30.6 C
Dar es Salaam
Saturday, November 23, 2024

Contact us: [email protected]

Bongo Star Search msimu wa 15 yazinduliwa, kusaka vipaji Kimataifa

Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital

Shindano maarufu la kusaka vipaji nchini Tanzania, Bongo Star Search (BSS), limezindua msimu wake wa kumi na tano kwa mabadiliko makubwa, ambapo kwa mara ya kwanza, shindano hilo litaenda kimataifa kwa kuhusisha nchi za Kenya, Uganda, Burundi na Congo.

Akizungumza jana Alhamisi Oktoba 24,202’ wakati wa uzinduzi huo, Mkurugenzi Mkuu wa Benchmark 360 Limited, Rita Paulsen, alisema kuwa msimu huu unatarajiwa kuwa wa kipekee na kihistoria, akisisitiza kuwa hatua ya BSS kuvuka mipaka ni ishara ya ukuaji na uwekezaji mkubwa katika kuendeleza vipaji vya Afrika Mashariki na Kati.

“Kwanza kabisa, napenda kuchukua fursa hii kumshukuru Mungu na kuwashukuru wote mliojitokeza kwa wingi kushuhudia tukio hili kubwa, uzinduzi wa msimu mpya wa Bongo Star Search Afrika,” alisema Paulsen.

“Kwa miaka mingi, tumeweza kuibua vipaji kutoka Tanzania pekee, lakini msimu huu tunaingia hatua ya juu kabisa. Kwa mara ya kwanza, tunavuka mipaka ya nchi, tukifanya usahiri katika nchi zaidi ya tano, zikiwemo Tanzania, Kenya, Uganda, Burundi, na Congo,” amesema.

Paulsen alifafanua kuwa lengo kuu la msimu huu ni kuwapa vijana wengi zaidi fursa ya kuonesha vipaji vyao na kufikia ndoto zao.

“Muziki ni lugha ya ulimwengu, na tunataka kuwapa wasanii chipukizi kutoka sehemu mbalimbali nafasi ya kuungana na kuonesha uwezo wao kwenye jukwaa hili kubwa. Msimu huu, kama mlivyosikia, utakua ni mkubwa zaidi kuwahi kutokea,” amesema Paulsen.

Kwa mujibu wa Paulsen, msimu huu utakuwa na mabadiliko makubwa, ikiwemo kuleta majaji wa kimataifa na waelimishaji wenye uzoefu mkubwa katika sekta ya muziki.

“Tumeweka mipango madhubuti kuhakikisha kuwa sio tu tunaboresha uzoefu wa mashindano, lakini pia tunapandisha kiwango cha ubora katika kila hatua. Tutakuwa na majaji wa kimataifa, waelimishaji wenye uzoefu, na wasanii waliobobea watakaoshirikiana na washiriki wetu ili kuhakikisha kuwa wanapata elimu ya juu na mwongozo sahihi wa kimasoko na kisanii,” aliongeza.

Kwa upande wake, Meneja Masoko wa Sartimes, David Malisa, alisema kuwa msimu huu wa kumi na tano wa BSS unasherehekea mafanikio ya miaka 15 tangu kuanzishwa kwake na kwamba hatua ya kuvuka mipaka ni hatua kubwa ya kuwapongeza waandaaji wa shindano hilo.

“Bongo Star Search itaanza kuonyeshwa Desemba 1 kupitia chaneli ya ST Bongo kwa hapa Tanzania, Uganda kupitia Star Times Makula TV, na Nairobi kupitia ST Swahili, chaneli namba 160 na 400,” alisema Malisa.

Mashindano ya Bongo Star Search kwa msimu huu yanatarajiwa kuvutia washiriki wengi zaidi na kuwa jukwaa bora kwa wasanii chipukizi kutoka nchi mbalimbali za Afrika Mashariki na Kati kuonesha uwezo wao na kujenga majina yao katika tasnia ya muziki.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles