25.7 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

Khimji awatahadharisha wapanga safu za uchaguzi

Na Nora Damian, Mtanzania Digital

Naibu Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Saady Khimji amewatahadharisha walioanza kupanga safu za wagombea katika uchaguzi wa ndani wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) waache tabia hiyo kwani watakivuruga chama.

Khimji ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Ilala ameyasema hayo wakati wa hafla ya kumuaga aliyekuwa Mtendaji wa Kata ya Zingiziwa, Tatu Nyamoga aliyehamishiwa Kata ya Ukonga na kumkaribisha mtendaji mpya, Gerald Sarota.

Naibu Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Saady Khimji, akilishwa keki na aliyekuwa Mtendaji wa Kata ya Zingiziwa, Tatu Nyamoga, wakati wa sherehe ya kumuaga baada ya kuhamishiwa kata nyingine.

“Masuala ya 2024/25 hayo tumuachie Mungu na kama tunaamua tupange safu itakayokisaidia Chama Cha Mapinduzi na si kutuvuruga. Kama mnaona viongozi walioko madarakani waliwavusha basi muwaangalie kwa jicho la huruma.

“Fitina majungu, mapambano yetu tuliyoyazoea tuyaache, tukianza kuwatengenezea mazingira ya kuwaondoa tutakuwa tunatenda dhambi,” amesema Khimji.

Kuhusu mtendaji huyo Khimji amempongeza Diwani wa Kata ya Zingiziwa, Maige Maganga, aliyeandaa hafla ya kumuaga akisema amekuwa akijituma tangu alipoingia madarakani kuhakikisha kata hiyo inapata maendeleo.

“Ni jambo la kipekee na tunajifunza jambo la kimahusiano na hata mtendaji mpya anatakiwa kujifunza zaidi kwanini watu wote wameacha shughuli zao kuja kumuaga mtendaji aliyekuwepo. Ni kitu gani alichokuwa akikifanya kwa miaka sita, maana yake kilikubalika na viongozi wa chama na Serikali,” amesema Khimji.

Naye Diwani wa Kata ya Zingiziwa, Maige Maganga, amesema kata hiyo imenufaika na miradi mikubwa kama ya ujenzi wa madarsa 12, kituo cha afya chenye thamani ya Sh milioni 500, Sh milioni 100 za ujenzi wa Soko la Zingiziwa zilizotolewa na halmashauri, kuchonga barabara na kwamba nyingine ziko kwenye mpango wa kujengwa kwa kiwango cha lami.

“Mikakati yetu ya baadaye ni kuhakikisha Zingiziwa inapata mawasiliano na changamoto za wananchi tunazitatua kwa kushirikiana na viongozi wa kata na halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam,” amesema Maganga.

Akimzungumzia aliyekuwa mtendaji wa kata hiyo amesema amefanya kazi nzuri ndio maana alimuandalia hafla ya kumuaga kutambua mchango wake na kuzidi kujenga umoja na mahusiano mema.

Kwa upande wake Tatu ameshukuru kwa kuandaliwa halfa hiyo huku mtendaji mpya Gerald Sarota akiahidi kufanya kazi kwa bidii ili kuhakikisha Zingiziwa inapata maendeleo zaidi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles