32.2 C
Dar es Salaam
Sunday, November 24, 2024

Contact us: [email protected]

CAF yaitosa Yanga

kikosi-cha-yangaNA ADAM MKWEPU, DA ES SALAAM

SHIRIKISHO la Soka Afrika (CAF) limekataa ombi la klabu ya soka ya Yanga kutaka mabadiliko ya tarehe na muda katika mchezo wa Kombe la Shrikisho wa Kundi A dhidi ya TP Mazembe, unaotarajiwa kuchezwa Juni 28 mwaka huu.

Kutokana na uamuzi huo tarehe ya mchezo huo itabaki pale pale ambayo ni Juni 28 saa 4:00 jioni badala ya Juni 29  saa 7:15 usiku ambayo Yanga iliiomba CAF.

Yanga ambayo ipo kambini mjini Antalya, Uturuki katika Hoteli ya Rui  ilikuwa ikihaha kubadili  tarehe ya mchezo huo pia ikiwataka mashabiki wake kuamua muda gani  mchezo huo uchezwe ili kuwazidi kete wapinzani wao TP Mazembe.

Kwa mujibu wa taarifa ya CAF iliyotumwa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), sababu kubwa iliyochangia ombi hilo kukataliwa ni Mwenyekiti wa Mashindano wa Yanga, Isaac Chanji, kukubali muda na tarehe iliyopangwa na CAF ambayo ni Juni 28 mwaka huu kabla Yanga kuomba kufanya mabadiliko hayo.

“Hakuna kitakachobadilika  katika mchezo huo kwani kila kitu kitakuwa kama kilivyopangwa awali  kutokana na Meneja wa Mashindano wa Yanga  kuthibitisha muda na tarehe ya mchezo huo kabla ya kutuma maombi ya kutaka mabadiliko.

“Michuano hii ina mambo mengi kabla ya kupangwa muda na tarehe ya mchezo kunakuwa na makubaliano ambayo yanapaswa kutekelezwa kama yalivyopangwa, haiwezekani kufanya mabadiliko kienyeji,” ilisema taarifa hiyo.

Awali akizungumza na MTANZANIA jana, Katibu Mkuu wa TFF, Celestine Mwesigwa, alisema kwamba uamuzi wowote unaofanyika ndani ya CAF unazingatia  haki ya wadhamini  wa michuano  hiyo.

“Yanga iliandika barua ili kuomba mabadiliko katika mchezo huo na tulipowasiliana na  TP Mazembe walisema wapo  tayari kwa chochote.

“Kutokana na umuhimu wa wadhamini ndani ya michuano hiyo inaweza  ikachangia CAF kukubali au kukataa ombi hilo,” alisema Mwesigwa.

Kwa upande wake, Ofisa Habari  na Mawasiliano wa klabu hiyo, Jerry Muro,  alisema kwamba  sababu za kukataliwa ombi hilo zinatokana na jenereta  za Uwanja wa Taifa kutokuwa katika hali ya kufanya kazi.

“Hakutakuwa na mabadiliko yoyote ya mchezo huo, hivyo utachezwa  siku ya Jumanne Juni 28 mwaka huu,” alisema Muro.

Hata hivyo, taarifa kutoka viwanja vya hoteli ya Rui, Uturuki  ilipo kambi ya Yanga zinadai kwamba, wachezaji wa timu hiyo wanaendelea  vizuri na mazoezi huku  Oscar Joshua, akianza mazoezi mepesi baada ya kuwa na majeruhi ya paja aliyoyapata kwenye mchezo uliopita dhidi ya Mo Bejaia.

“Wachezaji wana hamasa ya  ushindi katika mchezo huo, licha ya  Nadir Harub ‘Cannavaro’ na Said Makapu kusumbuliwa na homa ya malaria,” ilisema taarifa hiyo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles