27.1 C
Dar es Salaam
Thursday, January 2, 2025

Contact us: info@mtanzania.co.tz

Buriani George H.W. Bush (1924-2018)


 Othman Miraji, Ujerumani                      

George Herbert Walker Bush, aliyefariki dunia siku kadhaa zilizopita huko nyumbani kwake katika Mkoa wa Texas, Marekani, alikuwa na umri wa miaka 94, akiwa Rais wa mwisho wa Marekani aliyekuwa mwanajeshi katika Vita vya Pili vya Dunia. Alishikilia urais kutoka 1989 hadi 1993, katika kipindi ulipoanguka Ukuta wa Berlin uliokuwa alama ya mgawanyiko wa dunia kinadharia baina ya kambi ya Mashariki ya Ukoministi na ya Magharibi ya Ubepari. Ni wakati pia ambapo dola kuu la Soviet Union  (Urussi ya zamani) lilisambaratika.

George Bush alijulikana sana kwa ucheshi wake, masihara na mizaha, tabia ambayo ilimpatia heshima hata kwa marais waliomfuata kuishi katika Ikulu mjini Washington. Wamarekani wengi, hata hivyo, hivi sasa hawaukumbuki udhaifu aliokuwa nao mwanasiasa huyo. Ikiwa ni robo karne sasa tangu alipoacha urais, si watu wengi wanayakumbuka mambo yaliyojiri wakati Bush akiwa mtu muhimu nambari moja duniani. Hasa kwa vile jina lake limegubikwa na lile la mwanawe, George Bush (Mtoto) na ambaye pia baadaye akawa Rais wa Marekani.

Ni kutokana na kazi yake kubwa aliyoifanya ndio maana kipindi cha wasiwasi mkubwa na zahama za kisiasa duniani- mwisho wa miaka ya 80  ambapo dola kuu la Soviet Union (Urusi ya zamani) lilisambaratika na kambi ya kijeshi ya Mashariki (Warsaw) mwishowe ilikoma- kilipita salama. Bush, aliyekuwa fundi wa diplomasia, alifaulu kutumia lugha ya kupapasapapasa iliyowalainisha viongozi wa Moscow wayakubali mambo kadhaa, muhimu kabisa kati ya hayo ni kuunganishwa tena dola mbili za Kijerumani (ya Mashariki na ya Magharibi). Jambo hilo lilisababisha  kuanguka kile kilichoitwa Pazia la Chuma lililoigawa Ulaya.

Wakati huo Bush alikuwa ni mtu mwenye uzoefu mkubwa katika Ikulu ya Washington, kwa hivyo alifaulu kuziondoa hofu za Waziri Mkuu wa Uingereza, Margareth Thatcher na Rais wa Ufaransa, Francois Mitterand, pia za Wapolandi ambao wakati huo walikuwa na wasiwasi kwamba Ujerumani iliyoungana ingeweza kuwa kitisho kwa majirani zake.  Bush aliwaamini Kansela Helmut Kohl wa Ujerumani na Rais Michail Gorbaschov wa Urussi. Kwa vyovyote vile, yeye alikwishatambua wakati huo kwamba kiuchumi na kisiasa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Ujerumani (Ujerumani Mashariki) isingeweza kusimama yenyewe kwa miguu yake.

Rais Frank-Walter Steinmeier wa Ujerumani amemsifu Bush kama rafiki wa kweli wa Ujerumani. Bush amedhihirisha wazi namna anavyoyang’ang’ania maamuzi yeyote anayochukua. Hata katika hali ya wasiwasi unapozuka mzozo wa kisiasa, alikuwa tayari kuchukua hatua ya kijeshi kuutanzua mzozo huo. Mfano ni mwaka 1990 pale Rais Saadam Hussein wa Iraq alipotuma majeshi ya nchi yake kuivamia nchi jirani ya Kuwait. Papo hapo Marekani iliunda ushirika wa kijeshi wa mataifa 34 ulioweza kuyatoa majeshi ya Saadam Hussein kutoka Kuwait mwaka 1991.  Hatua hiyo ya kijeshi iliungwa mkono na Azimio la Umoja wa Mataifa.

Bush alihofia kwamba pindi Kuwait ingeangukia mikononi mwa Saadam Hussein, basi Saudi Arabia (mshirika mkubwa wa Marekani) ingefuata. Zaidi ya hayo, visima vikubwa vya mafuta vya Kuwait vilikuwa vinaweza kufikiwa kwa urahisi na wanajeshi wa Iraq. Bush alituma wanajeshi wa Kimarekani nusu milioni kuikomboa Kuwait na kuyafurusha majeshi ya Iraq kutoka nchi hiyo.

Itakumbukwa pia kwamba Bush aliendesha vita vilivyomuondosha kutoka madarakani mtawala wa kijeshi wa Panama, Manuel Noriega.

Lakini yeye hajawa na mafanikio katika siasa zake za ndani kama vile ilivyokuwa katika siasa za nje. Alirithi nakisi kubwa ya Bajeti ya Serikali kutoka kwa mtangulizi wake, Ronald Reagan. Iimbidi awazidishie kodi wananchi, jambo ambalo alipinga kulifanya wakati alipokuwa anaendesha kampeni za kutaka kuchaguliwa kuwa rais. Kutokana na kwenda kinyume na ahadi aliyoitoa na pia kudodora uchumi, miaka minne baadaye Bush alishindwa kuchaguliwa tena. Kwa muda wa miaka minane kabla alikuwa Makamo wa Rais chini ya Ronald Reagan. Linapokuja suala la ufasaha wa lugha, Bush alishindwa na Reagan, tukitambua kwamba Reagan, kabla ya kuwa Rais, alikuwa mwigizaji wa sinema.

George Bush alikuwa tayari ana heshima na umaarufu hapo kabla alipokuwa kijana. Alijiandikisha jeshini akiwa na umri wa miaka 19, rubani wa kijeshi kijana kabisa. Ilikuwa ni baada ya Wajapani kuzishambulia manuwari za Kimarekani katika Bandari ya Pearl.

Bush amepata mapigo kadhaa katika maisha yake ya kisiasa. Mara mbili alishindwa kukinyakua kiti cha Mkoa wa Texas katika Senate huko Washington. Pia katika uchaguzi wa mchujo kuwania nafasi ya mgombea wa urais kwa tiketi ya chama cha Republican alibwagwa chini na Ronald Reagan. Lakini chama  cha Republican baadaye kiliona  bora kimteue Bush kama mgombea wa Makamo wa Rais baada ya kuweko ule mshtuko wa kashfa ya Watergate ili kupunguza aibu iliyopata chama hicho.

Mwaka 1973 Bush akawa kiongozi wa chama cha Republican. Na licha ya ujanja mchafu uliotumika katika kampeni za utawala wa Nixon, George Bush alibakia kuwa mwaminifu kwa Rais huyo. Mwishowe Agosti 1974 ilimbidi ambane na kumlazimisha rafiki yake Nixon ajiuzulu, kwa ajili ya maslahi ya chama na nchi. Bush baadaye akashika nyadhifa ya Balozi mjini Peking, China na pia aliwahi kuliongoza Shirika la Upelelezi la Marekani (CIA).

Si tu siasa na utumishi serikalini, Bush alikuwa pia mfanyabiashara aliyefaulu. Msingi wa utajiri wake ulitokana na kuanzisha kampuni ya mafuta ambayo aliiuza miaka kumi baadaye. Punde baadaye alijichovya katika siasa kama alivyofanya baba yake, Prescott, hapo kabla. Akina Bush ni familia ya wafanyabiashara kutokea Mkoa wa Connecticut. Baba Prescott alianzia kufanya kazi benki. Mwenyewe George alisoma katika Chuo Kikuu cha Yale

Mwaka 2015 George Bush alisema kwamba anadhani kwamba mwanawe, George Bush Mtoto, alifanya makosa kuwaachia Dick Cheney (Waziri wa Mambo ya Kigeni) na Donald Rumsfeld (Waziri wa Ulinzi) kufanya walivyotaka. Mawaziri hao wote wawili walikuwamo katika Serikali ya George Bush Baba, lakini baadaye wakati wa George Bush Mtoto walijibadilisha kuwa wenye siasa kichwa ngumu.

April mwaka huu, mke wa George Bush, Barbara, aliaga dunia baada ya kuwa pamoja kwa zaidi ya miaka 70. Rais Trump hajakuweko mazikoni, lakini walioketi katika viti vya mbele kabisa mazikoni walikuwa mke wa Trump, Melanie, Hilary na Bill Clinton na pia Barack na Michelle Obama. Hiyo ilikuwa picha ya kuvutia. Lakini mara hii Rais Trump atakuweko katika mazishi ya Bush. Trump amenukuliwa akisema:

Bush alikuwa na maisha makubwa yaliyochanganya sifa kubwa mbili za Taifa la Marekani: kufanya biashara na kutumika serikalini.

Mwisho….

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
593,000SubscribersSubscribe

Latest Articles