26.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, April 17, 2024

Contact us: [email protected]

Sekta ya mifugo inavyonufaisha wafugaji Kaliua

Na Allan Vicent, Tabora

SEKTA ya mifugo ni miongoni mwa sekta zenye mchango mkubwa sana katika suala zima la maendeleo ikiwemo kuinua maisha ya wakulima na wafugaji na kuongeza mapato ya serikali.

Lakini mifugo pasipo wafugaji ni kama gari pasipo mafuta, hivyo ndivyo ilivyo kwa maeneo mengi hapa nchini, ambapo watu wanathamini mifugo pasipo kumthamini mfugaji na kumwekea mazingira mazuri ya shughuli yake.

Halmashauri ya wilaya ya Kaliua mkoani Tabora ni miongoni mwa halmashauri zenye mifugo mingi hapa nchini, ambayo imetambua umuhimu wa sekta hiyo na kutumia wataalamu wake ipasavyo kwa lengo la kuboresha mifugo na ufugaji.

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Jerry Mwaga, akiongea na Mtanzania Digital amebainisha kuwa wameweka program ya kutoa elimu ya ufugaji bora na wa kisasa ili kuhakikisha uzalishaji wa mifugo unaongezeka.

Anabainisha kuwa tayari wameanzisha mashamba darasa ya ufugaji wa kisasa ambapo baadhi ya wafugaji walioko vijijini wamepewa elimu na kuanza kufuga kwa kutumia ng’ombe wa kisasa ambao wanatoa maziwa mengi.

Anasisitiza kuwa hili limeleta neema kubwa kwa wafugaji, kwani wana uhakika wa kupata maziwa mengi ambayo wanayatumia kama lishe na biashara, pili wanapata kitoweo cha nyama na kuuza na kupata faida kubwa tofauti na zamani.

“Elimu hii ni endelevu, tunataka wafugaji wote waliopo vijijini hadi mjini katika wilaya yetu waige kutoka kwa wenzao ili waanze kufuga kisasa ili kunufaika zaidi na mazao yatokanayo na mifugo na halmashauri pia ipate mapato,” anasema.

Mwaga anabainisha kuwa mifugo ni rasilimali yenye manufaa mengi, ikisimamiwa ipasavyo na wafugaji wakapewa elimu na kuwekewa mazingira mazuri inaweza kuifanya sekta hiyo kuwa ya kwanza kwa kuliingizia mapato mengi taifa na kubadili historia ya mifugo na ufugaji hapa nchini.

Anaongeza kuwa wafugaji wengi hapa nchini wanafuga kwa mazoea na hawajasaidiwa vya kutosha, ikiwemo kuwekewa mazingira mazuri ili mifugo yao ilete tija katika maisha yao na kuongeza mapato ya serikali.

Mwenyekiti wa halmashauri hiyo, Jafael Lufungija anafafanua kuwa mbali na kuboresha mifugo na ufugaji pia wamedhamiria kuboresha miundombinu na kusimamia ipasavyo masoko ya mifugo kwenye minada.

Anaeleza kuwa katika kuongeza ustawi na afya ya mifugo katika wilaya hiyo wametoa elimu ya uogeshaji mifugo ambapo jumla ya ng’ombe 3,065, mbuzi 908, kondoo 165 na mbwa 5 waliogeshwa huku ng’ombe 1,805, mbuzi 403, kondoo 131, mbwa 22, nguruwe 60 na kuku 5,270 wakinyunyiziwa dawa.

Aidha, anaongeza kuwa wanavijiji 15 wamepewa elimu ya ufugaji bora wa samaki kwenye mabwawa ya kuchimba na kujengewa ikiwemo kuboresha na kusimamia minada ya mifugo kwa kuboresha afya za mifugo na kuongeza mapato ya halmashauri.

Anataja minada hiyo kuwa ni Ugansa, Upele, Mkuyuni, Wachawaseme, Zugimlole, Mwamnange, Ulyankulu na King’wangoko ambapo jumla ya ng’ombe 22,854, mbuzi 8,869, kondoo 896 na nguruwe 34 waliuzwa na kuingizia wafugaji kiasi cha sh bil 5.2.

Mwenyekiti anabainisha kuwa dhamira yao ni kuhakikisha halmashauri hiyo inakuwa mfano wa kuigwa hapa nchini kwa kuzalisha idadi kubwa ya mifugo na kuwa miongoni mwa wazalishaji wakuu wa maziwa, nyama na ngozi.

Wafugaji waeleza manufaa wanayopata

Wiliam Luhemeja (76) mfugaji mkazi wa kijiji cha Mtakuja-Igagala kata ya Igagala wilayani humo anaipongeza halmashauri kwa mikakati yao mizuri kwani itawasaidia kuacha kufuga kienyeji hivyo kupata manufaa makubwa.

Anaeleza kuwa baada ya kupata elimu ya ufugaji bora wa kisasa ameanza kunufaika, kwani awali alikuwa akipata lita 100 tu za maziwa lakini sasa anakamua lita kati ya 500 hadi 1000 kwa siku na zinaongezeka zaidi.

Anaongeza kuwa awali wafugaji walikuwa hawathaminiwi licha ya mifugo yao kuwa na thamani na kuingiza mapato mengi, na kubainisha kuwa sasa heshima ya mfugaji itarudi kama mkakati huu utasimamiwa vizuri.  

Lusubilo Makaranga (59) mkulima mkazi wa Kijiji cha Kamsekwa anaeleza kuwa malengo ya halmashauri ni mazuri sana ila akaomba utaratibu mzuri uwekwe ili kila mfugaji apate ng’ombe wa kisasa na elimu hiyo iwafikie wote.

Anasisitiza kuwa ufugaji wa kisasa utasaidia kumkomboa mfugaji aliyekuwa akiishi kama mkimbizi kwenye nchi yake kwa kuhamahama kila kukicha, licha ya kupaza sauti kwa muda mrefu ikiwemo kufanya mikutano na viongozi wa serikali.

Mwenyekiti eleza mikakati ya baadae

Lufungija anadokeza kuwa halmashauri imejipanga vizuri ili kuhakikisha mkakati huo unawafikia wafugaji wote popote walipo katika wilaya hiyo, anatoa wito kwa Watalamu kwa kushirikiana na Madiwani na Watendaji wa Vijiji na Kata kukaa na wafugaji katika maeneo yao ili kufikisha elimu hiyo katika vijiji vyote.

Anabainisha mikakati ya baadae kuwa ni kujenga viwanda vya kuchakata mazao ya mifugo ambavyo ni pamoja na kiwanda cha maziwa, nyama na kuchakata ngozi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles