimia 7.9 na sekta ya ujenzi 2015 ilikua kwa asilimia 13.8 sasa imeshuka kwa asilimia 4.30 ndani ya miezi 10.

Sehemu nyingi za ujenzi zimesimama, watu waliokuwa wanajikimu kwa njia hii wanahaha kutafuta vibarua. Sekta ya kilimo cha kujikimu ndio usiseme, nyanya 2015 sokoni Kariakoo ilinunuliwa kati ya Sh 1,800 hadi 300,000 sasa hivi ni kati ya Sh 6,000  hadi 8,000. Reja reja ilikuwa nyanya tatu kwa Sh 500 sasa nyanya nne – tano kwa Sh 300 lakini watu wanashangilia! Hii meli ikizama, tutazama wote!

Gavana wa BoT, Profesa Benno Ndullu, anasema uchumi wa Tanzania unatazamiwa kukua kwa asilimia 7.2. Lakini toka awamu zote tatu zilizotangulia, wananchi wamezoea kuambiwa hivyo kwamba uchumi unakua, lakini hawaoni mabadiliko katika maisha yao. Si siri kwamba uchumi wa vitabuni na uhalisia wa maisha haviendani.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles