Evans Aveva ashangaa wanaobeza usajili Simba

Evans AvevaNA WINFRIDA NGONYANI, DAR ES SALAAM

UONGOZI wa klabu ya Simba umewashangaa baadhi ya watu wanaobeza usajili wa wachezaji uliofanywa na timu hiyo ukihoji kwanini wanatoa maoni kabla hata hawajakiona kikosi kikiwajibika.

Kauli hiyo imekuja siku chache baada ya taarifa kusambaa katika vyombo mbalimbali vya habari kuwa Simba imefunga rasmi zoezi zima la usajili, ambapo baadhi ya makundi ya watu wamekuwa wakiiponda timu kwa kufanya usajili wa kawaida.

Akizungumza na MTANZANIA jana, Rais wa Simba, Evans Aveva, alikanusha taarifa za kufungwa kwa zoezi la usajili na kuongeza kuwa bado uongozi wa timu hiyo unaendelea kufanya tathmini mbalimbali.

“Hatujafunga usajili kama taarifa zilivyozagaa, watu waache kusema mambo wasiyokuwa na uhakika nayo, sisi tunafanya tathmini katika mambo yetu yote wala hatukurupuki,” alisema.

Aidha, Aveva aliwataka wale wanaobeza usajili uliofanywa na uongozi huo kuacha kufanya hivyo kwa kile alichodai kuwa wanajua wanachokifanya na kuwasihi kuacha papara, badala yake wasubiri kuona kasi mpya ya Simba.

“Mimi nawashangaa sana yaani wala hawajaiona timu inafanya nini wameshaanza kutoa maoni, wasubiri waone nini tumekiandaa, kimya kingi kina mshindo mkuu,” alisisitiza Aveva.

Rais huyo aliwataka mashabiki wa timu hiyo kuendelea kuisapoti na kuahidi kuwa Simba imeweka mikakati kabambe itayoirudisha timu hiyo katika hadhi yake.

Hadi sasa Simba haijawatangaza rasmi wachezaji iliyowasajili na imekuwa ikifanya mambo yake kimya kimya, hali iliyotajwa kuwa ni mbinu mbadala za kutaka kuirejea kileleni mwa Ligi Kuu Tanzania Bara ambayo imeikosa kwa misimu minne mfululizo.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here