30 C
Dar es Salaam
Monday, November 18, 2024

Contact us: [email protected]

Bonnah aridhishwa na miradi inayotekelezwa jimboni kwake

Na Nora Damian, Mtanzania Digital

Mbunge wa Jimbo la Segerea, Bonnah Kamoli amekagua ujenzi wa miradi mbalimbali ya maendeleo na kusema ameridhishwa na kazi iliyofanyika hadi sasa.

Februari 28,2024 Bonnah amefanya ziara kukagua mradi wa ujenzi wa jengo la utawala katika Shule ya Msingi Kifuru Mpya, Daraja la Majoka na Barabara ya Kichangani inayotarajiwa kujengwa katika awamu ya pili ya mradi wa DMDP (Kata ya Kinyerezi).

Pia amekagua ujenzi wa soko la mama na baba lishe, ukarabari wa ofisi ya walimu katika Shule ya Msingi Vingunguti (Kata ya Vingunguti) na Barabara ya Faru inayotarajiwa kujengwa kwa lami kupitia mradi wa DMDP (Kata ya Mnyamani).

Meya wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, Omary Kumbilamoto, akimweleza Mbunge wa Jimbo la Segerea, Bonnah Kamoli (kulia), kuhusu ujenzi wa soko la mama na baba lishe Vingunguti wakati wa ziara ya mbunge huyo kukagua miradi ya maendeleo.

Meneja wa Tarura Wilaya ya Ilala, John Magori, amesema ujenzi wa Daraja la Majoka umefikia asilimia 80 na kuahidi kuwa baada ya wiki mbili litakuwa limekamilika.

Katika Shule ya Msingi Kifuru Mpya, Mwalimu Mkuu, Adeltus Kazinduki, amesema jengo la utawala limekamilika na kuomba wapatiwe samani na vifaa ili waanze kulitumia.

Katika Shule ya Msingi Vingunguti, Mwalimu Mkuu, Mfaume amesema tayari wamepokea Sh milioni 23 kutoka katika Mfuko wa Jimbo kukarabati ofisi ya walimu na kumshukuru mbunge huyo kwani ofisi hiyo ilikuwa chakavu kwa muda mrefu.

Mbunge wa Jimbo la Segerea, Bonnah Kamoli, akizungumza na wananchi wa Mtaa wa Kichangani Kata ya Kinyerezi wakati wa ziara ya kukagua miradi ya maendeleo.

Meya wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam ambaye aliambatana na mbunge huyo, amesema wamepokea Sh bilioni 240 na kila kata miradi ya maendeleo inafanyika.

Amesema mradi wa ujenzi wa soko la mama na baba lishe ambao unagharimu Sh milioni 354 wameongeza maduka 36 na baada ya wiki tatu utakuwa umekamilika.

“Baadhi ya changamoto ndogondogo ziko ndani ya uwezo wetu tutazitatua, changamoto ya pampu ya maji Mtaa wa Kichangani wiki ijayo nitawapa Sh 650,000 warekebishe,” amesema Kumbilamoto.

Diwani wa Kata ya Kinyerezi, Leah Mgitu, amesema Daraja la Majoka limeleta matumaini makubwa kwa wananchi wa Mitaa ya Kibaga na Kifuru ambao walikuwa wakishindwa kuvuka hasa wakati wa mvua na kumshukuru mbunge huyo kwa jitihada zake.

Kwa upande wake Bonnah amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuelekeza fedha nyingi katika jimbo hilo ambazo zimewezesha kutekelezwa miradi ya miundombinu ya barabara, madaraja, elimu na afya.

“Tunamshukuru sana mheshimiwa rais, baadhi ya miradi kama Daraja la Majoka limejengwa kwa dharura na dharura ziko Tanzania nzima lakini na sisi hatujasahaulika. Kilio kikubwa ni ujenzi wa barabara na nyingi tayari zimepitishwa katika mradi wa DMDP 2 nawaomba wananchi wawe wavumilivu kazi inafanyika,” amesema Bonnah.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles