32.2 C
Dar es Salaam
Thursday, November 21, 2024

Contact us: [email protected]

BoT yawaonya Watanzania biashara ya noti chakavu

Na Esther Mnyika, Mtanzania Digital

Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imewaonya Watanzania dhidi ya kununua na kuuza noti chakavu mitaani, ikieleza kuwa ni kosa kisheria na kwamba biashara hiyo ni ya kitapeli.

Kauli hiyo imetolewa jijini Dar es Salaam leo, Oktoba 31, 2024, na Kaimu Mkurugenzi wa Usimamizi wa Sarafu BoT, Ilulu Ilulu, alipokuwa akitoa taarifa kuhusu mpango wa kuondoa noti za zamani kutoka kwenye mzunguko wa sarafu nchini.

Ilulu amesema wananchi wanapaswa kubadilisha noti chakavu kupitia madirisha maalum ya benki za biashara nchini, ambapo BoT imehakikisha huduma hiyo inapatikana.

“Suala la kununua na kuuza sarafu mitaani halipo kisheria; ni utapeli kwa sababu kinachofanyika ni kumtapeli mwenzako kutokana na ukosefu wa taarifa sahihi. BoT imetoa fursa kwa benki zote za biashara nchini kuwa na madirisha maalumu ya kubadilisha noti chakavu,” alisema Ilulu.

Aidha, amewataka wananchi kufuata utaratibu wa kwenda kubadilisha fedha hizo wenyewe kwenye madirisha hayo badala ya kushirikiana na watu wasiofuata sheria ambao lengo lao ni kupata faida kwa kununua noti chakavu kwa bei ndogo na kisha kuzibadilisha kwa faida kubwa.

Ilulu ameeleza kuwa BoT haitatumia mawakala katika zoezi hili; badala yake, benki za biashara zitakuwa pekee zinazotumika kwa kipindi cha miezi mitatu, hatua inayotarajiwa kumalizika kufikia Aprili 5, mwakani. Pia, amewakumbusha wananchi kupeleka noti zilizo halali na zenye alama za usalama ili kupata thamani halisi.

“Inapotokea kusitishwa kwa uhalali wa noti fulani, wananchi hupewa muda maalum wa kuzibadilisha kabla ya muda huo kwisha. Tunapenda kuutaarifu umma kuwa zoezi hili la kubadilisha noti za zamani litaanza rasmi Januari 6, 2025, na litakamilika Aprili 5, 2025,” alisema Ilulu.

Kwa mujibu wa BoT, baada ya tarehe hiyo, noti hizo zitakoma kuwa halali kwa malipo ndani na nje ya nchi. Zoezi la ubadilishwaji litaendeshwa katika ofisi za BoT na benki zote za biashara nchini, huku wananchi wakilipwa thamani sawa na kiasi walichowasilisha.

Noti zinazotarajiwa kuondolewa ni zile za toleo la mwaka 1985 hadi 2003, pamoja na noti ya shilingi mia tano ya toleo la mwaka 2010.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles