31.7 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

NAFASI YA TANZANIA KATIKA UENEZI WA DIPLOMASIA YA ANC

NA ZITTO KABWE

MWISHONI mwa miaka ya 1980, dunia ilisimama pamoja kuupinga ubaguzi wa rangi nchini Afrika Kusini, ikisusia bidhaa za nchi hiyo na kukata mahusiano nayo ya kidiplomasia, mbinyo uliotishia kuangusha uchumi wa Taifa hilo.

Hatua hii ilimleta mezani Rais Frederik Willem de Klerk, kwanza kufuta uharamu wa chama cha ANC, kuwatoa gerezani wafungwa wote wa kisiasa, na kuanzisha majadiliano na ANC chini ya Hayati Nelson Mandela, juu ya mustakabali wa Taifa hilo, hatua iliyosababisha kuyakabidhi madaraka ya uongozi wa Taifa hilo kwa weusi wengi mara baada ya Katiba mpya iliyosababisha Uchaguzi Mkuu wa mwaka 1994.

Mafanikio hayo ya watu wa Afrika Kusini yana machozi, jasho na damu za wananchi karibu wote wanyonge wa Taifa hilo, wakipambana kwa umoja wao kudai haki na kupinga ukaburu, iwe ni gerezani, shule ama vyuoni, uhamishoni au hata mtaani Soweto.

Lakini mtu mmoja alifanya juhudi zaidi, anastahili tuzo zaidi, anastahili kupongezwa zaidi kwa mafanikio yale. Mtu huyo ni mzee wetu Oliver Reginald Tambo (marehemu), akitumia miaka zaidi ya 30 ya uhai wake (1960 – 1990) kuzunguka kuieleza dunia juu ya madhila ya Taifa lake na kuishawishi kuweka mbinyo utakaosaidia kuwaleta mezani watawala dhalimu wa kikaburu kuzungumza na wanyonge wengi weusi wa Taifa hilo.

Juhudi hizi za Oliver Tambo zilizaa matunda kwa dunia kuisusia na kuitenga Afrika Kusini, hatua iliyotishia kuuangusha uchumi wa Taifa hilo na kutishia masilahi ya kiuwekezaji ya mabeberu weupe (white monopoly capital), wakakosa njia zaidi ya kumwachia Mandela na wenzake pamoja na kuanza mazungumzo yaliyowaleta weusi madarakani. Amefanya kazi kubwa mno, Tambo ametimiza miaka 100 tangu kuzaliwa kwake, ni muhimu kuukumbuka mchango wake huo.

Tambo hakwenda jela kama Mandela, wala hakuwa mstari wa mbele kwenye mapigano kama Chris Hani, mchango wake kwa Taifa lake ulikuwa ni uwezo wake wa kujenga hoja kuifafanulia dunia juu ya mapambano ya Taifa lake, akitumia hekima, busara na njia ya amani kueneza diplomasia yake na kuilinda ANC dhidi ya migongano ya ndani. Kwangu Tambo ni kiigizo chema.

Tanzania ina nafasi ya kipekee katika mafanikio hayo ya ‘Diplomasia ya Tambo’, tulisimama kama ngazi yake ya kupanda kueneza diplomasia hiyo, tukimfungulia milango ya kila pahala alipotaka kutoa ushuhuda wa madhila ya Taifa lake, ndiyo maana wakati wa mazishi ya mzee Nelson Mandela, ni Rais Mstaafu Jakaya Kikwete pamoja na Kenneth Kaunda ndio walipewa nafasi ya kuzungumza kwa sababu ya nafasi yetu katika ukombozi wa Taifa hilo (Rais Joyce Banda wa Malawi akipewa nafasi ya kuzungumza kama Mwenyekiti wa AU wa wakati ule).

Desemba 15, 2013, dunia ilikumbushwa historia ya Tanzania juu ya ukombozi wa Afrika, kule kijijini Qunu, katika wasaa ule wa Misa ya kumuaga Shujaa wa Demokrasia na Ukombozi wa Afrika Kusini, Komredi Nelson Mandela. Rais Jakaya Mrisho Kikwete kwa fahari kabisa aliieleza dunia juu ya kila hatua za kiutu za kujitolea ardhi, rasilimali na hata watu ambazo Taifa letu lilizichukua kwa ajili ya Ukombozi wa Afrika ya Kusini.

Sehemu kubwa ya maisha yake mzee Tambo ameishi Zambia, lakini akija kila mara Tanzania kukagua hali za kambi mbalimbali za MK pamoja na kuhamasisha upazaji sauti wetu kama nchi kinara wa Ukombozi wa Afrika, tukiwa na makao makuu ya Kamati ya Ukombozi wa Afrika (African Liberation Committee) hapa nchini mwetu, na Watanzania wenzetu, mzee Oscar Kambona, Balozi Sebastian Chale, Balozi George Magombe na kisha Brigedia Jenerali Hashim Iddi Mbita, wakiiongoza kamati hiyo tangu kuasisiwa kwake mpaka ilipovunjwa baada ya ukombozi wa Afrika Kusini.

Nafurahi kuwa nyumba ya mzee Tambo aliyoishi katika miaka yake 30 ya uhamishoni pale Lusaka sasa imegeuzwa kuwa Makumbusho ya Taifa, hatua itakayosaidia mno kulinda historia hiyo isiyofutika, historia ya mchango wa Zambia katika ukombozi wa Afrika Kusini. Nasi tunapaswa kuiga hatua hii muhimu, ili kulinda historia ya Taifa letu.

Mwaka 1984, ANC walifukuzwa nchini Msumbiji, wakiagizwa wasiitumie ardhi ya nchi hiyo kama kichaka cha mapambano yao, hatua iliyopunguza nguvu na kasi ya mashambulizi ya wana MK ndani ya Afrika Kusini kwa kupitia Msumbiji, ikiwa ni matokeo ya Serikali ya Kikaburu ya Afrika Kusini kujibu mashambulizi ya Diplomasia ya OR Tambo iliyoanza kuwachafua duniani. Nchi kadhaa zikaanza kusita kuisaidia ANC.

Ndani ya kipindi hicho kigumu ikatokea ajali iliyosababisha kifo cha Waziri Mkuu wetu, Edward Moringe Sokoine, ajali ambayo ilihusisha gari ya ANC iliyoendeshwa na mwana ANC, mkazi wa kambi ya ANC ya Dakawa, Dumisani Dube. Aprili 12, 1984, ikawa siku iliyotikisa mahusiano ya Tanzania na ANC, maadui wa ANC wakitarajia kwamba tungewaondosha nchini kwa mtu wao kuhusika katika ajali iliyosababisha kifo cha Waziri wetu Mkuu.

Mzee Tambo alishiriki katika mazishi ya Sokoine kule Monduli, akiwa kichwa chini kwa huzuni na taharuki, akiwaza na kuwazua athari za msiba ule kwa ANC endapo Serikali ya Tanzania ingewafukuza. Rais Nyerere aliiona huzuni hii ya Tambo, baada ya msiba alimwandikia barua fupi, lakini yenye kuonyesha mshikamano wetu nao, barua iliyowahakikishia ANC na watu wa Afrika Kusini juu ya umoja wetu kwao.

Kisha Mei 2, 1984 mzee Tambo alikuja Mazimbu, Dakawa, Morogoro, katika kambi mashuhuri ya watu wa nchi yake, wakati huu yeye akiwa ndiye Rais wa ANC, nafasi ambayo alijiuzulu kumpisha Mzee Mandela mara baada ya kutolewa gerezani, alisema yafuatayo:

“Kwa hakika, ni nafasi ya kipekee kwangu kuja tena Mazimbu, kuja tena SOMAFCO (Solomon Mahlangu Freedom College), kuona majengo haya, kuona ngome hii, kijiji maalumu kilichojengwa kwa kujitolea pamoja na weledi, kikiwa ni mnara na ishara ya watu wa dunia kusapoti mapambano yetu, nina furaha kuwa hapa. Tunaishukuru sana Serikali ya Tanzania”.

Furaha ya miaka 100 ya Mzee Tambo. Mola amlaze pema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles