Na MAREGESI PAUL – DODOMA
BOMOABOMOA inayoendelea nchini kwa wananchi waliojenga katika maeneo ya Shirika la Reli Tanzania (TRC), imewakera baadhi ya wabunge.
Wabunge hao walionyesha hali hiyo bungeni jana wakati walipokuwa wakichangia Muswada wa Sheria ya Reli ya Mwaka 2017, uliowasilishwa bungeni na Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa.
Katika mchango wake, Mbunge wa Kaliua, Magdallena Sakaya (CUF), alionyesha kutoridhishwa na bomoabomoa hiyo kwa kuwa baadhi ya wanaovunjiwa majengo, walianza kuyamiliki miaka mingi iliyopita.
Kwa upande wake, Mbunge wa Moshi Mjini, Jafary Michael (Chadema), pamoja na kulalamikia bomoabomoa hiyo, alitaka viongozi waliosababisha wananchi wakajenga katika maeneo ya reli, kuchukuliwa hatua.
“Hii bomoabomoa inaumiza wananchi na kwa kuwa inaonekana baadhi ya waliojenga katika maeneo hayo walikuwa na vibali vya Serikali, basi waliotoa vibali hivyo wachukuliwe hatua kwani wamesababisha wananchi wapate hasara bila sababu,” alisema Michael.
Mbunge wa Tabora Mjini, Emmanuel Mwakasaka (CCM), alisema kuna haja kwa Serikali kuangalia namna ya kuwafidia waliovunjiwa nyumba zao kwa kuwa baadhi waliuziwa viwanja na Serikali.
Mbunge wa Nzega Mjini, Hussein Bashe (CCM), alilalamikia bomoabomoa hiyo na kusema mkoani Tabora kaya zaidi ya 500 zitavunjiwa nyumba, akiwamo kikongwe mwenye miaka zaidi ya 70 ambaye alianza kumiliki eneo lake miaka mingi iliyopita.
Mbunge wa Tunduma, Frank Mwakajoka (Chadema), alisema nyumba zaidi ya 3,244 zitabomolewa na kwamba kuna haja watakaobomolewa, kulipwa fidia ili wakajenge makazi mapya.
Mbunge wa Viti Maalumu, Anna Lupembe (CCM), alitaka Serikali iimarishe ulinzi wa reli ili kudhibiti majangiri wanaong’oa mataluma kwa lengo la kupora mali za abiria.