31.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Bingwa Kombe la FA kumfunika wa Ligi

pg32*Atacheza mechi saba tu atanyakua mil. 50/-

 

NA ELLY MHAGAMA, DAR ES SALAAM

BINGWA wa mashindano ya Kombe la FA ‘Azam Sports Federation Cup’, anatarajia kumfunika vibaya bingwa wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, kwa fedha ya zawadi inayotolewa na wadhamini wa michuano hiyo.

Wakati wadhamini wa Ligi Vodacom wakitoa zawadi ya Sh milioni 70 kwa bingwa wake baada ya kucheza michezo 30, bingwa wa FA yeye anatarajia kuondoka na Sh milioni 50 baada ya kucheza michezo saba tu.

Mashindano ya FA kwa mwaka huu yamedhaminiwa na Kampuni ya Azam Media Limited, ambao wamesaini mkataba wa miaka minne na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), wenye thamani ya Sh bilioni 3.3 kudhamini mashindano hayo.

Hii ni mara ya kwanza kihistoria michuano ya Kombe la FA kuwa na udhamini, huku miaka ya nyuma imekuwa ikiibuka na ‘kuyeyuka’ tangu mwaka 1967 kabla ya kupotea moja kwa moja mwaka 2002.

Akizungumza  jijini Dar es Salaam jana, wakati wa hafla iliyofanyika kwenye  ukumbi wa mikutano wa kimataifa wa jengo la Kisenga LAPF, Kijitonyama, Dar es Salaam, Rais wa TFF, Jamal Malinzi, alisema amefurahia kufanikisha azma ya kurejesha mashindano hayo.

“Tumeona bingwa wa michuano hii apate Sh milioni 50 kwa sababu atakuwa amecheza mechi saba, yule wa Vodacom anayecheza michezo 30 anapata Sh milioni 70.

“Nitafurahi sana kuona klabu ya Daraja la Pili inashinda Kombe hilo, michuano hii ipo duniani kote, hivyo natamani klabu za chini ziwapige ‘visu’ wale wakubwa,” alisema Malinzi.Alieleza mbali na bingwa kutwaa kitita cha Sh milioni 50, kila timu itakayokwenda kucheza ugenini itapata Sh milioni tatu za safari na mwenyejii atapewa Sh milioni 1 ya maandalizi.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano ya TFF, Geoffrey Nyange ‘Kaburu’, alisema mashindano ya mwaka huu yatashirikisha klabu 64 na yataendeshwa kwa njia ya mtoano.

Kaburu, ambaye pia ni Makamu wa Rais wa Simba SC, amezitaja timu hizo kuwa ni pamoja na klabu 16 zinazoshiriki Ligi Kuu Bara, timu 24 za Daraja la Kwanza na idadi kama hiyo za Daraja la Pili.

Alisema mshindi wa kombe hilo atapata nafasi ya kuiwakilisha nchi katika michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika (CAF) mwaka 2017.

Alifafanua timu 16 za Ligi Kuu ya Bara zenyewe zitaanzia raundi ya pili, itakayoshirikisha klabu 32 na kuongeza kwamba wiki ya mechi za Kombe la FA hakutakuwa na michezo ya Ligi ya Bara.

Mara ya mwisho Kombe la FA lilifanyika mwaka 2002 na JKT Ruvu ya Pwani ikaibuka bingwa baada ya kuifunga Baker Rangers ya Magomeni kwenye fainali.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles