NAIROBI, KENYA
JESHI LA Polisi limewatahadharisha Wakenya kuwa waangalifu na kuripoti mtu au kitu chochote kinachotia shaka baada ya bomu kulipuka na kujeruhi watu wawili mjini hapa juzi usiku.
Katika taarifa yake kwenye mtandao wa Twitter, jeshi hilo limewaomba raia kusaidia vikosi vya usalama kukabiliana na tishio lolote kwa kutoa habari muhimu.
Vilevile imewataka Wakenya kuendelea na shughuli zao za kawaida ikisema waathirika wawili wa mlipuko huo walipata majeraha madogo na walitibiwa na kuruhusiwa kurudi nyumbani.
Wamesema polisi imeanza uchunguzi kupitia picha za kamera za usalama, CCTV ili kumnasa mmiliki wa bomu aliyedaiwa kutoroka.
Jumamosi usiku, mlipuko wa bomu ulitokea katikati ya jiji la Nairobi na kuwajeruhi watu wawili, kwa mujibu wa maafisa wa polisi .
Walioshuhudia wanasema mlio mkubwa ulisikika katika eneo la Odeon, moja ya viunga vyenye shughuli nyingi na mikusanyiko ya watu wengi katikati ya jiji la Nairobi.
Bomu hilo lilikuwa limefichwa ndani ya begi na kusukumwa kwa mkokoteni.
Mkuu wa polisi wa jiji la Nairobi Philip Ndolo aliwaambia wanahabari kuwa, mtu mmoja mwenye asili ya Kisomali alikodi mkokoteni na kupakia begi lake, na walipofika eneo la tukio, kwenye makutano ya barabara za Tom Mboya na Latema alitoweka.
“Alimhadaa mwenye mkokoteni kwa kumwambia amsubiri akafuate kitambulisho chake, ambacho alikisahau, hakurudi na baada ya muda mfupi bomu lililokuwamo ndani ya begi hilo lililipuka,” alisema Ndolo.
Mlipuko huo uliozua taharuki kubwa eneo hilo lenye stendi nyingi za mabasi uliwajeruhi mwendesha mkokoteni na mfanyabiashara ndogondogo aliyekuwepo karibu na mkokoteni huo.
Shambulio hilo linakuja siku chache toka Hoteli ya kifahari ya DusitD2 kushambuliwa na kupelekea vifo vya watu 21.
Tayari eneo hilo limefungwa na polisi na vikosi vya kutegua mabomu vimeshawasili eneo la tukio.