LONDON, ENGLAND
KLABU ya Swansea City imemteua Bob Bradley kuwa kocha mpya wa timu hiyo baada ya kuachana na kocha, Francesco Guidolin, kutokana na mwelekeo mbaya wa michezo ya Ligi Kuu England.
Bradley anakuwa kocha wa kwanza kutoka Marekani kufundisha Ligi Kuu England, baada ya klabu hiyo kuachana na mpango wake wa kumuajiri Ryan Giggs ambaye awali alikaribia kujiunga na klabu hiyo.
Bradley alipendekezwa na wamiliki wa klabu hiyo raia wa Marekani, Steve Kaplan na Jason Levien na kufanikiwa kutia saini ya mkataba wa miaka miwili na nusu ya kuifundisha timu hiyo.
Kitendo hicho ni pigo kwa kocha Giggs aliyekosa kibarua hicho kwa madai ya kukosa uzoefu wa kufundisha timu kubwa.
Msimu huu Swansea wamefanikiwa kupata pointi nne katika michezo saba waliyocheza, huku wakicheza chini ya kiwango.
Mwenyekiti wa klabu hiyo, Huw Jenkins, alisema klabu hiyo iliumizwa kutokana na kushindwa kwa kocha huyo wa zamani wa timu hiyo.
“Guidolin ni kocha mzuri kutokana na mafanikio aliyoyapata msimu uliopita licha ya kutokuwa katika kiwango bora, tulitakiwa kufanya mabadiliko chanya kwa maendeleo ya klabu.
“Tunapenda kumshukuru kwa mafanikio aliyoipa timu yetu na wafanyakazi wa klabu kwa mchango wake na tunamtakia mafanikio mema,” alisema.
Akimzungumzia Bradley, alisema uzoefu wa kocha huyo utaipa mafanikio zaidi klabu hiyo.
“Falsafa yake inafaa na itatufanya tuwe imara na kuwa na ushindani katika michezo ya Ligi Kuu England.
“Si kazi rahisi kubadili kocha kila wakati, lakini tunaangalia maisha ya baadaye ya klabu na mafanikio,” alisema.