Na. M. M. MWANAKIJIJI
MIAKA ile ya zama zile, ile miaka ya wakati ule ambao mambo ya aina ile na ile yalikuwa ni ya kawaida hatukupenda sana kucheza na wale waliojulikana kama “watoto mayai”. Labda msemo huu umepotea kwa wengi, lakini kwa ufupi watoto mayai walikuwa ni wale watoto ambao walikuwa wamedeka wakadeka halafu wakapitiliza hadi kudekeka.
Watoto hawa walikuwa ni wale ambao mkicheza mpira – cha ndimu – au hata “tiara bado” wao walikuwa wa kwanza kulia “nimeumia”. Yaani, hakuhitaji kupigwa ngwala; tishio la kupigwa ngwala tu mtoto wa watu alianguka chini na kuanza kulia. Ilikuwa ni kero sana kucheza mchezo wowote na watoto ‘mayai’.
Wengi wa watoto hao walikwazika kwa maneno tu; yaani ukimfokea kidogo tu uso unamuanguka, anajihisi kuumia moyoni, na anajiuliza kwanini yeye anaonewa hivyo.
Mtoto mayai hakuhitaji kufokewa, kukemewa wala kukataliwa. Kila anachotaka ilibidi apewe na asipopewa atanuna hadi mvua inanyesha! Siyo tu walidekezwa na wazazi na familia zao, hata jamii za karibu zilijikuta zinalazimika kuwadekeza, kwani wakiangusha kilio unaweza kufikiria ameangukiwa na kontena la vyuma!
Naogopa sana kuwa inawezekana utawala wa mfumo wa kifisadi uliozaliwa, kukomaa na kukua katika uongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), ulitujengea Taifa la watu waliodeka wakadekeka. Mfumo huu wa kifisadi ulijenga Taifa la watu waliodekezwa ambao hawakujua kukataliwa, kufokewa, kuulizwa na wala kubanwa. Watu walizoea maneno ya upole, ya kubembelezwa na kuchekewa wakati wanakemewa. Watu hao ukiwakunjia ndita tu walianza kuangusha vilio!
Katika mazingira yale, watu hawakuwahi kufikiria kuishi kwa mapato halali, wala kudhania wanaweza kufanya kazi halali na kuweza kujipatia kipato halali. Leo hii wapo watu wanapata shida sana kila ikitokea kupanda na kushuka kwa thamani ya fedha, wanapata shida kila mvua ikichelewa kunyesha kidogo, wanapata shida kila wakiona mawingu, kwani wanadhania ni gharika inakuja na kila jua likiwaka wanahofia ukame! Ndugu zetu hawa wakiona upepo umeongeza kasi kidogo wanahofia ujio wa kimbunga na dimbwi likianza kujaa maji wanaanza kulia “mafuriko” na wengine watasema ni “gharika”.
Ndugu zangu, tumefika mahali hadi inabidi kujiuliza kama ni kweli watu wanapokosoa wanakosoa kwa sababu za ukweli kabisa au ni kwa sababu ya kutoka mazoea ya aina moja na sasa ni mazoea mengine? Hivi ni kweli kabisa watu wanaamini ili uchumi uende vizuri basi shilingi isibadilike hata chembe, bei ya vitu isipande na kusiwepo kabisa mfumo wa bei? Kwamba, shilingi ikishuka dhidi ya dola, bei za vitu zikipanda na ukiwepo mfumuko kidogo wa bei basi ni kiama? Kwamba, sasa uchumi una hali mbaya, taifa linakwenda kuangamia?
Hivi ndugu zetu hawa kama ikitokea wakapata madaraka wanataka kutuambia kuwa katika miaka yao yote watakayokuwa madarakani, bei za vitu hazitabadilika, thamani ya shilingi itapanda tu hadi iwe karibu ya dola moja kwa shilingi moja? Kwamba, wakati wa utawala wao wenzetu hawa, mvua zitanyesha, mavuno yatakuwapo, na kila mtu atakula na kusaza? Kwamba, wao wakishika madaraka mapato yatakuwa ya uhakika wakati wote, na kila tatizo la kijamii na la kiuchumi linaloikabili Tanzania litatatuliwa ndani ya miaka miwili tu ya utawala wao?
Ndugu zangu, haina maana mtoto mayai hatakiwi kulalamika. Ni kweli wakati mwingine wanaumia kweli, lakini kwa tunaojua watoto mayai, tunajua kabisa, watoto mayai wakiumia kweli au wakikutwa na baya la kweli hawalii kama wanaojisingizia, watalia na utajua kweli hawa wameumia.
Tatizo ni kuwa, kumeanza dalili ya kuwepo kati yetu watu ambao wako kama yule mtoto aliyelia “mbweha, mbweha” wakati hakukuwapo na mbweha. Alilia hivyo kwa sababu alikuwa ameboreka kukaa kuchunga peke yake. Mwisho wa siku alipolia “mbweha” wakati mbweha kweli alitokea watu walisita kukimbia kumsaidia, kwani walijua anafanya utani wake tena!
Tusitengeneza taifa la watoto mayai, ambao hawataki kutoka jasho, hawataki kukemewa, hawataki kukataliwa, na hawataki kuambiwa. Na wale walioko madarakani na wao wasiwe kama watoto hao hao. Taifa zima la wananchi na viongozi wake wakiwa watu waliodeka na wanaodeka litakuwa ni taifa lililogumu sana kulijenga upya.