31.2 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

Biashara ya Mifugo Kaliua yaingiza Bilioni 5.2

Na Allan Vicent, Kaliua

USIMAMIZI mzuri na maboresho ya miundombinu ya mifugo wilayani Kaliua Mkoani Tabora umeleta neema kubwa kwa wafugaji baada ya mauzo ya mifugo yao kuongezeka hadi kufikia sh bil 5.2 hivi karibuni.

Hayo yamebainishwa juzi na Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya hiyo, Jafael Lufungija alipokuwa akiongea na Wataalamu, Watendaji na madiwani katika ukumbi wa mikutano wa halmashauri hiyo.

Alisema kuwa usimamizi mzuri wa minada na maboresho ya huduma kwa mifugo yameleta neema kubwa kwa wafugaji ambapo kwa mwaka huu pekee jumla ya ng’ombe 22,854, mbuzi 8,869, kondoo 896 na nguruwe 34 waliuzwa na kuingizia wafugaji kiasi cha sh bil 5.2.

Alitaja minada hiyo kuwa ni Upele, Mkuyuni, Wachawaseme, Zugimlole, Mwamnange, Ulyankulu na King’wangoko ukiwemo mnada wa Ugansa ambao ukarabati wake unaendelea na unatarajiwa kugharimu kiasi cha sh mil 35.

Lufungija alisisistiza kuwa katika kuongeza ustawi na afya ya mifugo katika wilaya hiyo halmashauri imetoa elimu ya uogeshaji mifugo ambapo jumla ya ng’ombe 3,065, mbuzi 908, kondoo 165 na mbwa 5 waliogeshwa huku ng’ombe 1,805, mbuzi 403, kondoo 131, mbwa 22, nguruwe 60 na kuku 5,270 wakinyunyiziwa dawa.

Aliongeza kuwa wanavijiji 15 wamepewa elimu ya ufugaji bora wa samaki kwenye mabwawa ya kuchimba na kujengewa ili kuwainua kiuchumi na kuongeza mapato ya halmashauri.

Lufungija alibainisha kuwa dhamira yao ni kuhakikisha halmashauri hiyo inakuwa mfano wa kuigwa kwa kuzalisha idadi kubwa ya mifugo na kuwa miongoni mwa wazalishaji wakuu wa maziwa, nyama na ngozi.

Halmashauri ya wilaya ya Kaliua mkoani Tabora ni miongoni mwa halmashauri zenye mifugo mingi hapa nchini, ambayo imetambua umuhimu wa sekta hiyo na kutumia wataalamu wake ipasavyo kwa lengo la kuboresha mifugo na ufugaji.

Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri hiyo Jerry Mwaga alibainisha kuwa wameanzisha program ya kutoa elimu ya ufugaji bora na wa kisasa kwa wakulima ili kuhakikisha uzalishaji wa mifugo unaongezeka.

Alifafanua kuwa tayari wameanzisha mashamba darasa ya ufugaji wa kisasa ambapo baadhi ya wafugaji walioko vijijini wamepewa elimu na kuanza kufuga kwa kutumia ng’ombe wa kisasa ambao wanatoa maziwa mengi.

Alisisitiza kuwa kupitia mkakati huu, wafugaji watapata maziwa mengi ambayo watayatumia kama lishe na biashara, pili watapata kitoweo cha nyama na kuuza na kupata faida kubwa tofauti na zamani.

Aliishukuru serikali ya awamu ya 6 kwa kuendelea kuleta fedha nyingi kwa ajili ya kuboresha utoaji huduma katika  sekta za afya, elimu, barabara na sekta ya mifugo na uvuvi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles