NA CLARA MATIMO
KATIKA kuadhimisha Siku ya Moyo Duniani, Hospitali ya Rufaa ya Kanda Bugando (BMC), imegharamia zaidi ya Sh milioni 27 kwa huduma ya vipimo vya ugonjwa wa moyo bure kwa wananchi waliojitokeza kufanyiwa uchunguzi.
Mkurugenzi wa BMC, Dk. Abel Makubi, alikuwa akizungumza katika kilele cha maadhimisho ya Siku ya Moyo Duniani yaliyofanyika hospitalini hapo juzi.
Mwaka huu maadhimisho hayo yalibeba kaulimbiu ya ‘upende na uuwezeshe moyo wako’.
Katika kuadhimisha siku hiyo, Hospitali ya Bugando ilitoa huduma za uchunguzi na upimaji wa magonjwa ya moyo bure kwa wananchi waliojitokeza tangu Septemba 27 hadi 29.
“Kawaida mgonjwa akija moja kwa moja hapa Bugando kutoka nyumbani bila kuwa na barua ya rufaa kutoka hospitali za rufaa za mikoa inabidi atoe Sh 20,000 kwa ajili ya kumuona daktari.
“Hivyo kwa siku tatu tulizotoa huduma ya upimaji bure tumeweza kuwaona watu wazima 687 na watoto 167.
“Wote ni 854, hivyo kama wangekuja kuonana na madaktari bingwa wangelipa zaidi ya Sh milioni 17.
“Baada ya kufanyiwa uchunguzi kati ya hao watu wazima 70 na watoto 35 walihitaji vipimo zaidi na walipimwa kipimo kinachogharimu Sh 100,000 kwa hiyo ingekuwa ni kulipa wangelipa Sh milioni 10.5,”alifafanua Dk. Makubi.
Mkuu wa Idara ya Upasuaji wa Moyo na Vifua wa Hospitali ya Bugando, Profesa William Mahalu, alisema changamoto kubwa inayowakabili ni vitendea kazi, uhaba wa wataalamu na mabingwa wa fani ya ugonjwa huo.
Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongela, Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana, Mery Tesha, alisema Serikali itaendelea kuboresha upatikanaji wa huduma za matibabu bingwa katika hospitali hiyo.
Aliwataka wananchi kujenga utamaduni wa kupima afya zao mara kwa mara kuliko kusubiri ugonjwa wao ufike hatua za juu