Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital
Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Dar es Salaam kimewahamasisha wananchi kujiunga katika vikundi vya kuweka akiba na kukopeshana maarufu Vicoba ili kujikwamua kiuchumi.
Akizungumza wakati wa sherehe za miaka mitano ya kikundi cha kikoba cha Tujijenge Pamoja kilichopo Kata ya Minazi Mirefu, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Dar es Salaam, Kate Kamba, amesema Vicoba vinawawezesha wananchi kuwa na maisha bora.
“Vicoba vinatusaidia sana mimi ninavyo vikundi vitatu na kwa Tanzania kinamama tunaheshimika sana kwa sababu Vicoba, pia ni sehemu ya kusaidiana…kikoba hiki lazima tukisimamie kifikie malengo yake,” amesema Kate.
Pia amewataka wanachama kuweka malengo kabla ya kuamua kukopa ili kuepuka kushindwa kurejesha mikopo hatua inayorudisha nyuma vikundi vingi.
Mwenyekiti huyo pia amewataka wanachama wa chama hicho kujitokeza kwa wingi kugombea nafasi mbalimbali za uongozi katika uchaguzi wa ndani unaotarajiwa kufanyika mwaka huu kwani kila mtu ana haki ya kugombea na kuchagua.
Aidha amewataka kujitokeza kwa wingi katika zoezi la sensa ya watu na makazi na kutoa ushirikiano kwa kujibu maswali yanayohitajika ili kuiwezesha Serikali kupanga bajeti yake vizuri.
“Tumuunge mkono mama Samia mambo aliyoyafanya ni makubwa, nia yake sisi wote tuishi maisha mazuri hivyo tumsaidie kuchapa kazi,” amesema.
Mwenyekiti huyo alikichangia kikundi hicho fedha taslimu Sh 100,000 na kuahidi kutoa mchango mwingine ili kukiwezesha kukabili changamoto ilizonazo. Naye Mwenyekiti wa kikoba hicho Hadija Magube, amesema kilianzishwa Machi 2018 na hadi sasa kina wanachama 30.
Hata hivyo amesema wanakabiliwa na changamoto kadhaa ikiwemo baadhi ya wanachama kutokuwa waaminifu na kushindwa kurejesha mikopo na kuomba wadau mbalimbali kujitokeza kuwachangia waweze kupata vyanzo vipya vya mapato ambavyo vinagharimu Sh milioni 21.4.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Kampuni ya Wahenga Alluminium ambaye alikuwa mgeni maalumu katika sherehe hizo, John Ryoba, ameahidi kutoa Sh 500,000 kuchangia kikundi hicho ili kiweze kutatua baadhi ya changamoto zinazowakabili.
“Nimekuwa mdau mkubwa wa kuchangia chama na nitaendelea kufanya hivyo kila mara, niko bega kwa bega na nyie kuhakikisha mnasonga mbele,” amesema Ryoba.
Mbali ya Ryoba wengine walioahidi kuchangia kikundi hicho ni Diwani wa Kata ya Kisukuru, Lucy Lugome (100,000), Madiwani wa Viti Maalumu, Rukia Mwenge (100,000) na Moza Mwano (100,000).
Mbunge wa Segerea, Bonnah Kamoli tayari alishatoa bati 20 kuezeka ofisi inayojengwa na kikundi hicho.