25.5 C
Dar es Salaam
Thursday, December 12, 2024

Contact us: [email protected]

Magufuli aangukia pua

Waziri John Magufuli
Waziri John Magufuli

Na Kulwa Mzee, Dar es Salaam

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu imewaachia huru Wachina wa ‘samaki wa Magufuli’ na kuamuru Jamhuri iwarejeshee vitu vyao ikiwemo meli ya Tawaliq 1.

Wachina hao Nahodha wa meli, Hsu Chin Tai na Wakala wa Meli ya Tawaliq 1, Zhao Hanquing waliachiwa jana kupitia hati ya Nole ya kuwaondolea mashitaka.

Hii ni mara ya pili kwa Wachina hao kuachiwa kwani mara ya kwanza waliachiwa na Mahakama ya Rufaa Machi 28 mwaka huu, walikamatwa tena na kushtakiwa upya kwa mashtaka hayo hayo yaliyofutwa jana.

Washtakiwa hao walikuwa wakikabiliwa na mashtaka ya uvuvi haramu katika Ukanda wa Uchumi wa Tanzania.

Akiiomba mahakama kuifuta kesi hiyo mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi, Isaya Harufani, Wakili wa Serikali Mwandamizi, Prosper Mwangamila alidai kesi ilikuwa inatajwa lakini wao wanaomba kuwasilisha maombi kwa ajili ya kuifuta.

“Mheshimiwa hakimu Jamhuri tunaifahamisha Mahakama kwamba hatuna haja ya kuendelea na kesi dhidi ya washtakiwa, maombi yetu tunawasilisha chini ya kifungu cha sheria namba 91(1) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA) ya mwaka 2002,” alidai Mwangamila na kuwasilisha.

Wakili wa washtakiwa, Kapteni Ibrahimu Bendera alikubaliana na maombi hayo na kuiomba mahakama ikiwezekana iwarudishie hati zao za kusafiria, meli iliyokamatwa pamoja na samaki waliokuwemo.

Wakili Mwangamila hakuwa na pingamizi, alidai vitu vyote watarudishiwa.

Hakimu Harufani alisema mahakama imekubaliana na maombi ya Jamhuri hivyo inawaachia huru washtakiwa wote na kuamuru warejeshewe vitu vyao vilivyokuwa vinashikiliwa.

Wakati mawakili wa pande zote mbili wakikubaliana vitu vyote vya washtakiwa hao virudishwe, Meli ya Tawaliq 1 maarufu kama ‘Meli ya Magufuli’ ilizama baharini wakati kesi ikiwa bado inaendelea.

Kuzama kwa meli hiyo kunatokana na Serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi kushindwa kuitunza tangu ilipokamatwa Machi 8, 2009 ikiwa na tani 293 za samaki aina ya Jodari iliyowavua katika Bahari ya Hindi ukanda wa kiuchumi wa Tanzania (EPZ) bila kibali.

Mbali na meli hiyo ambayo ina uwezo wa kuvua samaki kwenye kina kirefu baharini kuzama baada ya wajanja wachache kukata vyuma vyake na kuviuza, samaki waliokutwa ndani ya meli hiyo wanaokadiriwa kuwa na thamani ya zaidi ya shilingi bilioni mbili wote waligawiwa katika taasisi mbalimbali baada ya Waziri wa Mifugo na Uvuvi wa wakati huo, John Magufuli kudai kuwa Serikali haiwezi kufanya biashara.

Inaelezwa kuwa sehemu kubwa ya meli hiyo ambayo imetengenezwa kwa malighafi aina ya Brass ambayo kilo moja kwa sasa inauzwa kwa Sh 5,200, vyuma vyake karibu vyote vimekwisha uzwa na wajanja wachache waliokuwa wakipenya baharini kwa ajili ya kuvikata.

Uamuzi wa sasa umekuja wakati Machi 28 mwaka huu, Mahakama ya Rufaa iliwaachia na kuwafutia adhabu ya kifungo cha miaka 30 na faini ya jumla ya Sh bilioni 22 waliyopewa baada ya kutiwa hatiani na Mahakama Kuu Februari 23, 2012 kwa kosa la uvuvi haramu katika Ukanda wa Uchumi wa Tanzania.

Washtakiwa hao waliachiwa baada ya mahakama kubaini sheria zilikiukwa wakati wa uendeshwaji wa kesi hiyo katika mahakama za chini.

Hata hivyo, walikamatwa nje ya Mahakama kisha kufunguliwa kesi mpya yenye mashtaka yanayofanana katika Mahakama ya Kisutu, walidaiwa kwamba wote kati ya Januari 10, 2009 na Machi 8, 2009 kwa pamoja walivua samaki bila leseni katika Ukanda wa Bahari wa Uchumi wa Tanzania.

Kosa la pili kwa washtakiwa wote pia, walidaiwa kati ya Januari 10, 2009 na Machi 8, 2009 walichafua bahari na kuathiri viumbe vilivyomo ndani ya bahari kinyume na sheria.

Jamhuri ilidai shtaka la tatu kwa ajili ya mshtakiwa Zhao Hanguin ambaye ni wakala wa meli, anadaiwa huku akijua ni kosa kuvua samaki katika ukanda huo bila leseni alimsaidia mshtakiwa wa kwanza kukwepa kuchukuliwa hatua na kupata adhabu kwa kosa alilotenda.

Washtakiwa hao walikamatwa mwaka 2009 na boti ya askari wa doria wa nchi za Tanzania, Afrika Kusini, Botswana na ilibainika kuwa leseni waliyokuwa nayo ilikuwa imemaliza muda wake Desemba mosi, 2008.

- Advertisement -

Related Articles

5 COMMENTS

  1. Kwa nini mahakama zetu zishindwe kutoa uamuzi sahihi kwa swala nyeti kama hili tokea Machi 8, 2009, kitambo kirefu hivyo? Tatizo ni mahakama zetu kutokuwa na uwezo wa kutoa hukumu sahihi na kwa wakati muafaka, waziri John Magufuli hana kosa. Ikizingatiwa ni meli iliyokuwa imesheheni kiasi kikubwa hivyo cha samaki ambao wangeweza kuharibika au kugarimu kiasi kikubwa cha kuwatunza, hukumu sahihi ilibidi itolewe kwenye kipindi kizichozidi wiki moja.Waziri wa sheria kipindi meli ilipokamatwa awajibishwe kwa hili.

    • ALENI,naminakuunga mkono uko sahihi.MH JOHN MAGUFULI
      alitimiza wajibu wake,na mpaka sasa ni fundisho mchezo
      muchafu huo umekoma kabisa.kama mahakama imewachia ni sawa
      .Lakini fidia ya nini???

    • Ni kweli wanasheria wetu hawana taaluma ya kutosha na hivyo kuwa wababaishaji kwani wengi wao ni wale waliosomea kwenye vyuo vyetu vya kizalendo ambavyo hata kimoja sio miongoni mwa vyuo 1000 bora ulimwenguni. Pia kigezo cha ubora mara nyingi hakizingatiwi sana serikalini, na mara nyingi wanasheria waliobobea huwa wakichukuliwa haraka na sekta binafsi ambayo huwa ikizingatia na kulipa vizuri zaidi kuendana na ubora.

  2. hio ishu ni uonevu wa serikali zetu za kiafrika kinadharia ilikuwa sio big dili sana kiasi cha kuwasotesha rumande watu bila hatia right,ingekuwa big dili basi serikali mara baada ya kuwatia hatiani wachina hao ingewasiliana ana kwa ana na international maritime organization,na swala lingepatiwa ufumbuzi bila upendeleo.ahsante…

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles