Na Abducado Emmanuel, Dar es Salaam
MCHEZAJI bora wa dunia wa zamani, Muitaliano Fabio Cannavaro, amenogewa na mandhari ya Tanzania pamoja na ukarimu wa watu wa hapa walioonyeshwa, akiwa na kikosi cha magwiji wa zamani wa timu ya Real Madrid.
Cannavaro ameongozana na magwiji hao wenzake akiwemo winga, Luis Figo, Christian Karembeu na Ruben de la Red, waliocheza na kikosi maalumu cha wachezaji wa zamani wa Tanzania ‘TSN Tanzania Eleven’ juzi na Madrid kushinda mabao 3-1.
Akizungumza na MTANZANIA Ikulu jijini Dar es Salaam juzi, wakati wa chakula cha usiku walichoalikwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete, Cannavaro alisema amefurahishwa sana na mandhari ya Tanzania pamoja na walivyopokelewa vizuri na Watanzania.
“Tanzania ni sehemu nzuri sana, nimeipenda kwa kweli nawashukuru Watanzania kwa kutupokea vyema, sijui chochote kuhusu hapa lakini ni eneo bora sana,” alisema Cannavaro.
Cannavaro aliyecheza mechi hiyo vizuri katika eneo la beki ya kati, aliwapongeza pia wachezaji wa kikosi cha ‘TSN Tanzania Eleven’ kwa kucheza vizuri kwenye mechi hiyo licha ya kutofanikiwa kupata ushindi.
“Ilikuwa ni mechi nzuri sana yenye burudani, wapinzani wetu walicheza vizuri licha ya kutopata ushindi, lengo ilikuwa ni kutoa burudani na tumefanikiwa kwa hilo,” alisema.
Cannavaro alikuwa mchezaji bora wa Dunia mwaka 2006 baada ya kuiongoza timu yake ya Italia akiwa kama nahodha kutwaa ubingwa wa Kombe la Dunia mwaka huo kwa kuifunga Ufaransa kwa mikwaju ya penalti 5-3 baada ya timu hizo kutoka sare ya bao 1-1.