BUJUMBULA, Burundi
SERIKALI ya hapa imetoa hati ya kimataifa ya kumkamata Rais wake wa zamani, Pierre Buyoya na maofisa wengine 16, kuhusiana na mauaji ya Rais wa kwanza wa nchi hii, Melchior Ndadaye aliyechaguliwa kwa njia ya kidemokrasia.
Mwendesha Mashtaka Mkuu, Sylvestre Nyandwi alisema juzi kwamba uchunguzi umebaini kuwa watu hao walihusika katika kupanga na kutekeleza mauaji ya Ndadaye ambaye pia alikuwa kiongozi wa kwanza kutoka jamii ya Wahutu.
Mauaji hayo yalifuatiwa na machafuko makubwa ya ukabila ambako zaidi ya watu 300,000 waliuawa.
Buyoya kwa wakati huu ni mwakilishi wa Umoja wa Afrika nchini Mal na ni mtu anayeheshimiwa Afrika na katika jumuiya ya kimataifa.
Buyoya, Mtutsi aliyeingia madarakani kupitia mapinduzi ya jeshi mwaka 1987, alikubali kushindwa na Rais Ndadaye katika uchaguzi wa mwaka 1993.
Hata hivyo Rais Ndadaye alikaa madarakani kwa miezi minne tu kabla ya akuuawa na kundi la wanajeshi Watutsi wenye misimamo mikali katika jaribio la mapinduzi lililoitumbukiza nchi katika mzozo ambao athari zake zinaendelea hadi leo.
Katika hati hiyo, serikali inazitaka nchi wanakoishi watuhumiwa hao kuwakamata na kuwarejesha nchini hapa ikisema ni muhimu watu hao kuhojiwa kuhusu mchango wao katika mauaji ya Rais Ndadaye.
Miongoni mwa watuhumiwa 16 pamoja na Buyoya, 11 walikuwa maofisa wa jeshi na watano waliobakia walikuwa raia wenye uhusiano ya karibu na rais huyo wa zamani.
Serikali ya sasa inaongozwa na Chama Cha Cndd-FDD cha Rais Pierre Nkurunziza, ambacho ni tawi la kundi la zamani la waasi Wahutu.