27.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, April 23, 2024

Contact us: [email protected]

POLISI WAZUIA MAOMBI KWA LISSU

Na Waandishi Wetu
KAMANDA wa Polisi Mkoa wa Rukwa, amekizuia
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) mkoani humo kufanya maombi maalumu kumwombea Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu, aliyelazwa katika Hospitali ya Nairobi nchini Kenya akitibiwa majeraha ya risasi.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Mwenyekiti wa chama hicho Mkoa wa Rukwa, Sadrick Malila, alisema wamezuiwa na Kamanda wa Polisi mkoani humo, George Kyando kwa kisingizio cha uvunjifu wa amani.
Alisema katika maombi hayo, waliwaalika viongozi wa dini wa makanisa ya Free Pentecostal Church (FPCT), Kanisa Katoliki, Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) na wachungaji mbalimbali.
“Baada ya kuzuiwa, tumewatangazia wanachama wa Chadema na wananchi wengine waliojiandaa kwa maombi hayo, kila mtu afanye maombi binafsi kwa sababu tunaamini Mungu ni mwema na atajibu maombi yao,” alisema Malila.
Kwa upande wake, Kamanda Kyando alikiri kuzuia mkusanyiko huo wa maombi kwa madai kuwa mwenyekiti huyo wa Chadema alizungumza naye, lakini hakuomba kibali cha mkusanyiko.

DEREVA WA LISSU ASAKWA
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Gilles Muroto amesema bado wanaendelea kumtafuta dereva wa Lissu, Simon Bakari Mohammed, huku akimtaka ajisalimishe katika kituo chochote cha polisi nchini.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini Dodoma jana, alisema wanaendelea kumtafuta dereva huyo kwa vile alikuwapo katika tukio la kupigwa risasi mbunge huyo.
“Bado hatujampata, lakini tunaendelea kumtafuta, popote alipo, tunamwambia tunamtafuta kwa kuvitumia vyanzo vyetu,” alisema.
Alipoulizwa kuhusu magari manane aina ya Nissan wanayoyashikilia kwa kuhusishwa na tukio hilo, Kamanda Muroto alisema bado wanaendelea kuyashikilia hadi watakapopatikana wahusika wa tukio hilo.
“Magari tunaendelea kuyashikilia, kikubwa tunataka usaidizi tuweze kuweka mambo yetu sawa,” alisema.
Kuhusu ulinzi nyumbani kwa Lissu, Kamanda Muroto alisema usalama upo wa kutosha baada ya polisi kuuimarisha.
“Pia tumeweka ‘road block’ (vizuizi), mji uko ndani ya bakuli, umezibwa na doria za magari na pikipiki, sehemu zote za kutoka na kuingia Dodoma zipo katika doria,” alisema.
Alipoulizwa ni kampuni gani inalinda katika eneo Lissu alipopigiwa risasi, alisema hawezi kujua ila anachojua ni kwamba kila nyumba ina mlinzi wake binafsi.
“Kila nyumba ina ulinzi binafsi, lakini ulinzi wa langoni upo kama kawaida, sema siwezi kujua ni kampuni gani inafanya ulinzi huo,” alisema.
MTANZANIA lilishuhudia gari la Lissu likiwa nje ya jengo la polisi likiwa limefunikwa upande ambao una matundu ya risasi, huku namba za gari hiyo zikiwa zimeondolewa.

WAOMBA MATUKIO YA KINYAMA YAKOME
Chadema, Mkoa wa Arusha jana walifanya maombi maalumu ya kumwombea Lissu yakiongozwa na Askofu Isaya Sizya wa Kanisa la FireAltar Ministry la Arusha.
Viongozi wengine wa dini ni pamoja na Ustadh Issa Juma na Mchungaji Nicholas Kissetu wa Kanisa la Shiloh Christian Ministries Tanzania.
Katika maombi hayo, Askofu Sizya, alisema wao kama viongozi wa dini wanaungana na watu wote kukemea vitendo vya kinyama na wanaomba Mungu matukio hayo yakome, yakiwamo utekaji wa watoto.
“Lengo kubwa ni kumwombea Lissu apone, Mungu akaushe majeraha ya ndani na nje, awe mzima kwa sababu ni raia wa Tanzania, anapaswa kuwa huru kiafya.
“Lissu tunajua yuko kwenye maumivu makali, yeye peke yake ndiye anaweza kuyasimulia, tushirikiane kwa maombi maalumu kwa Lissu,” alisema.
Kwa upande wake, Ustadh Juma, alisema Tanzania ilikuwa inajulikana kama kisiwa cha amani, ila vitendo vinavyoendelea hivi sasa vinatishia kutoweka amani.
“Tunalia kwa sababu amani inatoweka Tanzania, tunaogopa hata kutembea, tunakuomba Rais wetu Dk. John Magufuli utulinde, tunaomba uamuru jeshi lako litupe majibu ya kilichotokea kwa Lissu,” alisema.
Akitoa kauli ya kulaani shambulio la risasi dhidi ya Lissu, Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Arusha, Amani Golugwa, alisema tukio hilo la kinyama halitawatisha wala kuwanyamazisha.
“Waliopanga, waliojua mpango huo na aliyefyatua risasi na wanaomchukia Lissu, iwapo maisha yake yatakatishwa Mungu wa haki atawalipa sawasawa na ushetani wenu,” alisema.
Golugwa ambaye pia ni Katibu wa Chadema Kanda ya Kaskazini, aliwaomba wananchi wa mikoa ya Kanda ya Kaskasini kujitokeza kwa wingi kuchangia damu kwa ajili ya wagonjwa katika hospitali mbalimbali.

BAVICHA BUKOBA KUCHANGIA DAMU
Baraza la Vijana wa Chadema (Bavicha) Mkoa wa Kagera, limepanga kuchangia damu kupitia hospitali mbalimbali mkoani humo, kuunga mkono Watanzania waliojitokeza kuchangia damu iliyotumika kwa Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu.
Akizungumza kwa niaba ya Baraza hilo Mkoa wa Kagera, Mwenyekiti wa Bavicha Wilaya ya Bukoba, Ishengoman Audax, alisema uchangiaji damu utafanyika sambamba na maandamano ya amani kwa kila wilaya.
“Tuwe wazi… tukio hili lililomkuta Lissu ni la kinyama na halivumiliki kwa mtu yeyote, hivyo Serikali itusaidie kuwabaini watu wasiojulikana,” alisema Audax.
Habari hii imeandikwa NA JANETH MUSHI (ARUSHA), RENATHA KIPAKA (BUKOBA), RAMADHANI HASSAN (DODOMA) Na GURIAN ADOLF
(SUMBAWANGA)

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles