26.6 C
Dar es Salaam
Saturday, November 23, 2024

Contact us: [email protected]

Biashara ya unga balaa

Adamu Akida
Adamu Akida

*Mtanzania awekwa rehani Pakistan

Na Jonas Mushi, Dar es Salaam

NI biashara haramu ya unga, ndivyo tunavyoweza kusema baada ya kijana Mtanzania aliyejitambulisha kwa jina la Adamu Akida, mkazi wa Magomeni jijini Dar es Salaam kudai kutekwa nyara na kundi la maharamia nchini Pakistan.

Katika kile kinachoonekana kuwa ni dhuluma za kibiashara, inadaiwa kuwa Adamu alichukuliwa na mfanyabiashara mmoja anayejihusisha na biashara ya mihadarati, aliyemtaja kwa jina moja la Juma mkazi wa Kunduchi Dar es Salaam na kumweka rehani kwa maharamia hao, kwa ahadi kwamba angemfuata baada ya kumalizana nao kibiashara.

Taarifa zilizopatikana kwa watu wa karibu na Adamu  waishio Dar es Salaam, walisema kijana huyo alikwenda na mfanyabiashara huyo nchini humo, lakini baadaye alimwacha katika mikono ya maharamia hao kama dhamana ili baadaye awapelekee fedha zao.

Akitoa maelezo yake kwenye video ya sekunde 33  ambayo ilianza kusambaa juzi katika mitandao ya kijamii, Adamu anasikika akiomba msaada huku watu waliokuwa wamevalia mavazi ya ‘kininja’ wakiwa wamemshikia mitutu ya bunduki upande wa kushoto na kulia.

Katika video hiyo, kijana huyo alipofika katika eneo la kuanza kutaja mahali alipo watu hao walianza kumshambulia kwa mateke na ngumi, huku wakiahidi kutoa video nyingine ikionesha akiwa anachinjwa, iwapo fedha hazitatumwa.

Katika maelezo yake mafupi, Adamu alisema yupo Garita nchini Pakistani ambako aliachwa kama dhamana na mfanyabiashara huyo ambaye ni mkazi wa Kunduchi, jijini Dar es Salaam.

Kijana huyo alisikika katika video hiyo akitaja majina ya wazazi wake na eneo wanaloishi jijini Dar es Salaam pamoja na jina la mtu  huyo aliyemweka rehani ughaibuni.

“Nakaa Magomeni Mtaa wa Idrisa na Chemchem, Mama yangu anaitwa Rukia Daudi na baba yangu anaitwa Akida namwomba Juma ambaye mama yake anaitwa Mariamu alipe hela za watu kaniweka ‘Gerenta’ huku Juma anakaa Kunduchi,” alisikika kijana huyo akisema katika video hiyo huku watu hao wakimpiga alipoanza kutaja eneo alipo.

MTANZANIA yafika nyumbani kwao

Kutokana na video hiyo, gazeti hili lilifanya uchunguzi ili kubaini ukweli wa tukio hilo, ambapo lilifika Magomeni nyumbani kwao na Adamu na kukutana na mmoja wa ndugu zake ambaye alithibitisha taarifa hizo.

MTANZANIA lilifika Mtaa wa Idrisa na Chemchem nyumba namba 3 Kata ya Magomeni Manispaa ya Kinondoni  jijini Dar es Salaam, ambapo  majirani wa wazazi wa Adamu walisema wazazi wa kijana huyo wamehama na kumwacha baba yake mdogo aliyefahamika kwa jina la Kessy Baharia.

Baada ya kubisha hodi katika nyumba hiyo alitoka mwanamke aliyejitambulisha kwa jina la Khadija Katundu, ambaye ni mke wa Baharia.

Baada ya kuulizwa kama anamfahamu Adam ambaye ametekwa nchini Pakistani, Khadija alikiri kumfahamu na kusema kuwa ni mtoto wa shemeji yake, Akida (baba wa Adamu).

Mama huyo alisema, kwa sasa mzee Akida haishi katika nyumba hiyo kwani alishaiuza na kuhamia Bagamoyo mkoani Pwani.

“Hapa ni nyumbani kwao Adamu kwa sababu alizaliwa hapa na kukulia hapa, lakini baadaye nyumba hii iliuzwa na aliyenunua ni baba yake mdogo ambaye ndiye mume wangu,” alisema Khadija.

Maisha yake

Alipoulizwa wanapoishi wazazi na ndugu wa kijana huyo alisema baada ya nyumba hiyo kuuzwa uliibuka mgogoro baina ya ndugu hao na kusababisha wazazi wa kijana huyo kuondoka bila kuaga na kwamba hawana mawasiliano hadi sasa zaidi ya kusikia kuwa walihamia Bagamoyo.

Kuhusu anavyomfahamu Adamu, Khadija alisema kijana huyo ni kinyozi na ana mke na watoto wawili ambao walikuwa wanaishi bonde la Mkwajuni ambalo hivi sasa nyumba katika eneo hilo zimebomolewa, hivyo kwa sasa hajui mahali wanapoishi.

Polisi wafika

Taarifa za mkanda huo wa video zimelishtua Jeshi la Polisi ambapo tayari askari polisi jana walifika katika nyumba hiyo na kumuhoji mama huyo kuhusu Adamu na kumwonyesha video hiyo.

“Nilikuwa nasikia tu lakini sikuamini sana lakini leo (jana) askari walifika hapa na kunihoji na wakanionyesha video hiyo ndiyo nikaamini kuwa ni kweli Adamu ametekwa,” alisema  Khadija.

Kuhusu watu waliotajwa na kijana huyo kwa jina la Juma na mama yake Mariamu, alisema hawafahamu watu hao.

Akielezea hisia zake baada ya kupata taarifa za kijana huyo alisema anasikitika sana na kwamba kijana huyo yupo katika hatari ya kuuawa kama suala hilo halitapewa uzito na kufuatiliwa kwa kina.

“Kwakweli nimeshtushwa sana na taarifa hiyo na nilivyomwona Adamu yupo katika hatari ya kuuliwa kama hatofuatiliwa lakini naamini kwa sababu suala hili limekwisha enea dunia nzima ufumbuzi wake utapatikana na wazazi wake watajulikana walipo,” alisema Khadija.

MTANZANIA ilipomtafuta Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa, Balozi Dk. Augustine Mahiga, hakupatina. Hata hivyo  mmoja wa maofisa wa Kitengo cha Habari katika wizara hiyo, alisema hawezi kuzungumzia suala hilo kwani yupo likizo.

“Mimi niko likizo na leo ni ‘wekiend’ (mwisho wa wiki) binafsi siwezi kulisemea suala hilo sina taarifa rasmi juu ya suala hilo,” alisema ofisa huyo ambaye aliomba asitajwe jina lake gazetini.

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba hakupatikana kwani simu yake iliita kwa muda mrefu bila kupokewa na baadaye alituma ujumbe mfupi wa simu kwamba yupo kikaoni.

Hata alipotumiwa ujumbe mfupi wa simu ili kutoa ufafanuzi kuhusu suala hilo hakujibu hadi tunakwenda mitamboni.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles