Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
TISHIO la utakatishaji fedha na ufadhili wa vitendo vya kigaidi kupitia miamala ya simu za mikononi, sasa limedhibitiwa.
Taarifa hiyo ni kwa mujibu wa Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Profesa Benno Ndulu na Kamishina wa Kitengo cha Inteljensia ya Kifedha (FIU) katika Wizara ya Fedha, Onesmo Makombe.
Akizungumza hivi karibuni wakati wa uzinduzi wa Ripoti ya Maendeleo ya Dunia ya Benki ya Dunia 2016, Profesa Ndulu, alisema usajili wa watumiaji wote wa simu za mikononi umesaidia kupunguza uwezekano wa hatari hiyo.
Huduma za kibenki za simu za mikononi kama vile M-pesa, TigoPesa na AirtelMoney, ambazo zimezidi kupanuka kwa haraka nchini huhudumia idadi kubwa ya watu wakifikia huduma za kawaida za kibenki hasa maeneo ya vijijini.
Hata hivyo ongezeko hilo limesababisha wasiwasi wa vitendo vya utakatishaji wa kifedha na ufadhili wa vitendo vya kigaidi na hivyo kuiathiri sekta ya kifedha, kwa mujibu wa wachambuzi wa taifa wa usalama.
Ikiwa chini ya usimamizi wa idara katika BoT, ukomo wa mwanzo wa kuruhusu miamala ya fedha katika simu za mikononi kwa watu na kampuni ulikuwa kuhamisha hadi Sh 1,000,000 kwa siku.
Lakini kibali maalumu kinaweza kutolewa kwa mashirika kuhamisha viwango vikubwa vya fedha.
Taasisi za kidini zinazotafuta kibali huhesabiwa kama sehemu ya mashirika pale inapoonekana yamezoea kushughulika na mabilioni ya shilingi kwa mwezi, vinginevyo hayaruhusisi kufanya miamala ya viwango vikubwa kupitia simu za mikononi, maofisa walisema.
FIU ilipokea ripoti za miamala yenye shaka 68 mwaka 2013, likiwa ongezeko kutoka mwaka 2012, kwa mujibu wa nyaraka za idara ya kupambana na ugaidi ya Marekani.
Nyaraka hizo za Marekani zilikuwa zikikariri ripoti za kiintelejensia kutoka Tanzania na zilisema BoT ilikadiria mwaka 2013 kuwa miamala yenye thamani ya dola milioni 650 ilifanyika kila mwezi kupitia huduma za simu za mikononi kipindi hicho.
Ripoti ya nchi ya mwaka 2014 inasema Tanzania ilikuwa mwanachama wa kundi la vitengo vya FIU (Egmont Group), ambapo kitengo hicho kilipokea ripoti 65 za miamala yenye shaka inayohusiana na utakasishaji fedha mwaka 2014, likiwa ni punguzo dogo kutoka kesi 68 mwaka 2013.
Wawasilisha mada wakati wa uzinduzi wa Ripoti ya Maendeleo ya Dunia mwaka 2016, ilisema biashara ya miamala ya fedha imeendelea kukua nchini Tanzania na kuipiku Kenya kama mtumiaji namba moja duniani wa miamala ya fedha kupitia simu za mikononi.
Prof. Ndulu alisema imekuwa sera ya Tanzania inayohamasisha matumizi ya teknolojia mpya, lakini ilipitiwa baadaye na kurekebishwa ili kushughulikia shaka ya uwezekano wa kutumika kihalifu.
“Ilibidi kusajili watumiaji wa simu za mikononi kwa kutumia vitambulisho vyenye picha ili kuwezesha kuwatambua, vitambulisho vimesaidia kupunguza hatari,” alisisisitiza.
Awali Kamishina wa FIU, Onesmo Makombe aliliambia gazeti hili kuwa wasiwasi na hatari zilizoonekana kati ya mwaka 2012 na 2013 zimepunguzwa kwa kuwatambua watumiaji pamoja na uwapo wa kifaa maalumu kinachoratibiwa na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA).
Makombe alisema kupitia kifaa cha TCRA, serikali kwa sasa inaweza kufuatilia kila senti inayohamishwa kupitia mitandao ya simu za mikononi ili shaka yoyote iweze kuonekana na wahusika kutambulika.
Huduma za miamala ya fedha kupitia simu za mikononi imeongezeka, lakini hatari ya utakasishaji kifedha au kufadhli ugaidi imepunguzwa sana, alisema.
Takwimu za BoT zinaonesha idadi ya watumiaji wa simu za mikononi ni 29,126,517, ikiwa imepanda kutoka watumiaji 26,871,176 mwaka 2012. Idadi ya mawakala pia imepanda kutoka 97,613 mwaka 2012 hadi 119,719 kwa sasa.