25.8 C
Dar es Salaam
Tuesday, April 16, 2024

Contact us: [email protected]

HATUSHIBI UZALENDO BALI CHAKULA

NA MARKUS MPANGALA

TUMEHABARISHWA mitindo mingi kuhusiana na suala la uzalendo. Uzalendo ni hali ya mtu kuwa tayari kuifia nchi yake. Ni ile hali ya kuwa mzalendo, kwamba mtu anayependa nchi yake na yuko tayari kuifia au mtu aliyezaliwa mahali fulani; mtu aliye mwenyeji au mwenye asili na mahali fulani alipozaliwa.

Wananchi tunahamasishwa kuwa wazalendo katika mataifa yetu. Mbiu ya uzalendo imeshika kasi kila mahali. Wananchi tunasisitizwa, tunabembelezwa na kuombwa. Na zaidi tunaweza kuzodolewa pia iwapo tunaonyesha dalili za ukaidi.

Zipo sura mbili kuu za dhana ya uzalendo katika mataifa ya Afrika, ambamo Tanzania imo. Sura hii ilikuwa na matokeo yake chanya na hasi, na baadaye ilichochea kuibuliwa kwa sura ya pili, tatu na nyinginezo kama zipo.

Sura ya kwanza ni kipindi cha ukoloni ambacho kilikuwa cha kupigania uhuru wa nchi yetu, hivyo mapambano yalikuwa dhidi ya wakoloni wa Ujerumani, Ureno, Kiarabu na baadaye Waingereza. Kipindi hiki kiliwataka wananchi kuungana na wapigania uhuru kwa hali na mali. Wananchi nao waliunga mkono, wanafanya kila waliloweza kuhakikisha wapigania uhuru wanafanikiwa. Licha ya changamoto za hapa na pale walizokutana nazo, lakini walifanikiwa.

Sura ya pili ni baada ya ukoloni, ambapo wananchi wanahimizwa kuzipenda nchi zao chini ya utawala mpya wa wenzao. Kipindi hicho ndicho wananchi wenyewe walishiriki kwa dhati katika kampeni za uchaguzi, kupiga kura na kufanya kila njia ili wagombea wao washinde. Bahati nzuri ni kwamba, licha ya kurejeshwa vyama vingi nchini, bado juhudi za kuhimiza uzalendo zilibaki. Uzalendo huo ulikuwa na sura ya masuala ya uchumi na maendeleo. Ni sura ambayo ilianzia kwenye uhuru ni kazi, mtu ni afya pamoja na watu na maendeleo.

Sasa Watanzania tunashiriki hamasa ya uzalendo katika kipindi hiki cha vita ya kiuchumi. Kipindi cha mabadiliko ya sera kutoka ile ya ukombozi hadi ya diplomasia ya uchumi. Vita hii ndiyo ambayo mwananchi anatakiwa kushiriki kwa maombi, sala, nguvu na maarifa yake yote kadiri anavyoweza. Mwananchi anahitaji kujikomboa na kufanikisha mambo mbalimbali.

Ninaunga mkono ajenda ya uzalendo kwa masharti ya dhahiri kama njia mojawapo ya kuwasaidia wananchi wetu ili kuondokana na matatizo yanayowakabili katika kaya, vijiji, kata, tarafa, wilaya, mikoa, kanda na taifani.

Septemba mwaka huu, nilitembelewa na rafiki yangu mmoja mwanahabari. Yeye hujishughulisha na masuala ya habari za vijijini katika maeneo mbalimbali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Katika harakati zake anameshuhudia mambo mengi ambayo hakuwahi kuyajua. Katika mazungumzo yetu alinisimulia tukio moja la wananchi wa kijiji fulani kushindwa kupata hata mlo mmoja wa siku. Aliniambia kuwa, imekuwa vigumu kwa wananchi hao kupata hata Sh 5,000 ya matumizi yao ya kila siku. Hapo ndipo ilipo mantiki yangu.

Iwapo mwananchi anashiriki zoezi la uchaguzi, kisha waliochaguliwa wanapaza sauti kuwa awe mzalendo kwa nchi yake, ni vema tukajiuliza swali muhimu; mwananchi huyo atashinda uzalendo au kwa kula chakula?  Mathalani, chaguzi zote barani Afrika zimekuwa zikitawaliwa na mambo matano ya kuzingatiwa zaidi:

Mosi, Mapambano dhidi ya rushwa. Katika eneo hili serikali yetu imepambana kwa kiasi gani kukomesha rushwa hadi iungwe mkono na wananchi wetu? Ni vema kuchakata mawaidha hayo kwa minajili ya kuweka sawa sura ya uzalendo tunayotakiwa kuivaa sasa.

Pili, utoaji wa haki na elimu. Wananchi wanapata haki zao stahiki? Hii ni katika mifumo ya vyombo vya utoaji wa haki; Jeshi la Polisi kama msimamizi mkuu wa ulinzi na usalama wa raia pamoja na mali zao.

Pia chombo kingine ni mahakama, je; inatoa haki kwa wananchi wetu? Kesi zilizopo katika mahakama zinazotugusa walalahoi zinasikilizwa na kuamuliwa kwa haki? Je, kesi tunazofunguliwa walalahoi tunabambikiziwa au tunakutwa na makosa ya kushtakiwa?

Ni namna gani wananchi wanaridhishwa na utoaji wa haki katika vyombo hivyo viwili kwa mfano? Tumeona uhusiano baina ya raia na Jeshi letu la Polisi si mzuri kiasi kwamba kumekuwa na manung’uniko mengi sana. Ninakumbuka kwenye moja ya mazungumzo yake na jeshi hilo, Rais Magufuli aliwahi kukemea tabia za kuwabambikizia kesi wananchi.

Vitu kama hivi vinatafsiriwa kuwa chanzo cha ukosefu wa haki. Mwananchi huyu anayekosa haki anawezaje kuwa mzalendo, au kwanini tumtarajie awe mzalendo kwa upande wake pekee, huku mamlaka za usimamizi wa haki hazina uzalendo kwake?

Kwenye suala la elimu pia inafaa kama mwananchi huyu anapatiwa elimu sahihi ambayo itamkomboa na kuondokana na kiwango cha ujinga. Kwa mujibu wa takwimu za Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia ya mwaka 2016, asilimia 23 ya Watanzania, wakiwamo vijana na watu wazima, hawajui kusoma na kuandika.

Mpango uliopo serikalini ni kuhakikisha kuwa hadi mwaka 2030 nchi iwe imeondokana na watu wasiojua kusoma na kuandika. Safi, lakini je, katika pambio ni kwanini tusiwaambie hawa wasiojua kusoma kuwa si uzalendo? Kwa sababu tuna rekodi ya kutokamilisha mikakati mbalimbali tunayoanzisha.

Tatu, mafanikio ya kiuchumi au vita vya kiuchumi. Kwamba kila mwananchi anapambana na hali yake, lazima ajiulize, napata nini katika hali yangu; Masoko ya bidhaa za uzalishaji, barabara, ajira, vipato (njia za kujipatia pato). Mazao yao yana soko? Bei iliyopo sokoni ni rafiki kwao?

Kama wanazuiwa kuuza nje mazao ya chakula, ni nani ndani ya nchi yetu atanunua ili wakulima wajipatie kipato? Au kwanini serikali isichukue hatua ya kununua mazao hayo kwa wakulima ili kuweka ghalani au kuyauza kwa mujibu wa taratibu na sheria?

Nne, mapambano dhidi ya ugaidi. Hali ya usalama duniani imekumbana na tishio la ugaidi. Watanzania ni miongoni mwao wanaopatikana hapa duniani. Je, usalama wa raia na mali zao unawaridhisha?

Naamini demokrasia ni pamoja na uhai wa mwananchi na ulinzi mipakani. Kwa hiyo, tunapotaka kuwaimbisha wananchi dhana ya uzalendo, tuwahakikishie kwanza mlo, si vinginevyo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles