26 C
Dar es Salaam
Monday, March 4, 2024

Contact us: [email protected]

NDUGAI ATISHIA KUMFUNGA MDOMO ZITTO

Na MAREGESI PAUL

-DODOMA

SPIKA wa Bunge, Job Ndugai, amemuonya Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe (ACT-Wazalendo) na kumwambia kuwa anaweza kumzuia asiongee chochote bungeni hadi atakapomaliza ubunge wake.

Ndugai alitoa onyo hilo bungeni jana alipokuwa akimzungumzia mbunge huyo aliyesema anatoa kauli za kulidhalilisha Bunge licha ya juzi kuagiza ahojiwe na Kamati ya Bunge ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge kwa kosa hilo.

“Waheshimiwa wabunge, jana nilieleza pamoja na mambo mengine, mheshimiwa Zitto Kabwe ajieleze kwenye Kamati ya Maadili kwa sababu ya mambo yanayohusisha kudhalilisha Bunge.

“Kwa kiburi kikubwa, Zitto ameendelea tena kudhalilisha mhimili wa Bunge na kwa maneno mengi ambayo mengine yote ni ya kupuuza masikioni mwa Watanzania, kwani ni mtu anayejaribu kugawa Bunge kwa kujaribu kulinganisha uongozi wa sasa wa Bunge na uongozi wa Bunge la kumi la mheshimiwa Makinda na uongozi wa Bunge la tisa la marehemu Mzee Sitta.

“Nimwambie yeye na wengine wote wanaojaribu kufanya ulinganisho usiokuwa na maana, kila Bunge la miaka mitano huwa ni tofauti na Bunge jingine.

“Lakini nimwambie mheshimiwa Zitto, kwamba Sitta na Makinda ni walimu wangu na hata siku moja sikio haliwezi kuzidi kichwa na hawa ni watu nawaheshimu sana, wamenilea na ni sehemu ya walionifikisha hapa nilipo.

“Kwa hiyo, mimi ni kichuguu tu, sasa utalinganishaje na mlima mkubwa kama Kilimanjaro?

“Lakini, nimkumbushe tu kwamba katika Bunge la tisa, mheshimiwa Zitto alileta hoja fulani hapa bungeni na wengine hamkuwepo ila sisi tulikuwapo. Alileta hoja ya maana tu ikihusu Buzwagi, lakini hoja yake ikakataliwa hapa hapa na kwa kuwa alikuwa amekosa maadili fulani fulani, alihukumiwa hapa hapa kwa kupigwa nje miezi mitatu.

“Katika hili, mimi ni angalau namuanzia kule kwenye maadili ajieleze angalau asikike, au anataka niende mkuku mkuku kama wakati ule wa Bunge la tisa ili aone Ndugai anafanana na mzee Sitta?

“Namshangaa Zitto anapotaka kupambana na Spika, Zitto naweza kukupiga marufuku kuongea humu mpaka miaka yako yote ikaisha na hakuna pa kwenda, hakuna cha swali, hakuna cha nyongeza, hakuna cha kuongea chochote ndani ya Bunge utanifanya nini, pambana na kitu kingine sio Ndugai.

“Kwa haya ya Ndugai sina tatizo nayo ila ya kudhalilisha Bunge ambayo anaendelea kuyafanya, hayo siwezi kuyaacha kwa sababu ni wajibu wangu kulinda mhimili kwa nguvu zangu zote.

“Kwa hiyo, hili kosa la pili na lenyewe linakwenda kwenye Kamati ya Maadili, kwani ameudhalilisha mhimili wa Bunge kwa yale maandishi yake ya jana, tutaenda naye pamoja, tutakwenda sambamba mguu kwa mguu mpaka kitaeleweka,” alisema Ndugai.

Agizo hilo la Spika ni mwendelezo wa maagizo yake baada ya kuagiza juzi Zitto akahojiwe na kamati hiyo baada ya kukaririwa akisema Spika alikosea kutoruhusu taarifa za kamati alizounda kuhusu biashara ya madini ya tanzanite na almasi, zisijadiliwe bungeni.

Mbunge mwingine aliyetakiwa kuhojiwa na kamati hiyo kwa maagizo ya Spika, ni Saed Kubenea (Chadema) wa Ubungo, ambaye anatuhumiwa kusema Spika alilidanganya Bunge kwa kutaja idadi ndogo ya risasi zilizotumika kumshambulia Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu (Chadema), anayeendelea kutibiwa jijini Nairobi, Kenya.

Pia, Spika aliitaka Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Bunge, imhoji Kubenea kwa kuwa alipokuwa akizungumza kanisani juzi, alionyesha kuwa na taarifa za tukio la kushambuliwa kwa Lissu.

Hata hivyo, Zitto aliandika kupitia mtandao wa kijamii wa Twiter kwamba hatua ya kuitwa kwake ina lengo la kutaka kuwahamisha Watanzania kwenye mjadala wa kuhoji hali ya afya ya Lissu.

Pamoja na hali hiyo, alisema atakwenda kwenye kamati hiyo kama alivyotakiwa na Spika.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
584,000SubscribersSubscribe

Latest Articles