Baada ya vurugu hizo kuisha Jaji Warioba hakurejea na badala yake Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere, Joseph Butiku, alisimama na kuiita siku ya aibu kwa Watanzania.
Alisema tukio la vurugu ndani ya ukumbi wa mdahalo huo limeshuhudiwa na Watanzania nchi nzima.
“Baadhi ya wahuni waliofanya tukio hilo tunawatambua hivyo katika mikutano yetu ijayo hatutawaruhusu kushuhudia midahalo yetu,” alisema.
Butiku alisema kuwa tukio hilo halitakuwa mwisho wa kuendelea kwa midahalo ya taasisi hiyo iliyopangwa kufanyika Mwanza, Mbeya, Zanzibar na Tanga.
Jaji Warioba apata watetezi
Akizungumzia kadhia iliyotokea katika mkutano huo, mmoja wa waliohudhuria mdahalo huo, Halfan Said, alisema amesikitishwa na fujo zilizofanywa na vijana wa CCM waliofikia hatua ya kumpiga Jaji Warioba.
“Warioba kama raia mwingine wa kawaida anayo haki ya kutoa maoni yake na yanastahili kuheshimiwa na pia hakustahili kufanyiwa vurugu aliyofanyiwa na vijana hawa wa CCM ambao wameshindwa kuheshimu hata madaraka aliyowahi kuitumikia nchi hii na chama chake,” alisema.
Rudovick Mosha alisema kuonekana kwa kada wa CCM, Paul Makonda, kunaonyesha dhahiri chama hicho kilikuwa nyuma ya mpango huo mchafu wa kumfanyia vurugu Jaji Warioba katika mdahalo huo.
Katibu Mkuu wa Mtandao wa Wanafunzi Tanzania (TSNP-Tanzania), Alphonce Lusako, alisema amesikitishwa kwa tukio la vijana wa CCM kushindwa kusikiliza hoja na badala yake kufanya vurugu.
“Inatubidi vijana nchini tufikie mahali tukatae kutumika na kusema kuwa imetosha kutumika tuweze kusonga mbele kuepusha yaliyotokea,” alisema Lusako.
Naye Pius Mchulu alisema kumpinga Jaji Warioba ni kuukomaza na kuboresha ujinga na umasikini kwa wanyonge.
Aliyekuwa Mkurugenzi wa Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania (Tamwa), Ananilea Nkya, alitoa onyo kwa kundi lililofanya tukio hilo lenye nia ya kunyamazisha sauti za watu kuwa watakuwa wamejitafutia anguko.
“Suala la kusema na kusikilizwa ndiyo demokrasia na unapozuia mwisho hautakuwa mbali kwani Mungu anawaona na mwisho wa maovu yao unakaribia.
“Aliyeandaa tukio hilo la vurugu kwa Jaji Warioba atakutana na upanga wa Mungu na hata baki salama,” alisema Nkya.
Mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa (Chadema), alisema tukio hilo limedhihirisha kwamba dola inazama kwa kuwa mbinu wanazotumia kwa sasa ni dhaifu zilizowahi kutumiwa zamani na madikteta.
Katika vurugu hizo za kurushiana viti, mwandishi wa BBC, Arnold Kayanda alijikuta akipigwa kichwani na kiti.
Mabango, nyimbo zatawala
Baadhi ya mabango ya karatasi waliyosimama nayo vijana wa CCM yalikuwa na ujumbe uliosomeka: “Katiba inayopendekezwa tumepokea na tunaiunga mkono”, “Katiba hii tumeiona, tumeielewa na tunaikubali”. Mabango mengine yalikuwa na ujumbe wa matusi kwa Jaji Warioba.
Vijana hao ambao hata hivyo hawakuwa wengi katika ukumbi huo walianza kusikika wakiimba nyimbo za CCM kwa maneno ya ‘CCM nambari wani’.
Mmoja wa vijana hao alikataa kutaja jina lake lakini alisikika akisema kuwa, “tumechoka kudanganywa na Jaji Warioba.”
Wakati zilipozuka vurugu hizo na watu wakaanza kutoka nje, polisi walikuwa wakipiga risasi hewani nje ya ukumbi lakini hawakuingia ndani kuzuia vurugu hizo.
MUHESHIMIWA KIKWETE HAWA NDIO VIJANA WA CHAMA CHAKO? MBONA SASA CCM INAONESHA KUWA NI CHAMA CHA UPINZANI BADALA YA KUWA TAWALA AMBACHO KINATARAJIWA KUWA NA BUSARA NA HEKIMA? TUNASUBIRI HATUA ZAKO KWA WATOVU WA NIDHAMU HAWA WANODUMIZA DEMOKRASIA YA KWELI KUTOKA KWAKO WEWE RAIS NA MWENYEKITI WA CCM
hii ni aibu kubwa sana kwa chama tawala ambacho kinasifika kwa sera nzuri na za kistarabu. tulio ona tunashangaa kama kweli wapenda CCM tunaweza kufanya tukio la ajabu kiasi hicho. ni kweli mvunja chama ni mwanachama mwenyewe. huwezi kusema unapenda na kuthamin aman kama tunu na wakati huo huo unaleta vurugu na kufanya vitendo vya kihuni kama vile.
Polisi wa Tz ndio kazi yao waha daima huwa ni walinzi wa CCM na wapinzani wa CCM wakishakupigwa na wao ndio huja kuwaseidia CCM kufanya fujo.
Watanzania wote tulaani kitendo hiki cha aibu walochofanya CCM